MTU MZIMA DAWA, SIPITALI TWAFATANI?

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,284
1466225923592.jpg


Mtu mzima ni dawa, hutibu kwa njia gani?
Nauliza mnojuwa, nipate toka shakani,
Maradhi nikizidiwa, nimebwagwa kitandani,
Atibu nipate powa, nisibaki taabani,
Sipitali twafatani, ka' mtu mzima dawa?

Ajabu atapagawa, 'sijue afanye nini,
Tena macho tayatowa, mkonowe utosini,
Ama aweza amuwa, haraka sipitalini,
Nabaki nikitibiwa, yeye kaketi kitini,
Sipitali twafatani, ka' mtu mzima dawa?

Leo nataka kujuwa, msicheke si utani,
Nisemayo sijazuwa, nimeyaona jamani,
Miaka ukizidiwa, huwazalo si thamani,
Wanafanya kubaguwa, mtu mzima awazani,
Sipitali twafatani, ka mtu mzima dawa?

Mtoto aweza kuwa, na la maana kichwani,
Vema wakalichukuwa, wasilitupe jaani,
Akafanya wasojuwa, wakongwe wa duniani,
Jamii aka'okowa, isizame nakamani,
Sipitali twafatani, ka' mtu mzima dawa?

Mkongwe mtegemewa, 'sikute ni punguani,
Mambo akayachafuwa, mithili ya hayawani,
Hataki kushauriwa, kama nyumbu za mbugani,
Au wage kamwagiwa, alivyo na kisirani,
Sipitali twafatani, ka' mtu mzima dawa?

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
call/whatspp 0622845394 Morogoro.
 
Back
Top Bottom