Padri Dr Shukrani Mbirigenda: Nadharia ya elimu ya Plato na elimu yetu ya Tanzania

Padri Dr Shukrani Mbirigenda: Nadharia ya elimu ya Plato na elimu yetu ya Tanzania

Inside10

JF-Expert Member
Joined
May 20, 2011
Posts
33,615
Reaction score
40,161
NADHARIA YA ELIMU YA PLATO NA ELIMU YETU YA TANZANIA

UTANGULIZI

Plato ni mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi miaka 400 kabla ya Kristu. Katika kuzungumzia nadharia ya elimu, Plato aliwahi kusema kuwa watu ndani ya jamii wapewe elimu kulingana na kundi waliomo kwenye jamii.

Plato alitofautisha makundi matatu ya watu ndani ya jamii. Alisema kama mwili wa binadamu ulivyo na sehemu tatu, yaani kichwa, kifua na kiwiliwili, ndivyo watu walivyogawanyika ndani ya jamii. Kuwa kuna watu wenye akili za kufikiri, hawa hutumia kichwa zaidi, hawa wapewe elimu ya utawala ili watawale.

Aliwaita hawa “philosopher kings.” Na aliamini kuwa ili nchi ipate maendeleo yahitaji wanafalsafa wawe watawala au watawala wawe wanafalsafa. Na aliamini hawa watawala siyo lazima watoke kwenye ukoo wa watawala, bali kuna watu tangu wakiwa wadogo walionyesha kuwa na akili kubwa ya kufikiri, watengwe na wapewe elimu tofauti na wengine ya kuwaandalia kufikiri kutatua matatizo na hivyo kutawala.

Plato alitengeneza mtaala kuainisha nini hao wanaotayarishwa kuwa watawala wasome na kwa miaka mingapi, na mwishowe kwenye umri wa miaka 40 wawe wameshafanya practical experience kwenye ofisi za umma na sasa wanaweza kuanza kutawala.

Shida moja aliyoiona ni kuwa hawa watu wenye akili mara nyingi huwa hawataki kutawala, hupenda zaidi kufikiri. Na hata ukiwalazimisha huangalia tu lini watamaliza muda wao waende wakaendelee na kazi waipendayo ya kufikiri.

Hii hata Mwalimu Nyerere aliizungumzia kwenye kitabu chake cha “Uongozi wetu na hatima ya Tanzania” kuwa hawa ni wazuri sababu hata kama huna katiba nzuri hutapata shida maana wataondoka tu kwa vile hawapendi kutawala, tofauti na wanasiasa ambao hata muda ukipita watataka kubadilisha katiba waendelee kutawala.

Kundi la pili la watu katika jamii, Plato alisema ni wale wenye vifua vipana, wanaopenda kujionyesha wana mabavu (bully). Anasema tangu wakiwa watoto kuna ambao watajionyesha hupenda kutumia vifua.

Hawa hupenda kutishia na kuonea wenzao. Plato alisema hawa pia wanatakiwa wawekwe pembeni na wapewe elimu tofauti maana hawa wanafaa kuwa askari. Anasema hawa hawafai kuwa watawala maana wanatakiwa kuongozwa na wale wanaofikiri, ama sivyo itakuwa shida maana wataonea watu na hawaoni madhara maana hawafikiri wanaongozwa na ubabe wao.

Hivyo hawa wawe tu watu wa kupokea amri toka kwa wale wanaofikiri ili watumie ubabe wao vizuri kwa manufaa ya wote.

Kundi la mwisho, Plato anasema ni la wale ambao ni wazalishaji (artisans). Hawa wanaongozwa na “hamu” (appetite) zao, mfano tumbo lao huweza kuwafanya wafanye chochote (mfano mzuri hapa ni wa Esau kwenye Biblia alipouza uzaliwa wa kwanza kwa sahani ya dengu).

Hawa wakati wetu ni wale ambao wakienda kula utaona kwenye social media “nikiwa nakula bata na marafiki zangu”, wakiona watu wanagombana wameposti picha “nilishuhudia mtaani wakikung’utana”, wakigombana na mumewe au mkewe utaikuta “hata nashangaa niliolewaje/nilioaje mwanamke/mwanaume kama wewe.” Hawa ni wale ambao anaweza hata muandika baba au mama yale kwenye social media kuwa ni mlevi, mzinzi na kadhalika.

