Muujiza wa Tundu Lissu

Double Elephants

JF-Expert Member
Mar 25, 2013
522
464
JARIBIO LA KUMUUA TUNDU LISSU - SIMULIZI KUTOKA NAIROBI

Na: _Dr. Milton Makongoro Mahanga_

Wahaya kwa upande mmoja na wanyaturu na wanyiramba kwa upande mwingine ndio watani wa asili wa sisi waluo. Lakini tofauti na wahaya ambao mara nyingi hawataki kukubali kwamba ni "wajukuu" zetu, wakidai kwamba wao ndio "mababu", jambo ambalo ni kinyume, wanyaturu na wanyiramba wao hukubali kabisa kwamba ni wajukuu zetu waluo.

Hivyo tarehe 04/01/2018 saa 9.45 alasiri tulipoingia kwenye chumba cha wagonjwa cha Mhe. Tundu Antiphas Mughwai Lissu (Mb) katika hospitali ya Nairobi tukiongozana na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara, Mhe. John John Mnyika (Mb) na viongozi na wananchi kadhaa, mara baada ya kuniona tu, Mhe. Lissu akatamka "Babu, kama na wewe umekuja kuniona, basi nimeshapona". Nikamjibu "nimekuja mjukuu na Inshallah umepona!". Wote tukacheka. Nikampa pole nyingi na hongera kwa madhila aliyoyapata kutoka kwa "watesi" wake, na shukrani kwa Mungu na madaktari kwa kumweka salama. Hakika Mungu ni mkubwa! Kiongozi mmoja tuliyeongozana naye akasema kwa utani lakini kwa imani kubwa, "Kwa kawaida Mungu hushusha malaika wake kuwaokoa waja wake pale wanapopata matatizo makubwa, lakini kwa Lissu, naona Mungu alishuka mwenyewe kumfunika na kumlinda!" Wote tukacheka.

Niliposema neno "watesi" Lissu akaniuliza "babu na wewe vipi yule mtesi wako?" (na mimi nina "mtesi" wangu ingawa siyo kwa kiwango chake yeye - not to that extent!). Tukacheka tena, huku nikimkumbusha kwamba ilikuwa ni siku ile ile ya "mateso" yake (fateful day) tarehe 07 Septemba 2017, saa 3 asubuhi kabla hajaingia Bungeni aliponitumia ujumbe mfupi kwa simu akiniandikia "Babu nimeongea na yule mtesi wako na amesema atafikiria ombi lako kisha atanipa jibu".

Masikini "mjukuu" wangu, hata ujumbe wangu mfupi nikimshukuru kwa juhudi zake za kuanza kunisaidia hakuusoma, kwani alipotoka Bungeni saa 7 kabla hajasoma ujumbe huo, alipigwa risasi 16 na watu "wasiojulikana" kwa nia ya kumuua! Aidha hakuweza tena kushughulikia tatizo langu na "mtesi" wangu hadi leo kutokana na yaliomkuta..

Baada ya salaam za awali za pole na pongezi kwa kupona, Mhe. Lissu alianza kutusimulia yote yaliyomsibu na hali yake hadi sasa. Ilikuwa ni simulizi iliyotia uchungu, simanzi, hasira na wakati mwingine furaha na vicheko. Tulitumia muda wa saa 2 na dakika 15 pale chumbani kwake kuanzia saa 9.45 alasiri hadi saa 12 jioni, akisimulia na tukijadili madhila yaliyompata kuanzia hiyo tarehe 07/09/2017 hadi kuokolewa na madaktari na hali yake ilivyo hadi sasa. Aidha tulijadili hatma na mustakabali wa nchi yetu kisiasa na hali ya amani, mshikamano na upendo wa watanzania ilivyo mbaya kwa sasa.

Mhe. Lissu alianza kusimulia yaliyotokea hiyo tarehe 7 Septemba baada ya kutoka Bungeni saa 7 mchana kwenda kwa mapumziko ya mchana nyumbani kwake Area D, Site 3 (maarufu kama maghorofa ya mawaziri). Alinigeukia na kuniuliza "babu wewe wakati ule si ulikuwa unakaa pale pale lakini Block B hapa mwanzoni?", nilipoitikia akaendelea "sasa mimi naishi mwisho kabisa Block E". Aliendelea kueleza kwamba walipofika geti la kuingia kwenye makazi hayo ya Site 3 walikuta geti liko wazi na hakuona walinzi. Waliingia na walipofika kwenye maegesho yao ya Block E walikuta kuna nafasi moja tu ya kuegesha gari na dereva wake akalitumia egesho hilo kuweka gari.

Lakini kabla hawajashuka kwenye gari, dereva akamwambia asishuke kwani ana wasiwasi na gari lililokuwa linawafuata kuanzia maeneo ya Bunge na sasa liko tu nyuma yao. Lissu alichungulia kupitia kioo cha pembeni (site mirror) na akaona gari nyeupe aina ya Nissan likiwa na lenyewe limesimama nyuma yao kwa kukosa egesho. Wakiwa bado wanajiuliza, mtu mmoja aliyekuwa kiti cha nyuma cha gari hilo alishuka na kwenda kuongea na " boss" aliyekuwa kiti cha mbele cha abiria. Aliyeshuka alikuwa amevaa kofia aina ya kapero. Yaonekana alipewa maelekezo na "boss" kwani aliporudi tena kwenye kiti chake cha nyuma ghafla yeye na mwenzake waliyekuwa naye kiti cha nyuma wakatoka nje tena. Huyu wa pili alikuwa amevaa T-shirt nyeupe nyeupe hivi, wote wakiwa wameshika bunduki aina ya short guns. Mara moja walisogea mbele na kuanza kufyatua risasi kwa Lissu. Hawakuja pembeni kabisa kwa gari la Lissu kwa sababu ya magari mengine yaliyokuwa yamejaza maegesho hapo. Kwa hiyo walikuwa wanarusha risasi kwa nyuma lakini kwa upande wa Lissu. Haraka dereva wa Lissu alifungua mlango wake na kutoka nje huku akimvuta Lissu kwa shingo ili aangukie upande wake. Lissu akaangusha kichwa na mwili kwenye kiti cha dereva huku akijiongeza kwa kujivuta hadi kichwa kikawa kinaning'inia nje upande huo wa dereva. Wakati wote huo risasi zilikuwa zinaendelea kumiminika mwilini mwake kuanzia miguuni, mikononi, hadi tumboni, ambayo ndiyo maeneo ya mwili wake yaliyokuwa yamebaki wazi kwa "wauaji" hao.

"Hakika watu wale walitumwa kuniua, ni bahati yangu tu kwamba gari lao halikupata egesho sambamba na gari langu, na pia wauaji hao hawakufikiria au hawakupata muda wa kuzunguka upande wa pili wa dereva ambako kichwa changu sasa kilikuwa kimening'inia. Wangezunguka wangenimaliza", alieleza Tundu Lissu kwa uchungu.

Baada ya kujiridhisha kwamba bila shaka wameshamuua Lissu, wauaji hao walipiga risasi matairi ya magari yaliyokuwa jirani kwa nia ya kutoa upepo na kuondoka mbio kutoka eneo hilo. Watu waliosikia milio ya risasi akiwemo binti aliyekuwa anatunza nyumba ya Lissu walitoka wakipiga kelele. Bahati nzuri kuna dada mmoja aliyekuwa anamjua vizuri Lissu aliyekuwa anaishi pia kwenye ghorofa hiyo alipata akili na kuleta gari lake haraka ndipo walipompakia Lissu kwenye gari hilo na kumkimbiza hospitali ya mkoa wa Dodoma. Kipindi hicho chote Lissu anasema alikuwa na fahamu zake huku akiwaomba watu hao wamjulishe Mwenyekiti Mbowe na familia yake. Baada ya kufika hospitali ya Dodoma madaktari walianza kufanya kazi kubwa ya kuokoa maisha yake. Aliweza kuwaona na kuwatambua baadhi ya waheshimiwa waliokuja haraka hospitalini hapo kumwona, akiwemo Mhe. Freeman Mbowe. Hapo sasa alianza kupata maumivu makali sana, hasa tumboni. Anakumbuka kumwambia Mbowe awaambie madaktari wamkalishe kitandani badala ya kulala akiamini maumivu yangeweza kupungua, lakini madaktari hawakukubali wakijua kumkalisha chini kungefanya damu izidi kutoka kwa wingi zaidi na hata kumpotezea maisha. Baada ya hapo alipoteza fahamu huku madaktari wakiendelea kudhibiti utokaji wa damu na kujaribu kutoa risasi mwilini. Alikuja kupata fahamu wiki moja baada ya kufika Nairobi na kupata huduma ya madaktari bingwa.

"Yaliyoendelea nilikuja kuambiwa baadaye, na hasa baada ya kufika hapa Nairobi na kuendelea na matibabu", anaendelea kusema Lissu. Anasema risasi zilizopigwa na wauaji hao kulingana na waliohesabu matundu ya risasi kwenye gari, zilikuwa takriban 38 lakini zilizoingia mwilini mwake zilikuwa 16 ambapo risasi 8 zilimpiga na kutokea upande mwingine wa mwili huku risasi zilizobaki 8 zikigota maeneo mbalimbali ya mwili. Anasema risasi hizo ziliharibu viungo vya mwili na kuvunjavunja mifupa. Risasi 3 zilivunjavunja mguu wa kulia. Mikono yote miwili ilivunjwa na risasi zingine zikiingia tumboni.

Lissu anasema Dodoma na Nairobi alifanyiwa jumla ya operesheni 17, kati ya hizo 4 akifanyiwa tumboni. Bahati nzuri vidonda vyote vya risasi na vya operesheni kwa sasa vimepona na kukauka. Kuhusu zile risasi zilizogota mwilini alisema madaktari wa Dodoma waliweza kutoa risasi 3, na risasi 4 zilitolewa hospitali ya Nairobi. Hata hivyo risasi moja bado iko mwilini kwenye nyama karibu na mfupa wa uti wa mgongo kwa ndani. Madaktari wamemhakikishia kwamba risasi hiyo haina madhara yoyote. Nilipomuuliza kwamba ndio itakaa humo milele, akajibu, " babu, kama kuna vyuma chungu nzima vimewekwa huko na madaktari, nini shida ikiongezeka chuma (ya risasi) kimoja zaidi?" akacheka. Lakini anasema madaktari wameeleza kwamba kuitoa risasi hiyo ni hatari zaidi kuliko kuiacha humo.

Mhe. Tundu Lissu akatuonyesha maeneo yote yalipoingilia risasi kwenye mikono, magoti, mapaja na tumboni, na jinsi madaktari walivyofanya kazi kubwa ya kutoa risasi mwilini, kuzuia damu kuendelea kutoka, kufunga vidonda na hata kuotesha nyama baadhi ya maeneo kwa nyama kutoka maeneo mengine ya mwili.

Tundu Lissu anawashukuru sana madaktari wa Dodoma na Nairobi kwa kuokoa maisha yake. Figo yake iliyokuwa imefeli nayo ilirudishwa kwenye hali nzuri. Amesema hospitali ya Nairobi ina madaktari na huduma nzuri pengine kuliko hospitali yoyote kwenye ukanda huu wa Afrika. Anawashukuru hasa wafanyakazi, wauguzi na madaktari bingwa wa hospitali ya Nairobi wakiongozwa na daktari bingwa wa mifupa, Dr. Vincent Mutisa, na mwingine wa magonjwa mchanganyiko, Dr. Frank Mongera.

Ameendelea kuwashukuru viongozi na wabunge wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Mhe. Freeman Mbowe, kwa namna walivyohangaikia matibabu yake toka akiwa Dodoma, kufanya mpango wa haraka kumleta Nairobi na kumwezesha mke wake kuwahi kufika Dodoma na kusafiri naye kuja Nairobi. Hapa mkewe Lissu, mama Alicia Lissu alielezea alivyopata taarifa za tukio hilo na namna alivyowahishwa kufika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kupanda ndege ya kumwahisha Dodoma. Alisema ilibidi afike mahali ashuke kwenye gari na kupanda bodaboda na kukatisha njia kutokea Tegeta kupitia Goba, Mbezi Juu na Kinyerezi ili kufika uwanja wa ndege mapema huku akijawa na wasiwasi wa safari hiyo ya bodaboda na hali ya mgonjwa Dodoma.

Lissu anatoa shukrani zake kwa watanzania wote na marafiki wa nje ya nchi waliomwombea, kumchangia gharama za matibabu na wengine kwenda kumwona hospitali ya Nairobi. "Hakika nitaendelea kuthamini upendo huu", anasema. Anamshukuru sana Mungu kumwepusha na kifo, na ukiacha kazi kubwa ya madaktari, anataja miujiza kadhaa zilizotokea na kumwokoa. Kwanza ni wauaji kukuta hakuna egesho sambamba na gari lake ikabidi wamtupie risasi kwa pembeni kidogo kwa nyuma, la sivyo wangemmaliza kirahisi wangekuwa sambamba. Muujiza wa pili ni akili ya dereva kumvuta ili aangukie upande wake wakati yeye dereva akiserereka nje. Tatu, ni risasi za wauaji kukosa kichwa chake, moyo wake na hata mshipa mkuu unaosambaza damu mwilini. Muujiza wa nne ulikuwa kupatikana kwa gari la haraka kumwahisha hospitali. Tano, ni uamuzi wa haraka wa Mwenyekiti Mbowe na chama chake kuamua kwa haraka na kuwezesha asafirishwe usiku huo huo kuja Nairobi, na muujiza wa mwisho ni bahati yake alipofika hospitalini Nairobi aliweza kuvukishwa mstari wa wagonjwa na kupelekwa chumba cha upasuaji mara moja.

Tundu Lissu anasema haya yalikuwa mashambulizi ya mauaji ya kisiasa. Anasema yeye amekuwa mhanga wa mauaji ya kisiasa kutokana na kuikosoa serikali ya awamu ya tano kwa kusema ukweli ambao watawala hawataki kuusikia na kusimamia utawala wa sheria. Amesema kwamba Serikali kutoonyesha kwamba inafanya upelelezi wowote, na kugoma kuruhusu upelelezi huru kunathibitisha kwamba hili lilikuwa shambulio la mauaji ya kisiasa. Mpaka sasa hakuna hata mshukiwa mmoja wa shambulio hili amehojiwa na Jeshi la Polisi la Tanzania. Hata yeye mwenyewe hajahojiwa. Lakini mazingira ya shambulio hilo pia yanaonyesha hivyo. Anauliza, ilikuwaje siku ya tukio geti la mbele la makazi hayo ya site 3 liwe wazi na walinzi wasiwepo? Aidha iliwezekana vipi walinzi wa jengo lao na walinzi wa jengo analokaa Naibu Spika upande tu wa pili nao wote wasiwepo muda huo? Hata kamera za ulinzi (CCTV) kwenye majengo hayo hazikufanya kazi siku hiyo!

Lissu ameonya kwamba yeye ni mfano tu na pengine watanzania wengine wanaweza kujikuta katika hali hii au mbaya zaidi. Lakini hii isifanye watu waache kuhoji watawala pale wanapokosea na kuminya uhuru wa kusema, uhuru wa kukusanyika na uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari. Kwa upande wake anaamini Mungu amemwepusha na kifo ili apone na aendelee kuwaongoza watanzania katika kudai haki yao ya kikatiba na ya kidemokrasia ya kufanya siasa na kuhoji Serikali pale haki zao zingine za kikatiba na kijamii zinapobinywa.

Mhe. Tundu Lissu anatoa wito kwa watanzania na wapenda demokrasia na haki popote duniani wasikae kimya tena kuhusu hali ya Tanzania. Wapaze sauti, waseme ukweli, wapinge maonevu na watetee demokrasia ya kweli nchini Tanzania. Ameomba jumuia za kimataifa, wafadhili na marafiki wa nje wa Tanzania wamweke chini Rais Magufuli wamweleze ukweli ili aache kuendesha nchi kwa mabavu na bila kufuata Katiba na Sheria. Amevitaka vyombo vya habari vya ndani na nje na vyenyewe vipaze sauti bila woga.

Alisema anakwenda Ubelgiji kwa hatua ya mwisho ya matibabu yake ambayo hasa yatakuwa ni kufanyiwa mazoezi ya mwili na viungo, na kuweka mwili sawa. Anaamini atarudi Tanzania akiwa na hali nzuri ya kuendeleza yale anayoyaamini kwa maslahi ya nchi yake.

Mhe. Lissu na viongozi tuliomtembelea tuliendelea kujadili mashambulizi hayo na namna alivyopona kwa miujiza ya Mungu. Tulijadili pia hali ya kisiasa nchini na mikakati ya kufanya siasa za upinzani Tanzania kwa sasa na siku za mbele.

Baada ya hapo tulimuaga Lissu na kumtakia safari njema huko Ulaya kwenye matibabu zaidi. Nilimshika mkono na kumwambia, "mjukuu nakuombea upate matibabu mazuri huko uendako na urudi unakimbia". Akasema "Amen babu, nitarudi ninakimbia".
 
Nampa pole sana Tundu Lisu kwa mateso yote anayopitia. Kwangu nimepata funzo kubwa sana kutokana na mkasa wake na ni vyema vijana kujifunza Kwenye hili kwa wakati wote wa maisha yetu kuwa wenye hekima na busara wakati tunapo shauri suala lolote liwe la kisiasa, kiuchumi au kitamaduni kinyume chake ni kujitengenezea maadui na mateso. Hiki ndicho kilichomkuta lLsu.
 
Awamu ya kwanza ya kumtunza Lissu inafikia mwisho kwa matibabu ya ubelgiji. Asante Mungu kwa kusimamia hilo.

Awamu inayonitia wasiwasi ni ile ya kupona na kuruhusiwa kurudi nyumbani.The way CHADEMA will handle this critical phase is of much concern to me, bearing in mind that the assasins are intent on concluding their mission.

Nawaonya CHADEMA wasije kupasua mtungi wa maji nyumbani.Wasije fanya shamrashamra za kutangaza ujio wa Lissu toka hospitali. Akiruhusiwa wamrejeshe Tanzania kimyakimya mpaka nyumbani kwake Singida. CHADEMA watangaze tu kwamba Lissu keshawasili Tanzania na yuko na familia yake nyumbani Singida.Au kuna kitakachowazuia CHADEMA kufanya hivyo?Jamani naomba mnielewe. Ile mishetani ya tarehe 7/9/2017 inajiandaa 'kumpokea' Lissu airport dsm au kia.
 
Back
Top Bottom