Rais Kikwete: umma unataka vitendo

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,039
Nkwazi Nkuzi
Tanzania Daima


VYOMBO ya habari viliripoti na kumkariri Rais Jakaya Kikwete akifanya kile vyombo vya habari vilikiita msimamo juu ya tuhuma za ufisadi zinazoikabili serikali, chama na maofisa wake waandamizi.

Tangu aingie madarakani miaka zaidi ya miwili iliyopita, Kikwete amewatia watu matumaini, kutoa ahadi, kuwa mpole na anayejali lakini asiyetekeleza kitu.

Hapa kinachotakiwa ni kwa Kikwete kuuhakikishia umma kuwa hatarudia mchezo ule ule wa kutoa kauli tamu na kuwasahaulisha. Umma umechoka na sasa unataka vitendo.

Kitu kingine ambacho vyombo vya habari vilisema ni kujibu mapigo ni nukuu ifuatayo:

"Hauwezi kuwa wewe ni mpelelezi, mwendesha mashitaka na hakimu. Ndiyo maana katika utawala wa sheria, mambo haya yanatenganishwa… lakini tukienda na tabia kuwa niliyemtaja mimi basi, huyo ana hatia, si sawa… tukiendesha nchi yetu hivyo tunaipeleka pasipo," Rais Kikwete alisema.

Kauli hii ya rais kweli inashangaza. Je, tabia ya mtu kuwa yeye katika vyote, inakuwa mbaya inaposhutumiwa serikali? Kama ni mtu kuwa yote katika yote kwenye kesi mbona serikali ndiyo bingwa wa mchezo huu? Au ni yale yale ya jogoo kuwafundisha vifaranga kujisaidia ndani halafu akajifanya hayumo?

Tumpe rais mfano wa hivi karibuni. Serikali ilipoletewa uchafu wa Richmond hata BoT, ikiwa kama mshutumiwa kutokana na kile wanasheria hukiita ‘vicarious responsibility’, sina Kiswahili chake, niseme uwajibikaji wa kiuwakilishi, badala ya kuruhusu Bunge ambalo lilikuwa limepokea kesi hizi, iliziteka na kupiga mizengwe hadi kuamuru TAKUKURU ichunguze.

Nakumbuka jinsi Waziri wa Fedha Zakia Meghji na Waziri Mkuu, Edward Lowassa walivyohangaika kukanusha kashfa ya Benki Kuu (BoT), huku wakitoa maelezo yasiyoshawishi badala ya gavana mwenyewe aliyekuja kujibu kwa kebehi na nje ya mada kiasi cha kuwaacha wananchi wamechukia na kushangaa!

Iulize serikali tangu zengwe hili lipigwe ni kitu gani kimefanyika? Wanaoituhumu serikali na maafisa wake wameona mchezo huu wa hovyo na mchafu kiasi, kama vifaranga na jogoo, kuamua kutumia wembe ule ule ili jogoo aone madhara yake.

Kitu kingine kilichofanya hali hii inayomkera rais ni ukweli kuwa vyombo husika vimeshindwa kutimiza wajibu wake. Chukulia kwa mfano kesi ya mbunge mmoja ambaye uchunguzi wa polisi ulithibitisha kuwa alighushi vyeti, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Badala ya serikali kumfikisha mahakamani, ilijitoa, kiasi cha walalamikaji kwenda wenyewe mahakamani, ambako nako haki imekuwa haba.

Mbona sheria ya nchi iko wazi kuwa atakayeshughulika na kupeleka mashitaka yote ya jinai mbele ya mahakama ni serikali? Je, kwenye sakata kama hili rais anategemea wahusika wafanye nini?

Mfano mwingine ambao ni aibu kwa nchi na watu wake ni mazoea ya kinyama ya kuwachoma moto vibaka. Kama tunakuwa wakweli na kuweka mbali sanaa na siasa, ni ukweli usiopingika kuwa ulegelege wa Jeshi la Polisi katika kupokea malalamiko na kuyafikisha mahakamani hata kuyachunguza umewafanya wananchi wakose imani na taasisi hii kiasi cha kugeuka wauaji.

Rais anajaribu kukumbusha utawala wa sheria ambao kwa Tanzania ni ngano za kwenye vitabu tu. Kama kweli kuna utawala bora, mbona rais amepigiwa kelele tangu siku aliyoingia madarakani juu ya kuwateua wabunge ambao ni wawakilishi wa watu kuwa mawaziri, kwamba ni kuwanyima wananchi haki yao hata kuwaibia mwakilishi wao na hajafanya kitu?

Bahati nzuri juzi juzi hata malaika wameingilia pale Ukerewe kijana Aaron Wambura, alipoamua kulazimika kubeba zigo la watu wazima baada ya kuona hawasikilizwi kwa kuhoji jinai hii.

Kuonyesha kuwa utawala wa sheria ni gea za majukwaani, hata aliyeulizwa, yaani Waziri Mkuu Edward Lowassa hakujibu zaidi ya kuacha vyombo vya usalama vimsumbue mtoto wa watu na wazazi wake!

Turejee kwa serikali. Mbona wabunge walipotaka kuona kilichomo kwenye mikataba ya madini ambayo ndicho chanzo kikuu cha hiki kinachomkera Kikwete, ikiwa ni haki yao kisheria, serikali ilikataa kwa kutoa sababu za ovyo? Hapa inajenga picha gani?

Rais anaona kama wapinzani walioshupalia uoza ndani ya serikali yake wana kimbelembele kutaka kufanya yote. Rais alitegemea wafanye nini kama serikali waliyoamishwa kuwa ingepambana na ufisadi haipambani nao bali kuupamba?

Je, rais hajui kuwa wapinzani wanajua kuwa mahakama stahiki na ya haki ni wananchi ambao wanachezewa Mahepe?

Maana kama serikali ingekuwa inawajibika vilivyo hata wananchi wangewauliza wapinzani ni kwanini wanakwenda kwao wakati serikali yao iko makini?

Kuna uwezekano mkubwa ushauri wa rais kupuuzwa kutokana na historia ya utendaji mbovu na wa kuchelewa wa serikali yake na watu wake.

Kitu kingine ambacho kimsingi kimefanya kadhia hii kutokea ni ukweli kuwa rais amepuuzia ushauri mwingi na wa maana kwa muda mrefu.

Mfano, ameonywa mara nyingi kujizungushia marafiki na wasaka ngawira, amepuuza. Hapa alishauriwa avunje baraza la mawaziri na kuwawajibisha watuhumiwa au kuwapa nafasi ya kusafishwa kisheria.

Hii ikichangiwa na hali ya serikali kuundwa na chama ambacho kimeanza kuparaganyika na kukosa mwelekeo ambapo turufu yake kuu ni kujuana na kulindana, ndipo imani ya umma inafutika kabisa.

Tumalizie kwa kuuliza. Je, kwanini rais amechelewa kutoa msimamo na ushauri wake hadi mambo yaonekane kuanza kuharibika kiasi cha pesa ya umma kuanza kutapanywa kutibu madhara ya ukimya wake?

Arejee kinachoitwa kutafsiri bajeti, ambapo mawaziri wake wamechemsha kwa kusema kinachodaiwa na upinzani ni umbea mtupu. Je, kama kweli ni umbea, serikali inapata wapi muda wa kuchunguza umbea?

Je, ni umbea au wambea ni wale wanaosema ni umbea? Je, serikali ya namna hii ambapo kila mtu anajisemea lake bado ina udhu na ithibati ya kuwaaminisha wananchi kuwa inaweza kutatua matatizo yao?

Kama rais anataka wananchi wamuelewe afanye yafuatayo:

Awateme watuhumiwa wote ili wachunguzwe vizuri.

Serikali yake iruhusu iundwe tume huru ya kuchunguza madai ya ufisadi.

Awaamuru mawaziri wake warejee kazini badala ya kufuja pesa za umma kwa mambo ya kipuuzi na uongo kiasi cha kumletea aibu kwa kuzomewa.

Awe mwepesi wa kujibu yanapotokea matatizo, tena kwa majibu yanayoingia akilini na kutekelezeka.

Akubali ameshindwa na kuanza upya na watu wapya ambao si marafiki zake.

Afanye kile Wazungu huita ‘to take a bull by its horn’. Akubali kuwa moja ya vitu vinavyofanya serikali yake kukwama hata kutoaminiwa na umma ni kujizungushia marafiki na wapambe wanaomdanganya ili waishi au wafiche uovu wao.

Pia apunguze ushawishi wa chama chake kwa serikali yake ambayo kimsingi inaonekana kuburuzwa na chama badala ya kutimiza wajibu wake.

Arejee wabunge kukaa kama kamati ya chama kupindisha au kuzuia hoja za wapinzani ambazo kimsingi ni za wananchi.

Atekeleze kanuni za utawala kwa vitendo na si maneno. Atimize ahadi alizowapa wananchi.

Nimalizie kwa kumkumbusha kutaja mali zake na familia yake na nyumba zetu ambazo bado tunazihitaji. Nafasi haitoshi. Yapo mengi.

Mungu ibariki Tanzania.


Nkwazigatsha@yahoo.com
 
Babu umenena yote. Pia apunguze safari za nje mara anapoona limeibuka jambo... utamwona huyooo... America, Dubai etc.. Hazina inakauka
 
Back
Top Bottom