Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 5, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 5, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
108
Balozi 16 zaitaka Tanzania kuachia wafungwa wa kisiasa, kusitisha utekaji na kurudisha miili ya waliouawa


Balozi za nchi 16 pamoja na Ujumbe wa Umoja wa Ulaya wametoa tamko kuonyesha huzuni na wasiwasi mkubwa kufuatia vifo, majeruhi na madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ulioripotiwa kutokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 nchini Tanzania.

Katika tamko lao la pamoja lililotolewa Desemba 5, 2025, ubalozi wa Uingereza, Canada, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Denmark, Ufini, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Hispania, Uswidi pamoja na Umoja wa Ulaya, wametaka uchunguzi huru, wa wazi na shirikishi. Nchi hizo pia zimezitaka mamlaka kukabidhi miili ya waliopoteza maisha kwa familia zao haraka iwezekanavyo, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa, na kuhakikisha waliokamatwa wanapata msaada wa kisheria pamoja na matibabu.

Maoni ya Wananchi:
Wengi wamesema kauli alizotoa Rais Samia katika mkutano wake na wazee ndio umepelekea balozi hizo kuja na tamko hilo. Baada ya Samia kuhoji ‘wao ni wakina nani’ kwa kejeli, wamekuja kujitambulisha, na kwa hali inavyoonyesha hawataishia kwenye salamu tu. Wananchi wanasema ikiwa hatua za makusudi hazitachukuliwa kuboresha mahusiano ya kidiplomasia, basi nchi inaenda kwenye anguko kubwa la kiuchumi.

Wengine wamepongeza tamko hilo na kusema msukumo kutoka nje una nguvu kubwa ya kupelekea wote waliohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi wawajibishwe, kwasababu Tanzania bado inategemea misaada kutoka nje kwa kiasi kubwa, na kuikosa itamaanisha athari kubwa kiuchumi.

Polisi yapiga marufuku maandamano ya Desemba 9, 2025

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limepiga marufuku maandamano yanayodaiwa kuwa ya ‘amani yasiyo na kikomo’ yaliyopangwa kufanyika kuanzia Desemba 9, likieleza kuwa hayajakidhi matakwa ya kisheria na yanaonyesha viashiria vya mipango ya uhalifu inayoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

Katika taarifa ya Desemba 5 iliyotolewa na Msemaji wa Polisi, DCP David Misime, jeshi hilo limesema halijapokea notisi yoyote ya maandishi kama inavyotakiwa na Sheria ya Polisi Sura ya 322, huku uchunguzi wake ukibaini mpangilio wa mbinu zinazodaiwa kuhamasishwa mtandaoni ikiwemo; mwito wa kutumia silaha, kusimamisha shughuli za kawaida, kuchoma minara ya mawasiliano, kufunga barabara na mipaka, kupora mali, kuzuia huduma hospitalini na kutoa vitisho vya kiusalama. Polisi imesema viashiria hivyo vinaonesha uwezekano wa kuvunjika kwa amani na kuathiri maisha ya wananchi, uchumi na miundombinu muhimu ya nchi.

Maoni ya Wananchi:
Wengi wameonyesha hasira na kuchoshwa na matumizi makubwa ya nguvu na kauli za vitisho, wakisema Serikali imekuwa ikizuia maandamano hata pale watu wanapotaka kujieleza kwa amani. Pia, wanasema kitendo cha kuyaita maandamano “Mpango wa uhalifu” bila kutoa vielelezo vya kutosha kinadhoofisha imani ya umma na kinaonekana kama njia ya kuzima sauti za wananchi.

Wengine wamesema hawatambui tamko hilo, kwani Polisi wanatakiwa kupewa taarifa ili wajue nini kitaendelea pamoja na kutoa ulinzi kwa wananchi lakini sio kuzuia maandamano wakisema Disema 9 watajitokeza kuandamana kama ilivyopangwa.

Aidha, wengine wamelitaka Jeshi la Polisi kuanzisha chama chake cha siasa iwapo wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa mtazamo wa kisiasa na kuwapendelea tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM), badala ya kuzingatia sheria na kutoegemea upande wowote.

Sweden: Tutasitisha ushirikiano wa kimaendeleo na Tanzania, sababu hazihusiani na matukio ya hivi karibuni

Serikali ya Sweden kupitia ubalozi wake nchini, imetangaza kusitisha ushirikiano wake wa maendeleo na Tanzania ifikapo Agosti 31, 2026. Ingawa ushirikiano uliopo utaendelea hadi muda huo, Sweden imeeleza kuwa uamuzi huu unatokana na mabadiliko ya vipaumbele vya sera zake za kimataifa, changamoto mpya za kiusalama na mkakati mpya wamaendeleo wa Serikali ya Uswidi.

Aidha, Sweden imesisitiza kuwa, kusitishwa kwa ushirikiano huu hakuhusiani na uchaguzi au matukio ya hivi karibuni yaliyotokea nchini.

Maoni ya Wananchi:
Wengi wameona hatua iliyochukuliwa na Sweden huenda imetokana na matukio yaliyotokea hivi karibuni nchini pamoja na hotuba ya Rais Samia alipokuwa kwenye mkutano na wazee. Wameongeza kuwa ikiwa juhudi za makusudi na haraka hazitachukuliwa kunusuru mahusiano ya kidiplomasia, basi nchi inaenda kwenye kipindi kigumu kiuchumi ikiwa na mataifa mengine yataendelea kusitisha misaada na ushirikiano wake na Tanzania.

Aidha, wapo wanaosema usitishaji wa mikopo na ushirikiano na nchi nyingine uendelee, kwani hii inaweza kuwa namna pekee ya kurejesha utawala wa sheria, uwajibikaji na kukomesha matukio yanayokiuka haki za binadamu.

Chalamila: Tutachukua hatua za kisheria kuhusu tuhuma za Padri Kitima dhidi ya TANESCO. Suala la Polepole, Polisi wataendelea kuchunguza

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Ofisi yake kwa kushirikiana na TANESCO haitabaki kimya kufuatia kauli za Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Fr. Charles Kitima kuwa tukio la uvamizi wake lilihusisha kuzimwa kwa umeme na TANESCO, akibainisha kuwa madai hayo ni mazito na yanahitaji uchunguzi wa kina.

Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Mita Janja za Umeme Desemba 5, Chalamila amesema alimsikia Kitima akidai kuwapo kwa “Conspiracy” kati ya wavamizi na TANESCO na hivyo kuzungumza na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Lazaro Twange, ambapo walikubaliana kufanyia kazi suala hilo sababu linagusa taswira ya Shirika. Amesisitiza kuwa shirika haliwezi kuhusishwa na kuzima umeme kwa nia ya kumdhuru raia, hivyo ni muhimu kupata ufafanuzi zaidi kutoka kwa Kitima, huku akieleza kuwa tayari wanasheria wameelekezwa kuchukua hatua zinazostahili.

Chalamila pia amewataka wananchi waendelee kuiamini Serikali na kuwaacha Polisi waendelee na uchunguzi wa kutoweka kwa aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, akisema hana taarifa za kina kuhusu suala hilo kwani alichokifahamu ni kupitia taarifa za mitandaoni. Akizungumza kwenye mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema hawezi kumtembelea kila mtu mwenye matatizo kwa kuwa mkoa una changamoto nyingi, na kusisitiza kuwa hakuna utaratibu wa mabalozi kuripoti kwa mkuu wa mkoa wanaporudi nchini.

Aidha, ameeleza kuwa uchunguzi wa Polisi unahitaji muda kutokana na aina ya tukio, huku akilaani vikali matukio yanayodaiwa kuongeza chuki katika jamii kama utekaji, ukosefu wa ajira, matumizi mabaya ya rasilimali za umma, na matumizi ya nguvu kupita kiasi. Vilevile, Chalamila amesema kuwa safari za watu kwenda nje ya Dar es Salaam ni jambo la kawaida lisilopaswa kuhusishwa na mambo mengine, akionya kuwa hofu ni janga linaloweza kutumiwa na maadui wa nchi.

Maoni ya wananchi:
Kuhusu suala la Kitima, wengi wamoji mpaka wakati huu kwanini hakuna majibu ya Polisi mpaka Chalamila na TANESCO watake kuanza upya uchunguzi? Wamesema hii inadhihirisha kuwa matukio haya ya watu kushambuliwa ama kutekwa hayachukuliwi kwa uzito unaostahili kwa lengo la kutafuta haki na uwajibikaji, bali huwa ni geresha tu kuonesha wanafanya kazi kwasababu wao ndio wahusika wakuu, na hawezi kujichunguza wala kujichukulia hatua.

