Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 6, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 6, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
108
Mohamed Ali Kibao alalamikia ukimya wa mamlaka kuhusu mauaji ya Baba yake, Mzee Ali Kibao, awashauri Rais na Waziri Mkuu kukiri yaliyotokoea

Zaidi ya mwaka mmoja tangu kuuawa kwa Mzee Ali Kibao September 2024, Mohamed Ali Kibao, mtoto wa marehemu ametoa malalamiko kutopata majibu yoyote kutoka kwa mamlaka licha ya kufuatilia kwa muda mrefu.

Amesema kinachowasikitisha zaidi ni kuona nguvu kubwa zikielekezwa katika kulinda maslahi ya watawala huku wananchi wa kawaida wakikosa haki, akirejea tukio la kijana aliyechana picha ya Rais kupotea na hatua dhidi ya Askofu Gwajima kufungiwa kanisa baada ya kukemea utekaji na watu kuuawa.

Mohamed ameongeza kuwa hali ya hofu nchini imefikia kiwango cha kutisha, kiasi cha watu kuogopa hata kutoa pole kwa familia za wafiwa. Amesema yeye binafsi hupokea maonyo ya kuwa makini bila kuelewa kosa lake, jambo analoliona kama taswira ya taifa lililokosa uhuru wa kuomboleza, kuuliza maswali au kutafuta haki bila kuogopa vitisho.

Ameshauri Rais na Waziri Mkuu kusikiliza na kukiri kilichotokea, akisisitiza umuhimu wa kutathmini matukio ya ukosefu wa usalama na haki, akitaja mifano ya Lissu kupigwa risasi, Polepole kupotea, Soka kupotea na Mzee Kibao kuuawa. Mohamed amesema uongozi uliokubalika utapiganiwa na watu wenyewe, ukiona kikundi kinaweza kuleta vurugu ujue kuna tatizo kubwa zaidi.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamekubaliana na yote aliyosema Mohamed, wakisema utawala wa sheria ni kama haupo, matukio ya watu kuuawa na kutekwa yakionekana kuwa ya kawaida na kuzoeleka huku imani kwa vyombo vya usalama ikiendelea kuporomoka kutokana na kuhusishwa na matukio hayo yanayofanya kwa maslahi ya viongozi wachache.

Askofu Bagonza: Gen-Z sitisheni maandamano, Disemba 9 iwe mazishi ya kitaifa

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, kupitia ukurasa wake wa Facebook, ametoa wito kwa vijana wa Gen-Z kutafakari na kusitisha maandamano yaliyopangwa Desemba 9, akieleza kuwa tayari dunia nzima, taasisi mbalimbali na hata mamlaka za ndani zimeonyesha msimamo wao kuhusu kile kinachoendelea nchini.

Amesema mazingira ya sasa yamejaa utashi, hofu na mkanganyiko, huku watekaji, viongozi wa dini, wananchi na hata wahusika wa usalama wakitoa matamko yanayoonyesha hali ya taifa ilipofikia. Askofu Bagonza ameonya kuwa chanzo cha sintofahamu ni utekaji unaoendelea, akisisitiza kuwa asiyekemea utekaji ndiye mtekaji.

Katika wito wake, amesema Tanzania imejengwa kwa miaka 60 lakini imebomolewa katika siku chache kutokana na kukosa usikivu na uwajibikaji. Ameshauri Serikali kusitisha vitendo vya utekaji na kauli za kufoka, huku Gen-Z nao wakisitisha maandamano ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya kitaifa. Aidha, amependekeza siku ya Desemba 9 itumike kama siku ya mazishi ya kitaifa kwa waliopoteza maisha, na kusisitiza kuwa risasi inaweza kuua mtu lakini haiwezi kuua mawazo.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamepinga wito wa kusitisha maandamano, wakisisitiza kuwa hawawezi kuwasaliti waliouawa katika ‘utawala batili’, na kwamba mazishi ya kitaifa hayawezi kufanyika hadi pale Serikali iliyo madarakani itakapoondolewa. Wamesema kuwa changamoto haiko kwa vijana bali kwa viongozi na vyombo vya dola ambavyo vinatajwa kuhusika na vifo vya raia.

Aidha, wengine wametafsiri ujumbe wa Bagonza kama ametoa baraka zake kwa vijana na Watanzania kwa ujumla kushiriki kwenye maandamano kwa kutumia mazishi, wakisema kwa namna hiyo kila mtu atajitokeza na vyombo vya dola havitaingilia kwakuwa wananchi watakuwa wanaenda kwenye kuzika ndugu zao.

Fortunatus Buyobe adaiwa kutekwa na ‘wasiojulikana’

Mwanachama wa JamiiForuma na Mtengeneza maudhui mtandaoni wa makala za uchunguzi, Fortunatus Buyobe anadaiwa kutekwa majira ya jioni maeneo ya Dar es Salaam na watu waliojitambulisha kuwa Polisi na kutokomea naye kusikojulikana.

Jana, Disemba 4, Buyobe kupitia ukurasa wake wa X (Twitter) alidai kuwa maisha yake yapo hatarini, akisema anawindwa na watu wenye silaha za moto ambao pia walivamia nyumbani kwake bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamesema matukio haya yanaongezeka kasi na hakuna dalili ya kuisha ikiwa Polisi wanaotakiwa kulinda wananchi ndio watuhumiwa wa kwanza. Wameongeza kuwa, njia pekee ya kuyakomesha ni endapo Serikali ya CCM itaondolewa marakani.
 
Back
Top Bottom