PENZI TATA KWELI TATA
Choveki mtani wangu, kwako ninarudi tena
Si mpya mada yangu, ulosema nayakana
Mimi mjuzi wa tangu, mapenzini si wajana
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Mapenzi kweli ajali, ajali iso na kinga
Hata wale marijali, waweza patwa ujinga
Duni ikawa akili, penye hoja wakapinga
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Waonyesha limbukeni, mapenzi bado kujua
Tena kwako ni mageni, na sasa yakusumbua
Hali yako iko duni, moyoni unaugua
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Ni lini utazinduka, kwa mola nakuombea
Ona ulivyo dhofika, mapenzi yakuchezea
Tatizo la kwako kaka, binti wamshobokea
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Na kwangu sio mageni, mapenzi ninakwambia
Ninae wangu mwandani, wa pwani kwa asilia
Si mtu wa kisirani, upole yake tabia
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Kutwa kuchwa twapeana, sasa nakusimulia
Twajua kuridhishana, kwa mia asilimia
Si usiku si mchana, penzi twalifurahia
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Mtani upo ta'buni, kweli nakuhurumia
Tatizo lako huoni, na sifa wamiminia
Binti yule nuksani, mbeleni utaja jutia
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Na wacha kudanganyia, ladhae yashinda pipi
Penzi hajakupatia, watulaghai kwa lipi?
Mtani wajisumbua, pale penzi halilipi
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Wazidi kutushangaza, hujui usipopendwa
Kwa mema unamjaza, ila bado unatendwa
Fanya hebu kutangaza, "penzile" umelishindwa
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Penzi tata penzi gani, ona hizo hati hati
Umebaki ujivuni, binti apaishwa chati
Shida yote hiyo nini, yeye kwako hana dhati
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Na wengi tumeshauri, ila hutaki sikia
Umejawa na kiburi, ya kwetu wapuuzia
Kaa chini tafakari, muda utaujutia
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Kwa hoja tunazojenga, vipi hutaki kuona
Ni vyema ukamtenga, sema mwambie hapana
Binti huyo wa kuringa, kaka mtaja shindwana
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
Na hapa nasimamia, ila hoja zingatia
Lengo si kukusakama, ni mema nadhamiria
Nae mola wa rehema, akupe yaso kadhia
PENZI TATA KWELI TATA, NI LINI UTAZINDUKA
SINDANO MWANA WA GANZI (SMG)
KIJIJINI TONGOLEANI