Plato anasema pia hawa watengwe tangu wakiwa wadogo na wapewe elimu kulingana na kundi lao la wazalishaji. Hawafai kutawala badala yake wanahitaji kutawaliwa ili kuzitawala tabia zinazotokana na hamu zao. Hawa wakiwa watawala wanaweza kuuza nchi kutunisha matumbo yao (hamu zao).

NADHARIA YA ELIMU YA PLATO NA ELIMU YETU

Plato anasema ni ukweli usiopingika kuwa watu wana uwezo wa kufikiri tofauti na si kuwa kuna mmoja aliye bora zaidi, ila kuwa si kila mmoja ana-fit kila sehemu katika jamii na hivyo huwezi kumpa elimu yoyote.

Ni kupoteza muda mzalishaji (artisan) kumfundisha kwa kutumia mtaala wa wale wanaotakiwa kutawala au wanaotakiwa kuwa askari (guardians). Kada hizo tatu zinategemeana na hakuna aliye bora maana watu hawa kuzaliwa na vipaji sawa, na si kuwa mmoja amejifanyia chochote, ila ni kuwa alizaliwa hivyo.

Kuna mwenye uwezo wa kufikiri kwa kiwango cha kuwa mtawala, na kuna mwenye kiwango cha kufikiri cha kuwa askari (hawezi kwenda zaidi) na kuna ambaye ana kiwango cha kufikiri cha kuwa mzalishaji (hawezi kwenda kiwango cha juu zaidi).

Hivyo kumpa mzalishaji elimu ya mtaala wa askari au ya mtaala wa mtawala ni upotezaji wa muda na rasilimali (waste of time and resources) na kumtesa, labda gatekeepers wasiwe serious ama sivyo hawezi, hatatoboa.

Sasa, elimu yetu wakati wa mfumo wa Ujamaa ilipangwa hivyo, vyuo vikuu, vyuo vya ufundi na vyuo vya ualimu. Vyuo vikuu vilikuwa kwa ajili ya kuwaandaa watu wanaofikiri.

Hawa waliandaliwa kuleta mawazo mapya. Vyuo vya ufundi viliandaa mafundi watakaofanyia kazi mawazo ya wale wanaofikiri. Hivyo kuna wanaotoa proto-type na wale wanaoangalia kama hiki kilichoko kwenye proto-type chaweza kuwa kiuhalisia (in reality). Hawa wa kufikiri si lazima wafikiri kinachowezekana kwa wakati huo. Kama hakiwezekani kwa sasa kitawekwa mpaka wakati sayansi au uelewa utakapokuwa na kuweza kufanyiwa kazi tena.

Hivyo tukawa na vyuo vya kutoa digrii, ambavyo elimu yao kwa mujibu wa mtaala wa digrii ni rarefied (kufikiri, nadharia). Halafu kukawa na vyuo vya ufundi na kati ambavyo vilitoa diploma, ambavyo kwa mujibu wa mtaala wao wa diploma ni watu wa kufanya/kutengeneza (vitendo), ni mafundi mchundo hawa (technicians). Wote wawili wakishirikiana kila mmoja kwake kuleta maendeleo ya nchi.

Maendeleo hayawi kwa fundi mchundo kupewa elimu ya anayefikiri au kufundishwa kwa mtaala wa yule anayetakiwa kufikiri. Fundi mchundo akipewa elimu ya kufikiri, atafeli au akipasi kwa uzembe wa mfumo, atabaki kuwa fundi mchundo mwenye cheti cha mmoja anayefikiri, lakini yeye hawezi kufikiri.

Vyuo vya kati ya biashara mfano vinatengeneza wahasibu, hawa kazi yao ni kufanya kazi kwenye mabenki na maofisi. Vyuo vikuu vinatengeneza wenye elimu ya uhasibu lakini kazi yao ni kufikiria mifumo mipya bora ya kufanya au kuweka mahesabu au jinsi ya kuboresha ile ya zamani.

Sasa baada ya kuingia katika uliberali, tuka-liberalize na elimu. Kwahiyo kwanza tukaamua vyuo vyote viwe vya wanaofikiri, vitoe digrii. Hivyo hata aliyetakiwa kuwa fundi mchundo analazimishwa kufikiri. Na mbaya tukaweka elimu sokoni, hivyo kila mwenye fedha anaweza kuinunua mpaka atakaposema basi.

Hivyo yule aliyetakiwa aishie diploma sababu si wa kundi la zaidi ya hapo anaweza kuinunua digrii ya kwanza na ya pili na hata PhD. Matatizo yake yanakuja kwenye kuhakiki ufikiri unaodaiwa na vyeti.

Mwenye digrii ya kiwango cha ufikiri aliyetakiwa kufikiri halafu aandike, anaanza kuandika kwanza ndiyo anafikiri baadaye, ndipo unajiuliza, “mmh, huyu mtu ana Master’s degree kweli?” au “Ana PhD kweli huyu?” Lakini ni mmoja aliyetakiwa kuwa na diploma ila sababu sasa tunadhani digrii ni bora kuliko diploma basi naye akaenda kuipata, na kwa vile elimu siku hizi inauzwa, ameweza kuinunua digrii ya kwanza, master’s mpaka PhD.

Sasa elimu ya digrii ni ya kufikiri na kufikiri kitu kipya au kuboresha cha zamani, kuja na innovation, creativity. Lakini kama mmoja mwenye kipaji cha kufanya (hands on tools) tunamlazimisha kufikiri hawezi kuja na kitu kipya. Analazimika ku-copy na ku-paste, editing here and there, but either it is essentially the same or destroying the internal coherence of what was there before.

Kiuhalisia hata watu wanaotuzunguka wanasema kuhusu makundi haya ya Plato. Wangapi tumezungukwa na marafiki ambao wanaweza kutushauri mambo ya maana? Au tunapoandika mambo ya maana kwenye pages zetu, ziwe za Facebook, Instagram, Twitter au telegram, marafiki zetu wangapi wanasoma? Lakini tukiweka picha zetu au ku-post za wengine na kuandika habari zisizo na faida kwa jamii, kama “Ona X kafumaniwa”, “Mwenzenu mama yangu ni mchawi” tutapata hundred “likes”.

Hii inasema mengi kuhusu sisi wenyewe na wanaotuzunguka, na tusipofikiri twaweza lewa hii tunajiona heroes, lakini heroes wa nini? Wanaotuzunguka hawa kama ilivyo rahisi ku-like na siyo kuchangia cha maana ndivyo itakuwa rahisi kutuacha maana they were never engaged with us. Ukiona umeandika vitu vya maana vya kutafakarisha, kufikirisha na watu wengi wanachangia, inaonyesha una marafiki wanaofikiri na wako engaged; pia kuwa tuna jamii yenye uelewa inayofikiri na kujishughulisha.

Ukiona comment 5 na likes 20 lakini picha wana-comment 70 na likes 180, inaongea kuhusu aina ya wanaokuzunguka na jamii yetu kiujumla. Waingereza walisema, show me your friends and I will tell you who you are, twaweza ipeleka mbele na kusema nionyeshe watu wako nami nitakuambia jamii yako ni ya aina gani.

Sasa basi, mfumo wetu wa elimu wahitaji marekebisho makubwa. Wahitaji kufumuliwa na kujengwa upya. Maana hata tukirudi kwenye vyuo vya ualimu ni shida hiyo hiyo. UPE iliingizwa kwenye uliberali lakini haikuwa -designed kwa uliberali. Wakati wa Ujamaa, shule za sekondari na vyuo vilikuwa vichache hivyo wengi walifikia ufaulu lakini hawakuweza kuchaguliwa kuendelea na masomo maana nafasi hakuna. Hivyo Nyerere aliamua hawa wapelekwe wakawe walimu, ndiyo iliyoitwa UPE.

Sasa sisi tukaiingiza kwenye uliberali, kipindi ambacho siyo wanafunzi wanatafuta shule za kusoma, bali shule zinatafuta wanafunzi wa kusoma. Sasa ukiendeleza mfumo ule wa UPE wa wale wanaoachwa uwachukue kuwapeleka ualimu manake unapeleka vituko. Lakini kwa miaka kadhaa tulifanya hii, mpaka kuna wakati likatokea jina maarufu la “Voda fasta” kumaanisha walimu waliofundishwa haraka haraka wakafundishe na wao.

NINI TUFANYE?

Kwenye Taaluma ya Maendeleo (Development Studies) tuna somo kwa postgraduate students linaitwa Political Thought, baadhi ya wanataaluma wa falsafa za siasa za Afrika wanasema kuwa tukitaka kutoka tulipo sasa yabidi tujipange upya.

Na mojawapo ya vitu wanavyosema ni kuwa twahitaji what they called “African Renaissance”. Katika kundi hili tunao akina Thabo Mbeki na shule ya Chango Macho W’obanda. Hii falsafa inasema tufufue ule moyo wa uanamapinduzi uliokuwepo na wanasema hapa kuna umuhimu wa kuachana na uliberali na kurudia mila na desturi zetu kama demokrasia ya makubaliano badala ya hii ya kiliberali. Hivyo twahitaji kujifunza historia ya kweli ya mwafrika na siyo hii tuliyokaririshwa na mkoloni.

Kundi la pili linasema tunahitaji nadharia ya uanamapinduzi mpya wa maendeleo. Katika hii wanasema siyo tu twahitaji kufufua mawazo ya wanamapinduzi wa Afrika bali pia kuendeleza, yaani kuona hayo tunayofufua yanatakiwa kuboreshwaje.

Hapa tunashauriwa kurudi kwenye falsafa za waanzilishi wa mataifa ya Africa, mfano “Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea” ya Nyerere bado ina maana, ni “valid and relevant” mpaka leo. Elimu ya ujamaa iliamini katika kumtengeneza mmoja kujitegemea. Wachache ndiyo walipewa elimu ya kufikiri. Sasa tuangalie elimu hii yaweza kuboreshwaje ili ikidhi mahitaji ya sasa.

HITIMISHO

Kwa elimu yetu ya sasa tumebadilisha kuwa wengi wawe wa kufikiri, lakini ukweli ni kuwa sababu wengi wanaopewa elimu ya kufikiri hawawezi kufikiri, hata wale waliotakiwa wawe na elimu hiyo sababu wanachanganywa na wenye ufikiri hafifu, wanafikiri kidogo sana na kujiona vinara.

Wakati wangepambanishwa wao kwa wao (wenye uwezo wa kufikiri watupu) ushindani ungekuwa mkubwa na ufikiri wao ungekua zaidi. Tatizo tumedhani elimu ni kitu cha kujivunia na siyo kile tunachoweza kufanya na hiyo elimu, tungeona elimu ni kile ninachoweza kufanya na elimu hiyo tungeona hakuna elimu iliyo bora zaidi ya ingine, si cheti, diploma wala digrii.

Kwa sabau elimu ni cheti na siyo tunachoweza kufanya kwenye jamii kutumia elimu hiyo, sasa kati yetu tupo wasomi wa kutosha ambao ukiondoa vyeti vyetu hakuna kitakachoonyesha kuwa tuna digrii ya kwanza au ya pili au hata PhD.

Hivyo yabidi tutangulize vyeti vyetu kuonyesha kiwango chetu cha elimu ili watu wasituweke kwenye kundi letu tunalostahili. Lakini makundi yetu haya si mabaya, ni kuwa sisi tulizaliwa hivyo (kila mmoja na kipaji chake tofauti) wala hakuna cha kujisifia tulichofanya, hivyo hatuna sababu ya kujisikia vibaya au kujivuna. Na zaidi la muhimu ni kuwa twahitajiana.

Anayefikiri anamuhitaji guardian kumlinda ili afikiri kwa uhuru na usalama, fundi mchundo kutengeneza kile kipya anachofikiria na mzalishaji kumpa chakula apate afya ya mwili na akili.

Guardian (mlinzi) anamuhitaji anayefikiri kumwambia cha kufanya na kufikiri zana mpya za kulindia, fundi mchundo kumtengenezea zana za kulindia na mzalishaji kumpa chakula. Mwisho, mzalishaji anawahitaji wote kuanzia anayefikiri kupata mbinu mpya za kilimo, guardian (mlinzi) kumlinda yeye na mazao yake, na fundi mchundo kutengeneza zana zake za kilimo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom