William Ngeleja.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Mwanza, kimewaomba wakazi wa Jimbo la Sengerema kukisaidia kumng'oa Mbunge wa jimbo hilo, William Ngeleja.
Chadema imesema ingawa kinafahamu kuwa kazi ya kumng'oa Ngeleja jimboni humo ni ngumu, lakini kwa kuwa amekichokoza kwa kuwahujumu viongozi na wanachama wake, watalazimika kujibu mapigo.
Aidha, kimesema tayari kimeshajipanga na kitawashirikisha baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete, amteme katika nafasi yake ya uwaziri.
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (Chadema), Ezekiel Wenje, aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika uwanja wa Mnadani.
Mkutano huo ulilenga kujijenga upya kwa chama hicho baada ya ofisi yake kufungwa kufuatia viongozi wake kukimbilia CCM na kupokewa na Ngeleja.
Katika mkutano huo, Wenje alisema awali alikuwa akimpenda Ngeleja, lakini baada ya kutishia chama chake kwa kuiba wanachama wake, basi sasa ametangaza vita na Chadema kitahakikisha kuwa anang'olewa kwenye nafasi ya uwaziri na hata ubunge mwaka 2015.
''Hakuna jinsi, nimeamua kuja kufanya mkutano hapa japokuwa najua Ngeleja anakubalika..nilipokuja katika uwanja huu mwaka jana, mliniambia huu ni uwanja wa Ngeleja, lakini bado kwa usajiri nimerudi kwa staili hii ya kuwaomba mtusaidie kumng'oa...hata sasa ninapohutubia hapa, Ngeleja yuko wilayani Magu kuendelea kuibomoa Chadema," alisema Wenje.
Pia Wenje alisema amekasirishwa sana na hatua ya Ngeleja kuendesha kikao cha ndani katika ukumbi wa jengo Chama Kikuu cha Ushrika cha Mkoa wa Mwanza jimboni kwake Nyamagana Januari 7, mwaka huu na kupokea wanachama 30 kutoka Chadema kutoka Wilaya za Magu na Kwimba na hivyo kutishia maslahi ya Chadema.
"Siko kwa ajili ya kusema mazuri wala kuipa ujiko serikali ya CCM au wabunge wake akiwemo Ngeleja, bali nipo kwa ajili ya kutetea na kulinda maslahi ya Chadema ili kuibomoa CCM," alisema.
CHANZO: NIPASHE