Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 8, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 8, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
108
Simbachawene: Maandamno ya Desemba 9 ni haramu, mtandao utazimwa hali ikiwa mbaya. Polisi wafuate sheria wanapokamata mtuhumiwa, hakuna kuvaa kininja

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema maandamano yanayodaiwa kupangwa kufanyika Desemba 9, 2025 ni haramu na hayakubaliki kisheria. Akizungumza leo Desemba 8, 2025, amesema maandamano hayo hayajawasilishwa kwa mujibu wa sheria, hayajatambulisha waandaaji wake, hayana malengo yanayoeleweka na yanatajwa kuwa yasiyo na ukomo, hali inayoyafanya yasitambuliwe kisheria.

Ameongeza kuwa taarifa za Polisi zinaonesha maandamano hayo yanatangazwa kuwa makubwa kuliko ya Oktoba 29, tukio lililosababisha uharibifu wa mali za umma na binafsi, taasisi za Serikali pamoja na vifo vya watu na kutoa wito kwa Watanzania kutokubali kurudia makosa ya nyuma. Kutokana na hilo, Simbachawene amesema Serikali haiwezi kuyachukulia kama maandamano bali kama viashiria vya vitendo vya mapinduzi, akisisitiza kuwa Vyombo vya Usalama vimejipanga kikamilifu kudhibiti hali hiyo na kulinda amani ya nchi pamoja na kuhakikisha usalama wa kila mtu.

Simbachawene ameisisitiza hakuna atakayelazimishwa kubaki nyumbani isipokuwa kwa sababu za dharura na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao muhimu na kuwa na kitambulisho pamoja na nyaraka nyingine zinazohitajika ili kuepuka usumbufu.

Kuhusu madai ya kuzimwa kwa mtandao, Simbachawene amesema hadi sasa Serikali haijaona sababu ya kufanya hatua hiyo. Alieleza kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ikitumiwa na baadhi ya wanaharakati kusambaza taarifa zenye taharuki, lakini bado haijafikia kiwango cha kuwa tishio la kiusalama kupelekea mtandao kuzimwa, ingawa amesema kuwa mtandao unaweza kuzimwa hali ikiwa mbaya.

Aidha, Simbachawene amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, kuhakikisha ukamataji wa watu unafuata taratibu za kisheria na amepiga marufuku Polisi kuwakamata watu kibabe wakiwa wamevaa kininja, bila sare na wakiwa na silaha nzito. Amesema anataka ukamataji wa wazi na wenye staha, unaofanywa na askari waliovaa sare na kwa kutoa taarifa kwa mtu anayehitajika, ili kuepusha hofu na athari za kisaikolojia kwa familia.

Maoni ya wananchi:
Kuhusu maandamano, wengi wamesema ni haki yao na wamefuata taratibu ya kuvijulisha vyombo vya dola na ndio maana mpaka wakati huu nchi nzima ina ufahamu kuhusu maandamano hayo, na wanachotaka ni vyombo vya usalama kuwapa ulinzi kwa raia watakaojitokeza kuandamana.

Aidha, wengi wamehisi tamko linalowataka Polisi kufuata utaratibu wanapokamata watuhumiwa limetolewa kama namna ya kuwatuliza wananchi kuonyesha Serikali inafanya kazi kukomesha na kutuliza uhalifu. Ingawa, baadhi wameona huu utakuwa mwanzo wa vitendo vya utekaji kukomeshwa kwakuwa wanaotuhumiwa kufanya hivyo ni polisi. Wapo walioanza kumuona Simbachawene kama mtu anayefaa kuongoza nchi kama Rais wakisema ‘alindwe’.

Rais Samia atuma salamu ya Sikukuu ya Uhuru, ashauri wasiokuwa na dharura kubaki nyumbani

Rais Samia, kupitia Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba amewatakia wananchi wote heri ya Sikukuu ya Uhuru wa Tanganyika inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Desemba, huku akiwasihi wananchi ambao hawatakuwa na dharura siku hiyo kuitumia kwa mapumziko na kusherehekea wakiwa nyumbani, isipokuwa kwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vyao vya kazi kwa mujibu wa maelekezo ya viongozi wao.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamehoji kwanini ujumbe huo umewasilishwa na Waziri Mkuu wakati Makamu wa Rais yupo?

Wengine wametafsiri ‘ushauri’ wa kutotoka nje kama ‘amri’ kutoka kwa Serikali, na kwamba huenda yaliyofanyika Oktoba 29 yakajirudia na watu wengi zaidi wakapoteza maisha na kujeruhiwa safari hii, hasa kwa kuwa wananchi wameahidi kufanya maandamano hayo kwa amani na kujizuia na vitendo vyovyote vinavyoweza kutaleta vurugu au uharibifu wa mali.

