TAMKO la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU) kuwa Taasisi hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya mfanyabiashara Haruni Daudi Zacharia limeibua mapya.
Zacharia, ambaye ni mfanyabiashara maarufu na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Al-Naeem yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa sukari hapa nchini na anayetuhumiwa kuficha bidhaa hiyo
TAKUKURU imebaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza sukari iliyokutwa katika maghala hayo kulikofanywa na mfanyabiashara huyo kwani hata sehemu ya Maghala ilipo sukari hiyo hapakuwa na dalili za upakiaji wa sukari hiyo ili iweze kusambazwa
Katika eneo la Kitumbini kumekuwa na wananchi wengi wanaohitaji bidhaa hiyo na wachache sana waliweza kuuziwa licha ya ukweli kwamba sukari ilikuwepo.
Kumekuwepo na mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na mfanyabiasha huyo kwa kununua sukari yote toka viwanda vya ndani na kisha kuihifadhi na kuuza bidhaa hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku wakati alikuwa na uwezo wa kuuza zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari katika soko.
Taarifa zaidi zinaeleza kufichuka kwa habari, ambayo kwa muda mrefu gazeti hili lilikuwa linaeleza namna mchezo unavyofanyika kwa mfanyabiashara huyo mwenye asili ya kiasia na mwenzake ambaye Salim Turk. Turk ni mbunge wa CCM katika jimbo la Mpendae Zanzibar.
Turk anatajwa kuwa mbia mkubwa wa mfanyabiashara huyo, na anadaiwa kuwa amekuwa akitumia nafasi yake ya ubunge kujinufaisha kibiashara hasa katika sekta ya sukari kwa muda mrefu.
Taarifa ambazo Jamvi La Habari imezipata zilieleza kuwa aliingiza tani 20000 kimagendo kutoka nje kwa kushirikiana na mfanyabiashara huyo, ambaye hivi sasa anachunguzwa na TAKUKURU kutokana na kitendo cha kuficha sukari.
Wafanyabiashara hao , wamekuwa wakiidanganya serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Nchini(TRA) kwamba inaingiza sukari inayopitishwa kwenda nchi jirani na badala yake wanaiingiza nchini na kuendelea kuiuza sukari ambayo inaelezwa pia inaweza ikawa haina ubora.
Licha ya Turky na Zacharia kuhusishwa katika suala la sukari, ambapo inaelezwa kuanzia mwaka 2009 mpaka 2012 pekee, zaidi ya Bilioni 462 zimepotea kwa udanganyifu wa wafanyabishara hao kwa kukwepa kodi.
Vilevile taarifa zinasema, kwa miaka kadhaa sasa, serikali imekuwa ikipata hasara ya kukwepwa kodi kwa zaidi ya bilioni 300 kila mwaka kunakofanywa na wafanyabiashara hao
Taarifa zaidi ilizozipata JAMVI LA HABARI, zinaeleza kuwa, uingizaji huo holela wa sukari nchini, unaenda sambamba na uamuzi wa serikali ya awamu ya nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete iliyoamua kutoa vibali kwa wafanyabiashara wachache nchini ili waruhusiwe kuagiza sukari kutoka nje, ambapo suala nzima la ugawaji wa vibali hivyo lilikuwa na utata mkubwa.
Inaelezwa kuwa suala hili la ugawaji wa vibali vya sukari, liliondolewa katika Wizara ya Kilimo na Chakula na kupelekwa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ilikuwa inashughulika na ugawaji wa vibali hivyo.
“Huu ni mchezo na taifa linakosa mapato mengi. Dalali wa vibali hivyo alikuwa mmoja wa mameya wa jiji la Dar es Salaam aliyekuwa anawapeleka wafanyabiashara mbalimbali kupata vibali vya kuagiza sukari nchi za nje,’’kilisema chanzo chetu cha habari.