Aidha, kuhusu uchunguzi wa tukio la kutoweka kwa Polepole, wengi wameonyesha kutokuwa na matumaini ya kupatikana akiwa hai kutokana na historia ya matukio hayo, ambapo waliowahi kupatikana wakiwa hai baada ya kutekwa ni wachache sana. Wameendelea kuelekeza lawama kwa Serikali na Polisi kuhusika na matukio haya wakidai ndiyo sababu hakuna wanaokamatwa kuhusika nayo.

UN yatoa wito kwa Tanzania kuondoa marufuku ya Maandamano yaliyopangwa kufanyika Desemba 9

Umoja wa Mataifa (UN) umetoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuheshimu haki za msingi za wananchi kabla ya maandamano yanayotarajiwa kufanyika Siku ya Uhuru, Disemba 9. Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Seif Magango, amewataka vikosi vya usalama kupanga na kutekeleza operesheni kwa njia inayowezesha wananchi kupata uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani.

Magango amesisitiza kuwa hatua za kuzuia maandamano zinakiuka haki za binadamu na zinapaswa kuondolewa, akibainisha kuwa silaha za moto hazipaswi kutumika kudhibiti maandamano isipokuwa kama suluhu ya mwisho dhidi ya tishio la dharura la kifo au majeraha makubwa. Umoja wa Mataifa umesisitiza jukumu la makamanda wa vikosi vya usalama kuhakikisha kanuni hizi zinaheshimiwa, na kuhimiza kwamba Siku ya Uhuru ya Tanzania iadhimishwe kwa uhuru, si kwa ukandamizaji.

Aidha, kuhusu Tume ya Uchunguzi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi, Magango alibainisha kuwa Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amekumbusha mamlaka kwamba uchunguzi huo ni lazima ufuate viwango vya kimataifa vya uhuru, usawa, ukamilifu, uharaka na uwazi, na pia uhakikishe ulinzi kwa wote watakaotoa ushirikiano ili wasilipiziwe kisasi.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameona tamko hilo halina nguvu yoyote kwa Serikali ya Tanzania kutokana na jinsi imekuwa ikijibu jumuiya za kimataifa waliposhauri au kutoa ripoti zao kuhusu matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi. Wapo wanaohisi huenda safari hii yakatokea madhara makubwa zaidi kwasababu Serikali na Rais kuonesha kuwa wamedhamiria kushikilia maamuzi yao.

Tanzania yajibu matamko ya Serikali na Mashirika ya Kimataifa kuhusu matukio ya wakati na baada ya uchaguzi

Serikali imesema imepokea na kufuatilia matamko na kauli mbalimbali ziliyotolewa na baadhi ya mataifa na washirika wa maendeleo kuhusu vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Imeeleza kuwa imepokea matamko hayo kwa wasiwasi, hasa ikizingatia mazungumzo ya wazi yaliyofanyika Novemba 28 kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na wanadiplomasia, ambapo kauli zao zinaonekana kutokuzingatia kikamilifu hatua za Serikali, ikiwemo kuanzishwa kwa Tume ya Uchunguzi ya matukio ya ghasia za baada ya uchaguzi. Serikali imesisitiza kuwa matokeo ya tume hiyo yataongeza uelewa wa kilichotokea na kuwa msingi wa majadiliano chanya katika siku zijazo, huku ikitoa wito kwa wadau kuruhusu mifumo ya ndani kuendelea na utekelezaji wa hatua zilizochukuliwa.

Aidha, Serikali imeuhakikishia umma wa kimataifa na washirika wa maendeleo kuhusu utayari wake na dhamira ya kuendeleza ushirikiano kwenye masuala yote ya maslahi ya pande zote, kwa usawa na kuheshimiana.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamebeza tamko hilo wakiuliza kile kiburi ilichokionyesha mpaka kuuliza Serikali na washirika hao “Who are you?” kimepotelea wapi, wakisema kuwa hawatakiwi kuomba msamaha wala kujishusha, bali waendelee kuwa na kiburi na kuona jinsi uchumi wa nchi utakavyoporomoka.

Aidha wengine wamesema fafanuzi za Serikali zinaongeza hasira ya wananchi na pengine kuja kusababisha machafuko zaidi mbeleni kutokana na kutotambua mauji lakini pia kuendelea kuelezea Tume ya Uchunguzi kama huru na yenye kutegemewa kuleta ufumbuzi wa msuguano kati yake na wananchi, wakijua fika haiaminiki.
 
Back
Top Bottom