RC Makalla ajitambulisha na kusema ‘Sitaki majungu, nimekuja kufanya kazi’

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
Ni maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla katika mikutano aliyoifanya alipokutana na wakazi, uongozi na watumishi wa halmashauri na wilaya za mkoa wa Mbeya kujitambulisha. Makalla anasema maana ya falsafa hiyo aliyoitoa kwenye kitabu kitakatifu kinachotumiwa na waumini wa dini za Kikristo yaani Biblia ni kuwa hakuna jipya analokuja nalo bali kuhakikisha yale yanayopaswa kufanyika kila siku yanafanyika ipasavyo.

Katika kujitambulisha kwake amesisitiza masuala kadhaa likiwemo la kutorithi fitina na majungu aliyoyakuta akisema hayamhusu kwani amekuja kufanya kazi. “Ndugu zangu mie sijaja kurithi mifarakano wala majungu. Nimekuja kupiga kazi. Kama mna figisu figisu vyenu mimi sivitaki. Nimekuja kufanya kazi na kila mtu, mimi ni wa wote.”

“Haihitaji kuwa na digrii kujua Makalla anatokana na chama gani lakini sikuja hapa kuwatumikia wana CCM pekee. Hata ukiwa diwani wa Chadema iwapo unaona kuna shida inayohitaji kuitatua kwa pamoja wewe niite nitakuja.Tupo kuwatumikia wananchi wetu wala siyo vyama,” anasema Makalla.

Makalla anasema hapendi kuona wananchi wakipata taabu ya kusafiri umbali mrefu kutoka vijijini kwenda ofisini kwake kupeleka matatizo ambayo yangetatuliwa na viongozi waliopo walikotoka. Ili kukabiliana na changamoto hiyo tayari ameagiza wakuu wa wilaya zote kutenga siku ya Alhamisi kusikiliza kero kutoka kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya husika na wataalamu wengine watakaa ukumbini kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana kuwasikiliza wananchi. Viongozi wa kata na vijiji wameagizwa kuwa na madaftari maalumu kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za kero za wananchi. Hii itasaidia kila ngazi ya uongozi kuwajibika katika utatuzi wa kero hizo na kuleta tija katika jamii.

“Haiwezekani kero ya kumalizwa na mwenyekiti au mtendaji wa kijiji mwananchi asafiri nayo mpaka kwa mkuu wa mkoa,hawa wanafanya nini. Kero za kuishia kwa mwenyekiti wa kijiji ziishie huko, za mtendaji wa kata au diwani ziishie huko, kama inamhusu DC na wataalamu wake waishughulikie,” anasema Makalla. “Mwananchi atakapokuja kwangu nitamuuliza ulikwenda kwa mwenyekiti wa kijiji? Kama hakupita nitamrudisha na akaanze upya, kama alipita huko kote na hakusikilizwa nitakuja mwenyewe.”

“Nitafanya pia ufuatiliaji wa agizo hili kwa kushtukiza, siwezi kutaja tarehe nitakayofika, kijiji nitakachokuta uongozi hausikilizi kero za wananchi sintoangalia serikali ya hapo imeundwa na chama gani nitavunja uongozi tupate viongozi wapya,” anasema Makalla. Makalla anasema tabia ya viongozi wa chini kutowajibika katika kutafuta ufumbuzi wa kero za wananchi ndiyo unaosababisha serikali kuchukiwa.

Anasema uzembe huo unasababisha pia msongamano wa kero za wananchi kwa viongozi wa juu. Anataka kero zinazomfikia ziwe na uzito unaolingana na nafasi yake na kama naye zinamzidi basi atalazimika kuziwakilisha juu yake. “Hatuwezi kubaki tunawasikia wananchi wetu wanapiga kelele….Tunamhitaji Magufuli aje hapa!...Tunamtaka Majaliwa aje tuongee nae…hivi sisi hatupo? Mimi nasema ninatosha, tutabanana hapa hapa wananchi watimiziwe,” anasema Makalla.

Usafi

Kwa suala la usafi, anasema hatovumilia kuona miji inakuwa michafu na kupoteza sifa yake ya kutoka katika mkoa wa Kilimanjaro unaoongoza kwa usafi nchini. “Nimehamia Mbeya nikitokea mkoa wa Kilimanjaro ambao hakuna asiyeijua sifa yake. Kila siku mmekuwa mkisikia Moshi umekuwa mji wa kwanza kwa usafi...sasa sitaki kuona nimehamia kwenye mkoa mchafu.”

“Usafi uanzie nyumbani kwa kila mmoja wetu. Niwapongeze watu wa Kyela mmefanikiwa kumaliza tatizo la kipindupindu. Sasa sitaki kusikia tena ugonjwa huu. Viongozi wa dini na wazee maarufu tusaidieni kulisisitiza jambo hili,” anasema.

“Katika harakati za kupinga kipindupindu hatuhitaji kuingiza tofauti za kiitikadi. Hauwezi kusema kipindupindu kinakuja kuua watu wa CCM. Kikija hakichagui huyu wa CCM wala Ukawa,” anasema Makalla. “Na kipindupindu si sawa na kuandama kwa mwezi. Mwezi ukiandama mtasema na sisi tumeuona huku ...mnafurahia kwa kuwa kesho yake inakuwa sikukuu. Lakini hauwezi kusema jamani na sisi huku tumekiona kipindupindu. Si jambo la kufurahia mkikiona mkifurahia mjue kinachofata ni kifo,” anasema.

