Nikilitazama taifa langu chini ya utawala wa CCM, naona kiza kinene

MMASSY

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
290
193
Siku ya Jumamosi ya tarehe 30/05/2015 nilishuhudia kituko cha Mwaka hapa Arusha pale kada mtiifu na fisadi mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi aliponunua watanzania wafia tumbo kutoka sehemu mbali mbali za nchi ili kutangaza kile alichokiita kuwa eti ni Nia ya kugombea Urais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania.Niliona namna watanzania kutoka mahali mbali mbali walivyoujaza uwanja ule na kukaribia kuingilia hata shughuli zetu tusiokuwa sehemu ya shughuli hiyo.Nilibahatika pia kuonana huku mjini na baadhi ya vijana "wasomi" niliowahi kusoma nao sehemu mbali mbali za nchi ya Tanzania.

Aliyoyasema Lowassa ni kama vile hakuwahi kuwa kiongozi wa nchi hii wala kushika nafasi yoyote ndani ya serikali na chama chake.Lowasa ameahidi kupambana na Rushwa na Ufisadi(Mama yangu!!) yaani yule ambaye hata walioko kwenye chama chake walimweleza kuwa yeye ni fisadi(Gamba).Hata watoto wadogo wanajua Lowassa ni fisadi(sijui wamejuaje).Niliwahi kumwuuliza mtoto mmoja katika shule moja huko moshi kuwa akiwa mkubwa anataka awe nani?

Cha kushangaza alisema bila kupapasa macho nataka kuwa fisadi kama Lowassa wa Richmond.Hii inatupa picha kuwa Lowassa bado si safi katika kashfa ya Richmond.Na akitaka kujisafisha ni hadi atakapoleta ushahidi kuwa hakuhusika na ufisadi wowote ndani ya serikali na awataje waliokula Richmond.Lazima atuambie hadi leo ni nani anayelipwa Capacity charge ya Millioni 152 kwa siku.Atalazimika kutuambia kuwa kwanini marafiki zake wa karibu wanao Muunga mkono ni wale waliotemwa katika nyakati mbali mbali serikalini?Wakina Karamagi wa Buzwagi,Rostam wa Richmond na EPA,Anaungwa mkono na Adrew Chenge wa Kashfa zote zilizowahi kkutokea nchi hii.

Kuanzia kashfa ya Buzwagi ,Radar,Ndege ya Rais hadi Escrow,hakuna ambayo hajatajwa kuhusika.Lowasa anaungwa mkono na mafisadi wenzake waliokubuhu.Anaungwa mkono na Prof.Anna Tibaijuka aliyetawa kuchota zaidi ya Bilioni moja na milioni mia sita kutoka kwa Rugemalira wa Escrow.Fedha hizi Mama Tibaijuka alidai ni za mboga kwa hiyo hatuna haja ya kuzidai.Huyu ndiye Lowasa,ndiye aliyewaambia wahudhuriaji katika mkutano wake kuwa atadhibiti rushwa kwa vitendo.

Kwake yeye kukodi watu 40 kutoka kila mkoa Tanzania na kuwagharamia usafiri,malazi na chakula pakoja na kuwapa fedha za posho za kushiriki sio rushwa,kuna rushwa ya aina nyingine anataa kuiondoa katika serikali anayotaka kuiunda hapo mwezi wa kumi(siku ya ndoto kwake).Lowassa anatuaminisha kuwa yeye ni rafiki sana wa machinga na mama Ntilie.Nashindwa kujua urafiki huo unatokana na nini kwa sababu hakuna historia wala ushahidi uliowekwa kuonyesha ni lini na ni wapi amekuwa rafiki wa hao akina machinga na mama Ntilie.

Hajawi kuonekana Bungeni wala jukwaani akitetea hao anaowaona leo kuwa marafiki zake.Badala yake Lowasa ameendelea kukaa kimya katika mijadala bungeni,hajawahi kuwatetea marafiki zake hao.Ameshiriki kupitisha sheria kandamizi bungeni.

Wakati akina Mchungaji msigwa,Sugu,Wenje na akina Lema wakipiga kelele kusaidia machinga,yeye aliungana na wabunge wa chama chake kuwananga wapinzani waliowatetea hao rafiki zake.Hizi ni ndoto za mchana kweupe tena anazoota mtu anayekuwa anafikiria.

