Serikali ikikumbatia dini moja hatari - Pengo
2009-02-23 10:03:38
Na Mashaka Mgeta
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amemuonya Rais Jakaya Kikwete kuwa majadiliano kati ya serikali na upande mmoja na waumini wa dini moja yanaweza kuhatarisha amani nchini.
Akizungumza katika hafla ya kumpongeza kwa kutimiza miaka 25 ya utumishi wake akiwa askofu juzi usiku jijini Dar es Salaam, Kardinali Pengo alisisitiza kuwa majadiliano yoyote yenye maslahi ya taifa yanapaswa kuhusisha viongozi wa madhehebu ya dini zote nchini.
Alisema kuwapo kwa majadiliano yenye lengo la kufanikisha upande mmoja (wa dini), inaweza kusababisha hasara kwa taifa endapo amani itatoweka.
Pengo alisema hayo mbele ya Rais Kikwete, marais wastaafu wa awamu ya pili na tatu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa Jaji Mkuu, Augustine Ramadhan na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Alitoa mfano kuwa ikiwa Rais Kikwete atahitaji kura za urais kutoka kwa waumini wa Katoliki nchini ni dhahiri kwamba atazungumza naye (Pengo) vizuri ili awashawishi waumini wa kanisa hilo wamchague.
``Ikiwa hivyo, mimi nitazungumza nao na kuwaambia, huyu ndiye wa kumchagua, utapata kura nyingi za Wakatoliki, lakini kama hazikuwa zinaridhia Watanzania kwa ujumla, kesho na keshokutwa hali itakuwa ngumu nchini,`` alisema.
Kardinali Pengo alisema viongozi wa dini wana wajibu wa kutoa sauti za kinabii katika jumuiya za watu, hivyo sauti hizo haipaswi kuzuiwa.
``Haitakuwa kitu kizuri kuzizima sauti hizo kwa sababu yoyote, iwe ya kisiasa, kiuchumi ama vinginevyo,`` alisema.
Pengo alisema kuna haja ya kupima sauti za unabii, kwa kuwa baadhi ya watu wanatumia mwanya huo kwenda kinyume, ikiwa ni pamoja na kusababisha mafarakano.
Siku zote dini zina wajibu wa kutekeleza jukumu la unabii wa kweli, kamwe dini zisitumike kama chombo cha siasa,`` alionya.
Kuhusu madai kwamba kuanzia siku za hivi karibuni amepunguza kukemea maovu katika jamii, Pengo alisema msimamo wake bado uko pale pale.
``Pengo wa zamani ni yule yule aliyepo leo, tofauti inayoonekana ni kutokana na mabadiliko ya siasa nchini,`` alisema.
Alisema mfumo wa sasa unatawaliwa na vyama vya siasa kumiliki ama kuwa na uhusiano na vyombo vya habari, hivyo anapokemea jambo baadhi ya vyombo hivyo haviandiki ili kulinda maslahi ya vyama husika.
``Sijapunguza kukemea mambo yasiyokuwa mazuri naposema lakini jambo lenyewe likawa halipendwi la chombo fulani cha habari, halitakichapisha,`` aliongeza.
Kwa upande mwingine, Kardinali Pengo alionya matumizi mabaya ya baadhi ya vyombo vya habari kwa kuwa vinaifarakanisha jamii badala ya kuiunganisha.
Alisema kwa maana hiyo serikali inapaswa kuepuka hali ya kutenda majukumu yake kutokana na taarifa za vyombo hivyo.
``Usipokuwa makini (Rais), Taifa litaongozwa na magazeti…sisemi uyafungie, utaitwa dikteta, cha msingi tuwe waangalifu, tusiruhusu taifa likaongozwa na vyombo vya habari, ni jambo la hatari,`` alisema.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kikwete alisema Kardinali Pengo ni nyenzo muhimu katika kushamirisha mazingira ya amani, maelewano na utulivu nchini.
Alisema kauli za Pengo mara kwa mara hazitoki kwa kukurupuka, bali zinatawaliwa na kiwango cha juu cha kutafakari kabla ya kutamka.
``Kwa maana usipojipa muda wa kufikiri, matokeo yake ni kukurupuka, kuropoka na baadaye kujutia…wewe ni msikivu, mpole, mvumilivu, unatafakari kabla ya kuamua, haukurupuki,`` alisema Kikwete.
Alisema Pengo licha ya kuwa kiongozi wa dini nchini, amechangia pia maendeleo na huduma za jamii, bila kujali tofauti za kiimani.
``Umefanikisha pia maelewano miongoni mwa waumini wa dini zote, hauna sifa ya ubaguzi kama ilivyo kwa viongozi mbalimbali wa dini na hata wanasiasa,`` alisema.
Rais Kikwete alisema ubaguzi wa kidini ni miongoni mwa hatari kubwa zinazoweza kuliangamiza taifa tofauti na ulivyo ukabila.
``Ukabila si tisho, bali kwa eneo dogo, lakini udini unaweza kuliyumbisha taifa, ukawa kama baruti ya kuwasha moto usiozimika, tukiwa na viongozi wa aina yako nchi inaepuka hatari hiyo,`` alisema.
Naye Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Askofu Alex Malasusa, alisema Pengo anatambuliwa na kuheshimika kama kiongozi wa madhebu ya kikristu nchini na si Wakatoliki pekee.
``Viongozi wa madhehebu tunamuona Pengo si kwa ajili ya Wakatoliki tu, bali mshauri na mwenye kuleta ujumbe wa Mungu kwa viongozi wa dini zote ni kama baba yetu,`` alisema.
Hafla hiyo, ilihudhuriwa na maaskofu wakuu na maaskofu wa kawaida (Wakatoliki) kutoka Malawi, Burundi na Tanzania, watawa na waumini wa kawaida.
Pengo pia alikuwa anatimiza miaka 38 tangu kupata daraja la upadre na miaka 10 alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Yonane Paul II kuwa Kardinali.
SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako