R.B
JF-Expert Member
- May 10, 2012
- 6,296
- 2,575
Mbunge wa Rufuji Mohamed Mchengerwa.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Mparange na mjumbe wa serikali ya kijiji cha Ikwiriri Kaskazini, wilayani Rufiji mkoani Pwani, Michael Lukanda, ameuawa kwa kupigwa risasi ya kichwani na watu wasiojulikana.
Watu hao wanadaiwa kuwa ni wawili waliotumia usafiri wa pikipiki ambapo mmoja walimpiga risasi marehemu mlangoni akiwa anataka kuingia nyumbani kwake kisha walitokomea. Tukio hilo limefuatia baada ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mparange kijijini hapo, Bakari Mpanawe kunusurika kifo baada ya kupigwa risasi ya tumboni na mkononi march 19.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, alikiri kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia march 29. Alisema tukio hilo ni la tano kutokea ndani ya mwezi huu, likihusisha uhalifu wa kutumia silaha za moto. Kamanda Lyanga, alieleza kwamba wanaendelea kuwasaka watu waliohusika kufanya matukio hayo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria .
Kwa upande wake, Katibu wa CCM wilayani Kibiti, Zena Mgaya, alisema hali ya kiusalama sio shwari katika baadhi ya maeneo wilaya ya Kibiti na Rufiji kijumla.
Alisema hali hiyo inajenga hofu kwa viongozi kupitia CCM ambao baadhi yao wameamua kukimbia miji kwa kuhofia kuuawa.
Zena alibainisha kwamba,matukio ya aina hiyo yanawasababishia kuishi pasipo na amani na wanaCCM kuhofia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo za chama na serikali za vijiji na vitongoji.
Alihamasisha wanaCCM kugombea nafasi mbalimbali bila kuweka uoga kwani kifo kinapangwa na Mungu. Nae Diwani wa kata ya Dimani, Ramadhani Manyema, alisema kuna wenyeviti wa vitongoji na vijiji vinne wamekimbia miji yao wakihofia maisha yao .
Alisema kukimbia maeneo yao ya kazi kumetokana na kutokea matukio ya hivi karibuni ambapo kuna Mwenyekiti wa kijiji cha Nyambonda pamoja na wenyeviti wa vitongoji viwili na mtendaji wa kijiji hicho kupigwa risasi.
Maeneo mengine ni Jaribu Mpaka ambako OC CID na mgambo wa maliasili walipigwa risasi na kufariki na huko eneo la Kifugo tendaji alijeruhiwa kwa kupigwa risasi.
Manyema alieleza, hali ya kiusalama sio shwari hivyo wanatilia mashaka kama watafanikiwa katika zoezi la uchaguzi wa chama.
Aliliomba jeshi la polisi mkoani Pwani, lishuke vijijini ambapo hali sio nzuri pasipo kukaa mjini pekee. Akizungumza katika ziara yake wilayani Kibiti, Katibu wa CCM mkoani Pwani, Hassan Mtenga aliwataka wazazi na walezi kuwafuatilia nyendo watoto wao kwani wapo vijana wanaotumika kwenye matukio ya kiuhalifu. Mtenga alisema ifikie hatua ya watu kubadilika kwa kuacha kuficha wahalifu kisa ni ndugu ,jamaa ama marafiki .