Juzi jumapili tena, nikaona katika vyombo vya habari Mwigulu Nchemba ambaye ni naibu waziri wa Fedha na Uchumi naye anatangaza nia ya kugombea nafasi hiyo hiyo ya Rais.Naye alichambua sana masuala ya kiuchumi na ya wananchi kwa ustadi wa kiuchumi.Naamini hii iitokana na ubobezi wake katika fani ya uchumi.Alichokisahau Mwigulu Nchemba ni kuwa na yeye ni sehemu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi na tena anasimamia masuala ya fedha.

Anasema atawasimamia wafanyabiashara walipe kodi isiyowaumiza.Amesahau kuwa yeye ndiye aliyekomalia wafanya biashara kulipa asilimia 18% ya VAT.Mwigulu I msomi mwenzangu wa degree mbili za uchumi(Master's) na inasemekana kuwa ni mmoja ya watu waliofaulu vizuri sana darasani.Leo hii msomi huyu anaongoza wizara ambayo sasa deni la Nchi ni Trilioni 30.7.Kwa maneno mengine kila mwananchi na hata mimba iliyopachikwa leo inadaiwa Tsh.845,350.78(Laki nane na arobaini na tano elfu na mia tatu hamsini na senti sabini na nane).

Mwigulu anataka kuleta muujiza ambao akiwa ndani ya chama kile kile kilichoongoza taifa hili tangia uhuru haujawahi kutokea.Yaani leo hii ukiwa na Dola moja ya Marekani unapata Elfu mbili na mia moja na hamsini.Yaani ndani ya mwezi mmoja shilingi imeporomoka kwa asilimia ishirini na sita(26%). Tuko chini ya wizara inayoendeshwa na Mwigulu ambapo hata samani za ofisi zote za nchi hii zinaaagizwa nje ya nchi ya Tanzania.Mimi ni mmoja ya watanzania wasioelewa kabisa utawala huu wa CCM ndani ya wizara ya fedha ambayo katika bajeti ya Mwaka huu kodi imepandishwa kwa asilimia mia moja (100%) katika bidhaa muhimu na hasa kwa wafanyabiashara.

Tunajiandaa watanzania kununua mfuko mmoja wa cement kwa shilingi elfu ishirini kutoka elfu kumi na nne ya sasa.Hii ni wizara ya fedha ambayo Mwigulu ni mmoja ya mawaziri.

Steven Masatu Wasira naye ametangaza nia akiwa Mwanza katika ukumbi wa BOT.Yeye anatuaminisha kuwa anataka kujenga Tanzania mpya.Yani yeye hakubaliani na Tanzania ya sasa.Kwake yeye hakubaliani na namna Chama Chake kinavyoongoza serikali serikali.Amekuwa mpinzani kwa serikali ambayo naye ni waziri na amekuwa waziri huko katika wizara mbali mbalimbali.Yeye anataka kutujengea Tanzania mpya,Huyu Bwana anatokea wilaya ya Bunda ambayo inashika nafasi ya mwisho kwa maendeleo nchi hii.

Sasa WASSIRA amekuwa mbunge kwa miaka lukuki,amekuwa Waziri tangia siku nyingi na ameshindwa kuondoa umaskini kwa wananchi wake.Kwa maneno mengine ameshindwa kujenga Bunda mpya na sasa anatuaminisha kuwa eti akipewa Urais atajenga TANZANIA mpya ambayo pia Bunda ni sehemu yake. Wasira kasahau kwamba ni waziri kama wengine walivyosahau,amesahau kwamba haya anayoyasema sasa angetakiwa awe alishayasema katika vikao ndani ya chama chake na hata Bungeni.

Yeye kasahau kuwa wapinzani wamekuwa wakikosoa sera za chama chake ndani ya vikao vya bunge na hata nje ya hapo.Kuna msemo usemao,"huwezi kusukuma gari ukiwa ndani ya gari hilo hilo".Yani Wasira anataka kuondoa nchi hapa ilipo kwa kutumia chama kile kile chenye sera zilezile,na aina ya uongozi ule ule.Najaribu kufuatilia nadharia zote za wataalamu wa masuala ya uongozi na maendeleo zinakataa kufiti hapa.Wassira hana jipya la kutueleza watanzania.

Kwa maneno mengine huwezi kuwa waziri wa kilimo na chakula halafu fedha za wizara zikawa zinaishia kwa wajanja wachache,kilimo kikaendelea kufa halafu bado ukautaka urais kutoka kwa wakulima hao hao.Hii inawezekana TANZANIA tu.

Jana tena Makongoro Nyerere,Professa Mwandosya na Karume tayari nao wameingia kwenye kinyang'anyiro.Hawa nao wamekuwa makada watiifu kwa chama chao na kuiacha nchi mbali.Makongoro ni kama akina Lowasa na Kikwete,hakukubaliwa na baba yake kuwa kiongozi.Alikuwa akipishana na baba yake kimtazamo hadi mauti yanamkuta.

Lazima tujikumbushe aliyoyasema Mwalimu hata kama leo watu wanachukulia kutokuwepo kwa Mwalimu kama fursa ya kuchuma na kupambana kuupata urais kwa gharama yoyote.Tunachojua ni kwamba,Mwalimu alitutahadharisha juu ya watu fulani fulani,Mfano: wakati aliwakataa akina Kikwete na sisi tukaendelea kuwachagua na tumeona matokeo yake.Sasa hivi kila mtanzania analia(kama sio live basi kimoyomoyo).Lowassa alikuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Kikwete,hakumaliza hata uhula mmoja,akang'olewa na Bunge.

Hii inaonyesha wazi Mwalimu alimkataa mtu si kwa chuki binafsi,bali kwa sababu alijua kiongozi huyo hatufai.Makongoro anasema anaweza kuwakomesha mafisadi ndani ya Ccm.Ni nani alimdanganya Makongoro?Baba yake aliona CCM inaelekea kusiko ndio maana alitishia kukihama.CCM walitoa orodha ya magamba na ikawatishia kujiondoa kwenye chama na serikali kabla haijawaathibu.Tangia kipindi hicho hadi leo, bado wapo wengine bungeni na kwenye utumishi wa umma.Hakuna utaratibu wala mkakati wa kuwamaliza mafisadi ndani ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu ufisadi ni utaratibu unaoratibiwa kwa ustadi wa hali ya juu ndani ya chama hicho.Kama ilivyo kwa Wasira,Makongoro angetakiwa awe alishafanya hayo kabla hajautaka urais.

Karume na Mwandosya nao wametangaza nia zao.Ni vizuri tukawapima wagombea kutoka CCM Kwa umoja wao na kwa tabia zao.Kuna msemo usemao " birds of the same feather Flocks together" Yaani ndege wenye mbawa zinazofanana huruka pamoja.Hii inatokana na ukweli kuwa, muundo/mfumo wa mabawa yao unawaruhusu kwenda masafa au kupapae chini chini kwa umoja wao.Kwa hiyo hakuna mtu wala kikundi kinaweza kuleta mabadiliko wanayodai akina Mwandosya na Karume hayawezi yakatokea ndani ya chama cha Mapinduzi.Watu waliozoe kufikiri vilevile,kutenda vile vile kwa namna ileile leo wanataka kuleta mabadiliko?kivipi?.

Mchungaji msigwa aliwaambia vizuri kupitia Bunge kuwa Problems cannot be solved by the same level of thinking that created them.Nchi hii itaondolewa hapa ilipo na ufikiri tofauti.CCM imeleta matatizo mengi nchi hii kuliko kawaida.

Ni CCM waliochochea mgogoro wa Waislamu na Wakristu.Kama kuna anayebisha aniambie Wasira alifanya nini kulipoibuka vurugu za kugombea kuchinja kati ya Waislamu na Wakristu kule kanda ya ziwa.Aniambie CCM ilifanya nini pale migogoro kati ya wafugaji na wakulima ilipoibuka Morogoro.Je hawakuchukulia kama mtaji wa kisiasa?Je migogoro iliyo kati ya wawekezaji na wenyeji kule Sanya Juu,Manyara,Mtwara na Geita si imesababishwa na Chama cha Mapinduzi ambao wanajali zaidi wawekezaji wenye fedha keshi na sio rasilimali ya nchi? Hakuna sehemu nchi hii pamekuwa na mwekezaji pakakosekana mgogoro.

Kama ipo basi ujue ni suala la muda,utatokea tu.Viongozi wetu wa CCM wamejaa tamaa na rushwa, wako radhi tule nyasi lakini wanunue ndege za kifahari ambazo ni mbovu, wako radhi tuuane lakini wao wapewe fedha(takrima) na wawekezaji. Kiongozi mmoja mkuu wa wilaya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi wiki iliyopita alisikika akiwaambia wananchi wazi kuwa wasitegemee kunufaika na uwekezaji eneo hilo jambo lililomfanya hata mwekezaji kutaamaki.

Hiki ndicho chama Cha MAPINDUZI katik ubora wake.Ninachoamini na ninachokijua ni kuwa chama hiki kimechoka kweli kweli.Waziri anaulizwa swali kuhusu mashine za BVR anajibu kupigia debe katiba pendekezwa.Ikumbukwe kuwa ni CCM hao hao waliovuruga Bunge la katiba na kuzaa katiba pendekezwa ya chama.Sasa viongozi waandamizi wa chama na serikali wako njia panda,hawajui wanatokaje katika mtanziko wa kikatiba.Sheria inayoongoza upatikanaji wa katiba mpya imeshavunjwa,ni lazima irekebishwe au irejelewe upya ndio mambo yaende.Wananchi wamekaa mguu sawa kupiga kura ya hapana muda wowote itakavyoitishwa.CCM hawana cha kupoteza.

Kupita katiba mpya kwao ingekuwa mwanzo wa kufa na kuporomoka ghafla kwa chama.Lakini pia hakuna ahueni kwa CCM katika suala la katiba mpya.Kutofanikiwa kuwapatia wananchi katiba mpya hadi october tayari ni pigo lingine ndani ya chama na hata nje ya chama.Ukawa waliweka mpira kwapani na kukimbia nao,CCM na mawakala wao wakabaki wakicheza mpira wa makaratasi.Sasa mshindi hapa anajulikana ni nani.

Rais Kikwete kwa kutumia mamlaka asiyokuwa nayo alitangaza kura ya maoni tarehe 30 april 2015.Pamoja na UKAWA kusisitiza kuwa haitafanikiwa,viongozi wote wa CCM na Serikali wakiongozwa na waziri mkuu Mizengo Pinda walisisitiza ni lazima kufanyika ndani ya tarehe hiyo, sasa hivi ukiwauliza imeishia wapi wote watatoa macho tu.Hii ndiyo nchi inayoongozwa na CCM.Ni nchi ambayo mambo yanafanyika kwa kulipua.CCM na serikali yao wana mgogoro wa wazi na kila kundi katika nnchi hii.Wanao mgogoro na Wakulima,upo mgogoro na madereva,upo pia na walimu,wafanyakazi,vijana,wazee,wanawake na wengine wengi.Uchaguzi wa mwaka huu ni kaa la moto kwa chama hiki.

Yaani kimekuwa dhaifu mno.Kila mmoja anaona anafaa kuwa Rais kwa sababu kuongoza Tanzania siku hizi hutumii akili,unatumia tu propaganda,jeshi la polisi kudhibiti wale wanaokupinga na usalama kung'oa meno na kucha wale wanaokuandika vibaya basi.Ndio maana tunaona foleni za wagombea urais ndan ya hiki chama kuliko wakati wowote ule.

Watanzania tunatakiwa tuwe makini sana hasa katika kipindi hiki.Tutaona na kusikia sarakasi nyingi sana kuelekea mwezi wa kumi.Hata shetani atajileta kama Malaika ili tu tumuimbie Mapambio/Kaswida.Nina miaka ya kutosha sana kushawishi umma kuwa Tanzania haitavuka kutoka hapa ilipo kwa utawala wa watu waliochoka.Hakuna anayeweza kuleta mabadiliko ndani ya nchi hii kwa kutumia mfumo ambao ni Corrupt.Hakuna mabadiliko yoyote kutoka kwa watu ambao wanawaza kwa namna ileile,wanatenda vile vile na wanategemea "matokeo makubwa sasa".

Naandika nikiwa naelewa si kila mmoja atakayefurahishwa na haya hasa wale waliotangaza nia na wapambe wao au hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi.Mnatakiwa muelewe kuwa huo ndio msimamo wangu duniani na hata mbinguni.Yaani ni hivi: "Kumtafuta mgombea Urais safi kutoka CCM ni sawa na kutafuta Bikra kwenye wodi ya wazazi!!" na hakuna muujiza ndani ya CCM utakaovusha taifa hili kwenda nchi ya ahadi.

Makala ijayo nitachambua kipaumbele cha Elimu kama kilivyotajwa na baadhi ya watia nia na namna taifa lilivyokwama kutokana na sera za Chama Cha Mapinduzi.

MMASSY JEROME
mmassyfm@rocketmail.com
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom