Ndoa inayokuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa, na jinsi ya kuivunja

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,411
Leo tuanze na swali..

Je unamiliki simu janja? Namaanisha smartphone?

Kama umeweza kusoma hapa nina uhakika kwa asilimia 90 ya kwamba unamiliki kifaa hiki.

Sasa linakuja swali la pili, ni mara ngapi unaishika simu yako kwa siku?

Labda hili linaweza kuwa swali gumu, maana kwa wengi ni vigumu kuhesabu. Basi tuligeuze na liwe hivi; unaweza kukaa muda mrefu kiasi gani bila ya kushika simu yako?

Nimeanza na maswali hayo rafiki yangu kwa sababu leo tunakwenda kuangalia ndoa moja ambayo umeingia na inakuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. hili ni jambo zito sana na unahitaji kuwa makini nalo hivyo ni muhimu twende pamoja katika makala hii na uamue kuchukua hatua.

Simu hizi za kisasa ni moja ya mapinduzi makubwa ya kiteknolojia ambayo yanatokea kwenye zama hizi, yaani yanatokea tukiwa tunaona. Na uwepo wa mitandao ya kijamii kunaleta mapinduzi mengine makubwa sana. Sasa hivi mawasiliano yamerahisishwa sana, na tulitegemea maisha yawe bora kwa ubora huu wa teknolojia na mawasiliano.

Lakini cha kushangaza ni kwamba maisha hayawi bora, hasa kwa wengi, na chanzo kikuu ni maendeleo haya ya teknolojia na mawasiliano. Maendeleo haya yamekuja kuwa kikwazo kwa wengi kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Simu hizi za kisasa zimekuwa sehemu ya maisha yetu kiasi kwamba tunaona maisha hayawezekani tena bila ya simu hizi. Hivyo kwa masaa 24 ya siku, mtu hawezi kukaa umbali wa mita tano na simu yake. Anatembea nayo kwenye mfuko, akiwa kwenye kazi anaiweka karibu, na hata akienda kulala anaiweka kwenye umbali ambao akinyoosha tu mkono anaifikia. Na hata kama simu itaisha chaji, basi atahakikisha anapata sehemu ya kuchajia ambayo ipo kwenye urefu wa mkono wake, yaani akinyoosha tu mkono anaifikia.

Hivi ndivyo unavyofanya kila siku, au angalau mara nyingi. Simu hizi zimeacha kuwa sehemu ya maisha yetu na badala yake zimeanza kutawala maisha yetu. Tumekuwa hatupati tena raha ya kufanya kitu, kwa sababu mawazo yetu hayawezi tena kukaa kwenye kitu tunachofanya, muda mwingi yapo kwenye simu. Unakula lakini hupati nafasi ya kufurahia chakula, badala yake unakula huku umeshikilia simu, unaperuzi mitandao na kujibu jumbe za watu. Mbaya zaidi hata usingizi, moja ya vitu muhimu sana kwenye maisha yako, unakosa thamani kwa sababu ya kifaa hiki. Unakaa nacho karibu yako kiasi kwamba mtu yeyote anaweza kukatisha usingizi wako kwa muda wowote anaoamua yeye, hata kama hana jambo la msingi analotaka kwako.

Kuna mengi sana ambayo yamefanya maisha yetu kuwa hovyo kutokana na maendeleo haya. Sasa hivi hata watu waikutana watakuwa pamoja kwa dakika chache tu, baada ya hapo kila mtu anainamia simu yake, anakazana asipitwe na kitu. Nafikiri watu walioishi miaka 500 iliyopitwa wakiletwa leo duniani wataona karibu kila mtu amechanganyikiwa. Kwa sababu watashangaa kuona watu wamekaa pamoja ila ni kama wana huzuni, kila mtu ameinama kama analia, kumbe wanaangalia simu zao.

SOMA; MITANDAO YA KIJAMII; JE NI BARAKA AMA LAANA KWAKO?

Moja ya mapinduzi makubwa yaliyoletwa na simu hizi za kisasa ni kuwaleta pamoja walio mbali, na kuwapeleka mbali walioko karibu. Yaani kama mimi na wewe tumekutana, ukaribu wetu unaondolewa pale ambapo kila mmoja wetu anaanza kutumia simu yake.

Ugumu wa kuvunja ndoa hii ambayo inatugharimu unatokana na vitu viwili;

Moja, hali ya kuona kwamba unapitwa. Kuna hali fulani ambayo watu wamejijengea kwamba kama usipoangalia simu yako mara kwa mara basi utapitwa na vitu vizuri. Lakini hii siyo kweli, na hata kama ni kweli basi siyo vingi sana unavyopitwa navyo. Unahitaji nguvu kubwa kuweza kuvunja hali hii.

Mbili, ni hali ya kuona utakosa fursa au kutatokea dharura. Watu wengi sana huwa wanadai simu ndiyo zinawaletea madili mbalimbali, ni kweli kwa baadhi ya watu, ila kwa wengi siyo kweli. Na hata wale ambao ni kweli, bado kukaa na simu masaa 24 siyo njia nzuri ya kupata madili mazuri. Bado unawez akupata madili mazuri kwa kutengeneza mfumo wako wa mawasiliano kuwa bora.

Sasa unawezaje kuvunja ndoa hii ambayo inakugharimu mafanikio yako?

Nianze kwa kusema hii siyo kazi rahisi lakini inawezekana. Na unahitaji kuamua kufanya kweli maana bila hivyo utajikuta unarudi nyuma.

1. Heshimu muda wako muhimu.

Kwa vyovyote vile usiruhusu simu iingilie muda muhimu sana kwako. Na muda muhimu ni upi?

Kwanza tuanze na kulala, unapolala zima simu yako, hakuna kikubwa utakachopoteza na hata kama kuna dharura imetokea saa tisa ya usiku, hakuna kikubwa unachoweza kufanya kwa kupewa taarifa muda huo. Heshimu usingizi wako kwa kuzima simu yako unapolala.

Pili unapopata nafasi ya kuongea na mtu yeyote basi weka simu yako pembeni. Hakuna kitu kinaumiza kama unaongea na mtu huku yeye anatumia simu. Na kwa kuwa bize na simu unayakosa mengi mazuri kwa yule unayeongea naye. Weka simu yako mbali unapokuwa na mazungumzo na wengine.

Tatu kuwa na muda wako maalumu ambao unakaa wewe kama wewe, bila ya simu bila ya usumbufu mwingine wowote. Huu ni muda wa kuyatafakari maisha yako, kutafakari kule unakokwenda na kuagalia changamoto unazopitia. Katika wakati huu usiwe karibu na usumbufu, hasa simu.

2. Tumia mitandao ya kijamii kwa akili.

Na nasema kwa akili kwa sababu matumizi ya mitandao ya kijamii kwa wengi siyo ya akili. Wengi wamekuwa wakiruka ruka tu kwenye kila mtandao. Mtu mmoja yupo kwenye mitandao zaidi ya mitano na kote anatembelea kila mara. Mtu mmoja yupo kwenye makundi zaidi ya matano ya wasap na kote hakuna kikubwa anachovuna zaidi tu ya kupewa habari ambazo hazina mchango kwenye maisha yake.

Chagua ni mitandao ipi ya kijamii utakuwa unatumia, na ambayo inakunufaisha. Na kuhusu wasap, hakikisha unakuwa kwenye makundi ambayo yana manufaa kwako, na manufaa haya ni kukuunganisha na watu muhimu kwako, au unajifunza au unakutana na watu ambao mnaweza kufanya mengi zaidi. Lakini haya makundi mengine ya habari za udaku, au vichekesho yanakupotezea muda wako.

SOMA; Hivi Ndivyo Mitandao Ya Kijamii Inavyoharibu Akili Yako, Kuwa Makini.

3. Tenga muda maalumu wa kutembelea mitandao ya kijamii.

Najua kwa sasa kila baada ya dakika chache unachungulia ni nini kinaendelea huko kwenye mitandao. Huenda hazipiti dakika tano unaingia na kuangalia. Sasa kwa njia hii huwezi kufanya kazi yoyote bora kwako. Badala yake tenga muda maalumu ambao utaingia kwenye mitandao hii, na usiwe muda mrefu. Katika muda huu pitia yale ambayo ni muhimu mengine achana nayo. Muda mwingine unaobakia ondoka kwenye mitandao hii na fanya kazi.

4. Itawale simu yako na siyo simu ikutawale wewe.

Mwisho kabisa ni wewe kudai utawala wako. Kwa kuamua ni wakati gani ukae na simu na wakati gani huhitaji simu. Ni wewe uamue wakati gani upokee simu na wakati gani usipokee. Na siku moja moja, angalau mara moja kwa mwezi uweze kukaa siku nzima bila ya simu au mtandao. Ni lazima udai utawala wako, kwa njia yoyote ile ni wewe unahitaji kuwa unaiendesha simu, na siyo simu ikuendeshe wewe.

Simu za kisasa na mitandao ya kijamii ndiyo changamoto kubwa sana tunayopitia kwenye kizazi hiki. Ni vyema ukalijua hili na kulifanyia kazi. Kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda ndivyo watu wengi wanaishia kuwa wateja wa simu na mitandao. Ukishakuwa mteja huwezi tena kufanya mambo yako kwa uhuru.

Nakutakia kila la kheri katika kuvunja ndoa hii inayokuzuia kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz
 
Safi kabisa kijana wangu, ni lazima tujifunze kujitawala na si kutawaliwa. Nikifka ofisini huwa nazima data kabisa sitaki kuingia WhatsApp na nikipata muda kidogo kama muda huu wa chai nachungulia kwa pozi hahhahaaa
 
Kwa maana ya ulinganifu unataka kutuambia kuwa wajima walipata mafanikio makubwa kuliko waishio zama hizi za technology?

Zama zenu ingewachukua wiki nzima kumfikishia taarifa za msiba ndugu yenu aliyeko lindi (kama unaishi dar)

Jipange na uelewe kuwa kila zama na kitabu chake.
 
Mkuu umetema madini haswa.
Hakuna madini yoyote hapo, ni uoga tu umeifunika akili ya mtoa mada!
Namfananisha na mzee wa shairi la "KARUDI BABA MMOJA" anawaambia wanae eti "kama mnataka mali mtaipata shambani" kwa maana kwamba yeye hakuitaka hiyo mali! maana hakusema kwa nini anakufa masikini hali ya kuwa kanuni ya kuwa tajiri anayo!!!!!!!
 
Back
Top Bottom