Return Of Undertaker
JF-Expert Member
- Jun 12, 2012
- 4,572
- 26,885
Tanga.Mgogoro uliopo ndani ya CUF umeendelea kukiletea chama hicho athari baada ya ziara ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya chama hicho Taifa, Julius Mtatiro jijini Tanga kuzuiwa na jeshi la polisi.
Mtatiro aliwasili jijini Tanga jana jioni kwa lengo la kufanya vikao vya ndani pamoja na kufungua matawi kazi ambayo ilikuwa aifanye leo na kesho.
Mwenyekiti wa CUF ,Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe amesema licha ya kwamba hadi jana jioni walikuwa na barua kutoka jeshi la polisi ya kuwaruhusu kuendelea na ziara ya Mtatiro lakini leo saa 3.00 asubuhi walizuiwa.
“Tulipopewa taarifa ya kuzuiwa, tuliamua kwenda kwa OCD Tanga tukiambatana na mheshimiwa Mtatiro kupata maelezo ya kwa nini tuzuiwe ndipo tukaambiwa Magdalena Sakaya ametuma barua ya kuzuia mikutano hiyo kwa madai kwamba hana taarifa,”amesema Jumbe.
Mwenyekiti huyo alieleza kushangazwa kwake na kitendo cha jeshi la polisi kufanyia kazi maelekezo ya Sakaya huku akisisitiza kwamba CUF
Tanga haimtambui kwa sababu alishafukuzwa uanachama.
“Magdalena Sakaya na Profesa Ibrahim Lipumba sisi Tanga hatuwatambui kwa sababu si wanachama wa CUF, hao ni viongozi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, watambue kwamba njama zao za kuiua CUF hazitafanikiwa kamwe,” amesema Jumbe.
Amesema Julias Mtatiro alikuwa amepangiwa kukutana na viongozi wa kamati ya utendaji ya Wilaya ya Tanga, madiwani, wabunge, kufungua matawi ya Kata ya Duga, Masiwani Shamba, Masiwani, Mabawa, Magaoni, Mnyanjani, Pongwe na Kwanjeka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema wamezuia ziara hiyo kufuatia jeshi la polisi kupokea barua mbili tofauti zenye kupingana jambo lililoashiria kuwa kusingekuwa na amani.
Chanzo: Mwananchi