Chama cha ACT-Wazalendo kimewataka Wanachama na Wafuasi wake kutoshiriki katika zoezi la kura ya mapema unaofanyika leo Oktoba 28, 2025, na badala yake wasubiri kushiriki Siku rasmi ya Uchaguzi wa Wananchi wote itakayofanyika Oktoba 29 Mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo ambaye pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama hicho, Othman Masoud Othman kupitia taarifa yake kwa umma.
Othman amesema uamuzi huo umetokana na mashauriano ya Chama hicho na Mamlaka husika, ambapo wamejiridhisha kuwa changamoto zilizokuwa zimebainishwa awali kuhusu maandalizi ya Kura ya mapema zitashughulikiwa ipasavyo ili kuhakikisha Uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
"Tumejiridhisha kuwa changamoto tulizozianisha zitapatiwa ufumbuzi, hivyo tunawahimiza Wanachama wetu wasiende Vituoni tarehe 28, bali wasubiri Siku rasmi ya Wananchi wote ya tarehe 29 Oktoba kushiriki kutekeleza haki yao ya kikatiba." alisema Othman.
Aidha, Othman amewataka Wafuasi wa ACT-Wazalendo kudumisha amani na kufuata maelekezo ya Viongozi wa Chama wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi.
Awali Chama hicho kilikusudia kuwataka Wafuasi wake waende kulinda kura katika Siku ya Kura ya Mapema ambayo imepangwa kufanyika Oktoba 28, 2025.