Ubalozi wa Ufaransa washauri Raia wake nchini kubaki majumbani Desemba 9

Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania umewashauri raia wake waliopo nchini kubaki majumbani tarehe 9 Desemba 2025, kufuatia mwongozo uliotolewa na Rais Samia kuwataka wananchi kubaki majumbani mwao kama hakuna ulazima wa kutoka nje.

Katika taarifa yao, ubalozi umesisitiza kuwa raia hao wanapaswa kutoka majumbani mwao endapo tu kutakuwa na hali ya dharura, kama hatua ya tahadhari na usalama.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamesema tangazo hilo ni kutokana na tishio la kiusalama, amani na utulivu nchini tofati na ambavyo Serikali imekuwa itingaza na kujipata, maana wangejihisi salama wasingekuwa na ulazima wa kutoa tangazo hilo na hilo linachangiwa zaidi na nguvu kubwa inayotumiwa na vyombo vya dola.

Hofu ya maandamano Desemba 9 yapelekea msongamano wa manunuzi wa mahitaji muhimu kwenye masoko na maduka

Msongamano mkubwa wa wananchi umeshuhudiwa katika masoko na maduka makubwa maeneo mbalimbali nchini, hususan jiji la Dar es Salaam ambapo watu wameonekana wakinunua mahitaji muhimu kama chakula, maji na bidhaa za matumizi ya nyumbani kwa wingi kutokana na hofu ya maduka kufungwa wakati wa maandamano.

Wananchi wengi wanasema wanajipanga mapema kutokana na uwezekano wa kukosekana kwa bidhaa iwapo hali ya kiusalama na kisiasa itayumba. Baadhi wamesema hawataki kurudia makosa ya Oktoba 29, ambako walijikuta wakiishiwa vyakula huku kukiwa na hofu ya kutoka nje kutokana na wananchi kuuliwa ovyo hata walipoonekana nje ya nyumba zao, huku wengine wakifuatwa ndani kabisa na kuuliwa mbele ya familia zao.

Aidha, hali imekuwa tofauti kwa wanaotegemea kipato cha kila siku kununua mahitaji yao kutokana na bidhaa nyingi kuisha madukani na masokoni, huku nyingine zikipanda bei kuliko kawaida na hivyo kuongeza ugumu kwa wao kumudu gharama za mahitaji yao.

Rais Samia akutana na Kaimu Balozi wa Marekani na kufanya mazungumzo; wakubaliana kumaliza mazungumzo ya miradi ya madini na gesi asilia

Rais Samia amefanya amezungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma, Desemba 8, 2025 ambapo baadhi ya masuala yaliyojadiliwa ni kukuza maeneo muhimu ya ushirikiano baina ya Tanzaniaa na Marekani na kuthibitisha dhamira ya pamoja ya kuendeleza ushirikiano wa kisiasa wenye manufaa kwa mataifa yote mawili, mageuzi ya kiuchumi, usalama wa kikanda pamoja na fursa za kubadilishana uzoefu kati ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

Pia pande hizo mbili zilikubaliana kumaliza mazungumzo ambayo yako hatua za mwisho, ikiwemo mradi wa LNG (mradi wa gesi asilia wenye thamani inayokadiriwa Dola za Kimarekani bilioni 42), Tembo Nickle (uwekezaji kwenye madini ya Nikeli wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 942) pamoja na Mahenge Graphite (mradi wa uzalishaji wa madini ya Grafiti).

Rais Samia amesema kuwa Tanzania kama taifa lisilofungamana na upande wowote iko wazi na tayari kushirikiana washirika wote wanaoheshimu uhuru na kuthamini maono yao ya ustawi.

Maoni ya Wananchi:
Wengi wamesema Rais baada ya kauli yake “Who are you” kwa mataifa ya nje na taasisi za kimataifa zinazochangia bajeti ya Tanzania kwa kiwango kikubwa kwenye miradi ya maendeleo, ameanza kujishusha na kusikiliza ushauri wa wataalamu pamoja na wananchi juu ya kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia, japokuwa wengi wanaona hilo linaweza kubadilika muda wowote ikiwa wananchi wataendelea kusisitiza andoke madarakani pamoja mataifa hayo kuwa upande wa wananchi.

Wengine wameona taarifa hiyo kutolewa siku moja kabla siku iliyopangwa kufanywa maandamano ni mkakati wa kuwaonyesha wananchi kuwa mataifa ya Magharibi na hasa Marekani wapo pamoja na Serikali, na hivyo kupunguza ari ya kuandamana kwa kuona hakuna anayewaunga mkono katika juhudi hizo za kutafuta ‘Haki’.
 
Back
Top Bottom