Matumizi ya vyoo

Anasema matumizi ya vyoo bora ni jambo muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huo. Anasema yapo mazoea ya baadhi ya wakazi hususan katika wilaya za Kyela na Rungwe huchimba mashimo kwenye mashamba ya mikokoa na kahawa na kujisaidia kisha wanafukia. Makala anasema, hivyo si vyoo vinavyohitajika hivyo ni lazima vijengwe vyoo bora.

Taarifa ya mapato

Anasema kutosomewa taarifa ya mapato na matumizi, kunasababisha pia wananchi kukosa imani na serikali yao. Wananchi wanahusishwa katika mradi wa kwanza na wanashiriki wakati mwingine hata kwa kuchangia mpaka unakamilika. Kabla hawajasomewa taarifa ya mradi huo wanafuatwa na kuambiwa mradi mwingine hivyo kusababisha maswali mengi.

“Viongozi wa vijiji na kata hakikisheni mnaweka wazi taarifa za mapato na matumizi ya miradi. Hii itasababisha wananchi kutambua nini kilikusanywa na matumizi yake yamekwenda vipi. Hata unapowafuata kwa ajili ya mradi mwingine itakuwa rahisi kwa kuwa wanaelewa hakuna unachowaficha,” anasema Makalla.

“Wakati mwingine tunatengeneza ugumu wa mambo kutokana na kutokuwa tu wawazi kwa wananchi. Ukimuuliza mwananchi kwa nini unaichukia serikali anakwambia tulichangia mradi hatujui pesa zetu zilitumika vipi. Mwingine atakwambia niliomba cheti cha kuzaliwa cha mtoto wangu mpaka leo sijapata. Vitu vidogo vinasababisha serikali ichukiwe,” anasema.

Upungufu wa madawati

Makalla anasema ni muhimu kila halmashauri itekeleze agizo la kukamilisha utengenezaji madawati kulingana na mahitaji yaliyopo kwenye eneo husika. Licha ya kuwa sera ya elimu bure imeongeza changamoto ya madawati lakini halmashauri lazima ziangalie zinatumia vipi mapato ya ndani kukamilisha jambo hilo. Ushirikishwaji wa sekta na watu binafsi ni muhimu pia.

Anasema suala la madawati linapaswa kwenda sambamba na harakati za kutokomeza ndoa za utotoni zinazosababisha watoto hususani wa kike kukosa elimu. Wakati akiwa kijijini Luhanga wilayani Mbarali anawataka wafugaji kuacha tabia ya kuozesha mabinti wadogo na kuwasababishia kushindwa kuendelea na masomo. Makalla anasema, vitendo hivyo vinasababisha kata ya Luhanga kuwa na udumavu kielimu kwani hata matokeo ya mitihani ya kitaifa yanaonesha kata hiyo kutofanya vizuri.

“Elimu ndiyo urithi pekee ulio bora kwa mtoto. Hata uwe na ng’ombe wengi,majumba mengi,vinaweza haribika wakati wowote na ukamwacha mtoto kwenye mazingira magumu iwapo haukumpa elimu,” anasema.

Kujiajiri

Makalla anasema, hatopenda kusikia miongoni mwa halmashauri zilizoshindwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya akinamama na vijana inatoka kwenye eneo lake la utawala. Anawataka madiwani kusimamia asilimia hiyo ya mapato ya ndani inatolewa mikopo kwa vijana na wanawake ili waweze kupata msingi wa kuinua uchumi wao. Makala amewaonya wananchi sambamba na viongozi hususani wa vijiji na kata kuachana na tabia ya kuuza ardhi ovyo.

Anasema wanapaswa kutambua kuwa watu wanaongezeka lakini ardhi inabaki kuwa ile ile hivyo kuuza hovyo hovyo kunasababisha wakazi husika kukosa maeneo kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwemo kilimo. Makalla anasema, kwa sasa serikali inahimiza kila mtu kujituma katika kazi lakini iwapo hakuna maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo vijana watakuwa wanaonewa pale inaposisitizwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu. Anasema uhakika wa kusimamia hayo yote anao kwa kuwa hajaja Mbeya kujifunza uongozi.
 
Hivi karibuni niliona kwenye vyombo vya habari kuwa alitofautiana na meya wa jiji lake kwa kile meya alichokiita dharau.

Mkuu wa mkoa alitembelea miradi ya halmashauri bila kuona umuhimu wa kuambatana na meya.

Kama wamshamaliza tofauti zao itakuwa rahisi kutekeleza haya aliyoyasema kwa manufaa ya wananchi wa Mbeya; tofauti na hivyo, atakuwa mnafiki!
 
Kama anataka kufanya kazi na watanzania asiyaogope majungu, kwa watanzania majungu ni sehemu ya maisha kwa kiingereza tunaita propaganda na sio ghossip
 
Back
Top Bottom