Mwendo kasi unauwa mheshimiwa..Punguza kidogo la sivyo traffic police watakuchukulia hatua

Apr 18, 2012
95
213
MWENDOKASI UNAUA!!

DEMOKRASIA NI NINI?

DEMOKRASIA ina maana pana sana katika uwanja wa siasa. Asili ya neno Demokrasia linatokana na lugha ya Kiyunani (Kigiriki) ambalo msingi wake ni maneno mawili "DEMO" ambalo maana yake ni WATU na "KRATOS" likiwa na maana ya UTAWALA . Kwa kifupi maana ya neno ni "Utawala wa Watu", kwa kumaanisha matakwa ya watu wengi. Na kinyume chake ni Autokrasi yaani Udikteta.

Kwa maneno mengini Demokrasia maana yake ni wengi wape au kuyakubali na kuheshimu maamuzi ya wengi. Kwa maana hiyo mtu hawezi kuwa mwanasiasa, bila kuwa mwanademokrasia, lakini inawezekana kuwa mwanademokrasia pasi na kuwa mwanasiasa. Kwa kuwa demokrasia ndio msingi mkubwa wa siasa, hivyo mwanademokrasia anaweza kuwa mwanasiasa mzuri kwa sababu ana msingi madhubuti wa kuelekea kuwa mwanasiasa.

Hata hivyo, mtu anaweza akawa na sifa zote hizo mbili na pia inawezekana akawa hana sifa hata moja katika hizo, lakini akajipa sifa hizo kwa nguvu. Kwa kukamilika, mwanasiasa mzuri lazima awe pia mwanademokrasia. Mwanasiasa mzuri lazima awe mtu mtaratibu, mpole, mstaarabu na mwenye kushauriana na wenziwe na awe anakubali kukosolewa.

Kubwa zaidi awe mwenye subira na mstahamilivu. Mtu akipungukiwa na sifa hizo, anakuwa ameikosa mihimili ya kuwa mwanasiasa.

Mwanasiasa siku zote huwa mkweli na muaminifu anayoyasema hayatofautiani na anayoyatenda. Kwa sababu wapo waliojipachika 'uwanasiasa", maneno yao ni tofauti kabisa na vitendo vyao, watu hao hatuwezi kuwaita wanasiasa bali ni wababaishaji tu wa siasa.

Nchini Tanzania tangu uanze mfumo wa vyama vingi, mwaka 1992 takriban watu wengi wamejifanya "wanasiasa" na wengine hata kufikia kuamua kuunda vyama vya siasa. Kwa kuangalia nyendo za watu hao inaonekana wanapenda tu, kuwa wanasiasa bila ya kuwa na misingi ya uwanasiasa. hivyo wanashindwa hata kukaribia kufikia hadhi ya uwanasiasa.

Katika kufuatilia kwa karibu nyenendo za baadhi ya wanasiasa, imebainika kuwa huwa wanatafuta kura za wananchi ili ziwawezeshe kutimiza matakwa yao ya kujipatia umaarufu, maslahi binafsi na kutambulika ili waweze kupata madaraka.

Kigezo na kipimo kikubwa cha kumfahamu mwanasiasa, kiko katika kuangalia nyendo zake na kuzilinganisha na misingi ya demokrasia. Misingi hiyo inazingatia Uhuru na Haki, kupinga aina zote za ubaguzi, ama wa rangi, kabila, dini, jinsia au umajimbo na kutoa haki ya kila mtu kushiriki katika mambo ya utawalawa katika nchi. Jambo la muhimu katika misingi hiyo ni nidhamu na si matumizi ya mabavu inayolazimisha wacheche wakubaliane na matakwa ya wengi, na wengi waheshimu maoni ya wachache, kila mtu awe na haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi.

Kwa mtazamo huo demokrasia inaweza kuwepo mahali popote ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa au katika mfumo wa chama kimoja mradi tu, misingi hiyo mikubwa inafuatwa. Hivyo demokrasia nchini Tanzania ilianza tangu enzi ya mfumo wa chama kimoja.

Katika kuangalia asili na misingi hiyo ya demokrasia, napata mashaka makubwa juu mwelekeo wa hali ya dhana nzima ya demokrasia hapa Tanzania. Pamoja na kwamba tunahubiri kuwa tunafanya chaguzi za kidemokrasia na nchi yetu kuwa ya kidemokrasia ni kweli kwamba yale tunayoyahubiri na kuyatenda hayasadifu kabisa msingi na dhima kuu ya demokrasia.

Hebu tuangalie maana ya udikteta:

"Udikteta ni mfumo wa Utawala wa nchi ambapo mtu mmoja asiyebanwa na sheria wala Katiba anashika madaraka ya serikali na ana uwezo wa kuyatumia jinsi anavyoamua mwenyewe" Mtu huyu anaitwa "dikteta" ingawa cheo rasmi mara nyingi ni "Rais" au Kiongozi wa taifa".

Katika misingi ya kidikteta, uhuru wa maono unabanwa na hata kupigwa marufuku kabisa. Serikali inasimamia vyombo vya habari hii inaweza kuwa moja kwa moja au kwa kuweka sheria kandamizi. Vyombo hivyo ni kama magazeti, redio na televisheni. Vyombo hivyo hudhibitiwa kutoa maoni ambayo hayaipendezi serikali.

Sambamba na hilo udikteta hauruhusu upinzani unaoendelea kueleza uhusiano kati ya makosa madogo na makubwa na muundo wa serikali. Upinzani dhidi ya viongozi wa juu haukubaliwi.

JE, tunaweza kuhusianisha hali ya demokrasia na udikteta katika nchi yetu kwamba ni mambo yanayokwenda kwa Pamoja au moja lipo ndani ya jambo lingine?

Naomba tutafakari kwa Pamoja kwa kina.Wakati tukiendelea kutafakari tujikumbushe kuwa Mwendokasi unaua!! Tunapokuwa na Mwendokasi katika maamuzi tunaharibu dhana nzima ya Utawala wa Sheria, Tunapokuwa na Mwendokasi katika matamshi yetu, tunaharibu dhana nzima ya Kuitwa Viongozi wenye hekima, tunapokuwa na Mwendokasi katika kila aina ya mambo ya msingi kwa mustakabali mwema wa taifa hili tunatengeneza taifa goigoi lakini ambalo mwisho wa siku litakuwa ni taifa lenye chuki dhidi ya waliasisi Mwendokasi huo!! Tunatengeneza taifa lisilokuwa na amani!!

Mwendokasi Unaua!!
Mwendokasi Unaua!!
Mwendokasi Unaua!!!!

Tutafakari kwa hoja kwa Pamoja!
 
Back
Top Bottom