mvua yabomoa nyumba zaidi ya 300 na kuacha 800 bila makazi

thesym

JF-Expert Member
Aug 15, 2012
3,827
4,757
mvua..jpg

Dodoma. Zaidi ya watu 800 hawana makazi baada ya nyumba walizokuwa wakiishi 358 kubomolewa na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia jana mkoani hapa.

Mvua hizo zilisababisha mafuriko makubwa katika kata za Mpunguzi, Matumbulu, Nzuguni na Dodoma Makulu zilizopo Manispaa ya Dodoma na ya Kigwe wilayani Bahi.

Mbali na nyumba kubomoka, familia nyingi hazina vyakula na nguo baada ya kusombwa na mafuriko.

Vilevile, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mpunguzi vitu vyao vilisombwa na maji.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mpunguzi na Matumbulu, Dionisi Samo alisema nyumba 70 zilibomoka katika eneo hilo na kuwaacha watu 300 hawana makazi.

Samo alisema maji yaliyovunja ukuta wa barabara yaliingia kwa wingi kwenye makazi ya watu na kubomoa nyumba za udongo.

Diwani wa Kata ya Kigwe, Paschal Sijila alisema nyumba 270 zilianguka katika kata yake na kuwakosesha watu 460 makazi.

Sijila alisema mafuriko hayo ni ya mara ya pili katika kipindi cha mwaka huu pekee.

“Kikubwa ambacho tunakiomba ni Serikali kufika hapa na kuwatafutia watu mahali pa kuishi, hawana nyumba, vyakula vimesombwa na maji, kuku wapatao 16 wamekufa na viongozi nilishawaambia wakaniahidi kuwa watakuja,” alisema Sijila.

Diwani wa Kata ya Makulu, Paschal Matula alisema nyumba 18 zimebomoka wakati Kata ya Nzuguni mafuriko yamevunja daraja upande mmoja hali iliyosababisha baadhi ya watumishi na wanafunzi kushindwa kwenda kazini.

Katika eneo la Mto Msangambijili Nzuguni, baadhi ya watu walikuwa wakivushwa kwa kubebwa mgongoni kwa malipo ya kati ya Sh500 na Sh1,000 huku wenye magari wakilazimika kuyaacha na kuvushwa ili kupanda daladala na kuwahi kwenye shughuli zao za ujenzi wa Taifa.
Source: mwananchi
 
Back
Top Bottom