Cuba. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo huu ni msemo ambao umekamilika kwa Makamu wa rais nchini Cuba, Miguel Díaz-Canel, anayetajwa na viongozi wa ngazi za juu nchini humo kuwa ndiye kiongozi mtarajiwa.
Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye aliandaliwa kwa muda mrefu kushika wadhifa huo anatajwa kumrithi ama kuchukua nafasi ya Raul Castro.
Miguel (55) ambaye kwa taaluma ni mhandisi anatarajiwa kuchukua ofisi baada ya zoezi la upigaji kura rasmi na mkutano wa kitaifa kuidhinisha uteuzi wake.
Makabidhiano ya madaraka yatahitimisha miongo sita ya utawala wa Castro na ndugu yake marehemu Fidel, ambaye aliongoza mapinduzi ya mwaka 1959.
Diaz-Canel huonekana kama huria kijamii na mtaalamu wa teknolojia mpya ingawa hatazamiwi kumaliza mfumo wa chama kimoja nchini humo, lakini ni mapema mno kumuweka katika nafasi ya namna hiyo kwa sasa.
Raul Castro ataendelea kuwa kiongozi mkuu wa Chama cha Kikomunisti mwaka 2021 mpaka mkutano mkuu ujao na anatarajiwa kuendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika jamii yake.
Kiongozi huyo ambaye tangu ateuliwe kuwa Makamu wa rais wa baraza la Congress la Cuba 2013 alikuwa mtu wa karibu zaidi na Castro.
Mwanasiasa huyo mkongwe alizaliwa Aprili, 1960 mwaka mmoja baada ya Fidel Castro alipokula kiapo cha kushika nafasi ya waziri mkuu.
Dioaz-Canel alisomea masuala ya uhandisi wa umeme na kuanza harakati za kisiasa mapema akiwa na miaka 20 akiwa mwanachama wa chama cha Kikomunisti.
Chanzo: MCL