NYEUSI NA NYEUPE; Njia Ya Haraka Ya Kutajirika Na Biashara Isiyo Na ‘Stress’.

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,411
Habari rafiki,


Karibu kwenye makala yetu ya leo ya NYEUSI NA NYEUPE, ambapo huwa tunauangalia ukweli kama ulivyo, bila ya kuupindisha kama ambavyo wengi wamekuwa wanafanya ili kujinufaisha. Moja ya kitu ambacho kimekuwa kinakimbiwa na wengi ni ukweli, lakini wenyewe huwa haupotei, bali hujitokeza, hasa pale usipotegemewa.


Leo tunakwenda kuangalia maeneo mawili ambayo watu wamekuwa wakidanganywa na kujidanganya sana. Watu wamenufaika kwa uongo mkubwa ambao umetengenezwa kwenye eneo hili. Na kitu kikubwa sana ambacho kimekuwa kinanishangaza kwenye eneo hili ni kwamba, hata mtu anayejua kabisa ni uongo, bado anaingia kwenye uongo huo na kujikuta akipoteza nguvu, fedha na muda.


Maeneo tunayokwenda kuangalia leo njia ya haraka ya kutajirika na biashara isiyo na ‘stress’.


NJIA YA HARAKA YA KUTAJIRIKA.


Hii ni kiu ya wengi, wapo watu ambao wamekuwa wanakesha usiku na mchana, kutafuta njia hii. Na uwepo wa mtandao wa intaneti, basi watu wamekuwa wanakesha kwenye mitandao kutafuta njia ya haraka na ya mkato ya kutajirika.


Ukitaka kuelewa vizuri hili, usiangalie tu sasa hivi, bali angalia historia ya dunia kwa miaka mingi iliyopita. Kwani hili limekuwa ni tatizo karibu kwenye kila kizazi.


Miaka mingi iliyopita ilikuwepo dhana inaitwa Alchemy, ambapo watu waliamini kuna njia unaweza kugeuza vyuma vya kawaida kuwa dhahabu. Mataifa yalilaghaika na hali hiyo, kutafuta watu wa kubadili vyuma kuwa dhahabu ili kupata utajiri. Lakini hakuna mtu aliyeweza kudhibitisha kufanya hilo, lakini bado watu waliendelea kuamini ipo namna.


Haya ndiyo yanayotokea sasa, japo hakuna namna mtu anaweza kupata fedha ya haraka kwa njia ya mkato bila ya kufanya kazi, bado watu wanaamini ipo njia ya kufanya hivyo. Wanaamini wale waliozipata fedha wana siri ambayo wao hawajaijua ndiyo maana hawapati fedha. Na hata siri inapokuwa wazi kwamba wenye fedha wanafanya kazi, tena sana, na wametumia muda mwingi kufika pale walipo, bado watu hawakubali, wanaendelea kuitafuta siri ya kupata utajiri wa haraka.


Hapo ndipo utapeli unapoanzia, maana matapeli wamekuwa wanatumia njia hii kujinufaisha tangu zamani. Kwa sababu wanajua watu wanatafuta njia ya mkato ya kutajirika, basi wanatengeneza siri ya uongo, na kuwapatia watu wakidai ndiyo itawapa utajiri. Wanafanya hivyo wakitengeneza njia ya wao kunufaika kupitia hilo. Hivyo wanakuwa wanauza siri ya utajiri, ambayo wao wenyewe hawajaitumia, na utajiri ambao wataupata wao, ni kupitia kuuza siri ya utajiri. Huoni namna inavyoshangaza eh!


Ukweli ni kwamba, mtu yeyote anayekuuzia siri ya kutajirika haraka bila ya kazi, siri hiyo ni wewe, na anayetajirika ni wewe. Na wewe ukitaka kutajirika inabidi utafute wajinga wengine ili nao uwahadae. Kwa maana hii, siri ya utajiri wa haraka na bila ya kufanya kazi, ni kuwapata wajinga na kuwalaghai. Sasa kama unataka kutumia njia hiyo, utaamua mwenyewe, kwa sababu mwishoni itakuumiza.


Angalia hadithi zote za kutapeliwa, ni zile zile na vinavyotumika ni vile vile. Mtu anauziwa chupa zilizosagwa akiamini ameuziwa madini kwa bei rahisi na atatajirika. Au anauziwa kipande cha sabuni akiamini anapata simu kwa bei ya kutupa.


Nimalize hapa rafiki yangu kwa kukuambia hakuna njia ya haraka na ya mkato ya kutajirika bila ya kufanya kazi. Haipo kabisa. Na kama ingekuwepo, wala watu wasingekuambia, wangekuwa ‘bize’ kweli kweli kupata utajiri huo kabla wengi hawajaijua. Kama unaona mtu anakutafuta kukuambia anakupa njia ya haraka na ya mkato ya kupata utajiri, stuka, anataka kukutapeli. Wakati mwingine anayekutapeli anajua, au hajui, kwa sababu na yeye pia ametapeliwa. Kaa mbali na michezo au mifumo yoyote unayoambiwa utapata fedha haraka bila ya kufanya kazi. Huenda hutasikiliza hili, kwa kuamini ipo siri hujaijua, na sitakulaumu kwa hilo, kwani utajifunza vizuri ukishatapeliwa na kupotezewa muda wako.


BIASHARA ISIYO NA ‘STRESS’.


Kwenye makala hii nitatumia neno stress kama lilivyo, bila ya kulielezea kwa namna yoyote ile. Nikiamini unaelewa ni kitu gani nazungumzia hapa, na iwapo huelewi basi hili litakuwa halikuhusu.


Wapo watu wamekuwa wakiomba sana ushauri wa biashara, na wanachotaka wao ni biashara isiyo na stress, biashara ambayo akishaweka fedha zake anachosubiri yeye ni kuvuna faida tu, hakuna usumbufu mwingine wa aina yoyote ile.


Na ninawaelewa vizuri sana. Maana ni tabia yetu binadamu kupenda kupata kikubwa zaidi kwa jitihada ndogo zaidi. Kama unabisha wacha nikupe mfano. Ipo kampuni ambayo inatengeza mikate, na mkate wa aina moja, unaofanana kila kitu kuanzia kutengenezwa mpaka ukubwa. Lakini mkate mmoja unauzwa shilingi 500 na mwingine unauzwa shilingi 600, wewe utanunua upi? Jibu lipo wazi, unanunua wa shilingi 500, utalipaje ziada wakati unapata kile kile?


Sasa dhana hii ndiyo tunapeleka kila mahali, mpaka isipofaa. Kama hivyo unavyotaka kupata biashara ya kufanya, ambayo haina stress, ukishaweka fedha tu basi unavuna faida.


Nina habari mbaya kwako, kwamba hiyo biashara unayotafuta haipo, na kama ingekuwepo, basi kila mtu angekua anaifanya. Dunia imejipanga vizuri sana kukujaribu na kukurudisha nyuma kwenye chochote unachopanga kufanya. Utaona watu wamelima nyanya mwaka huu wakapata kweli, mwaka kesho ukaenda kulima na wewe ili unufaike, hali ya hewa inakuwa mbaya na unapata mavuno kidogo sana. Au hali ya hewa inakuwa nzuri lakini mavuno yanakuwa mengi sokoni na hivyo bei kushuka.


Sitaki nieleze mengi hapa, ila ninachotaka kukuambia ni kwamba, usipoteze muda wako kutafuta biashara isiyo na stress, bali chagua stress za biashara gani unaweza kuzivumilia. Hivyo hapa utaangalia kile unachopenda kufanya, au kinachowasaidia wengine, hivyo licha ya kukutana na misukosuko, kuna kitu cha ziada unakipata ndani yako kwa kufanya biashara ile.


Yeyote atakayekuambia namna nyingine, kwamba biashara fulani ndiyo haina stress, stuka, kuna kitu anataka kukuuzia, au kwa wewe kujiunga na biashara hiyo, kuna namna ananufaika. Kila biashara ina stress zake, chagua zipi unaweza kuvumilia na weka juhudi kupata matokeo bora.


Hayo ndiyo mawili muhimu nimependa kukushirikisha leo rafiki yangu, kwa ukweli kabisa bila ya kukufichaficha wala kukulaghai. Kama utaendelea kupoteza muda wako kutafuta njia rahisi na za mkato, nikutakie heri, lakini ukishamaliza kuhangaika na kujidhihirishia wewe mwenyewe kwamba unachotafuta hakipo, kaa chini, chagua unachoweza kufanya na weka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.


Rafiki na Kocha wako,


Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com
 
Duuh uzi saf sna huu japo nilishajua toka siku nying kwamba ukitaka mali lazima uvije jasho nashukuru sikua na tamaa mpka ifikie kutapeliwa
 
kweliii mkuu upo vizuriii hata kina Dk.Mengi wana stress za biashara ambazo wamevumilia hadi kufikia hapo walipo but labda unaweza kuwa mfano mkubwa kwa watu kama millady ayo n.k
 
Ahsante school mate, nakumbuka kipindi kile kibaha wakati unaenda na vyombo vya chakula clax uka ni inspire kukesha
 
Safi kabisa. Huo ndio ukweli usiopingika. Tena, ni watu wengi sana ambao wanapata hasara kubwa sana ya kutapeliwa (kama wale wa DECI) kwa sababu ya kutaka kupata pesa chap chap.
 
Mi nadhan biashara ni kama maisha ya kawaida zile changamoto ukizifanya zitende kwa manufaa yako ndio faida inapokuja,..uko vizuri wafanyiabiashar sio kwamb wanavumilia stress ila wanatumia izo stress kutengeneza faida zaid kwa manufaa,..kwa mfano kampuni ya Nokia,ilikua kubwa sana lakin kutokana ilishindwa kubadilika na kuchukulia mabadiliko ya technologia na mienendo ya wateja wake,..ikawa imevumilia kwa kuona itashinda kwa kutofanya chochote,ikaanguka vibaya,..entrepreneurship is motivating profit through change and Patience,
 
Mi nadhan biashara ni kama maisha ya kawaida zile changamoto ukizifanya zitende kwa manufaa yako ndio faida inapokuja,..uko vizuri wafanyiabiashar sio kwamb wanavumilia stress ila wanatumia izo stress kutengeneza faida zaid kwa manufaa,..kwa mfano kampuni ya Nokia,ilikua kubwa sana lakin kutokana ilishindwa kubadilika na kuchukulia mabadiliko ya technologia na mienendo ya wateja wake,..ikawa imevumilia kwa kuona itashinda kwa kutofanya chochote,ikaanguka vibaya,..entrepreneurship is motivating profit through change and Patience,
Asante sana kwa nyongeza na mfano mzuri.
 
Back
Top Bottom