Habari wakuu. Nina MTOTO umri awake ni miaka 2 na miez 6. Ameacha kunyonya miez 9 iliyopita. Tangu aache kunyonya amekuwa akisumbua kula chakula. .nimempima minyoo na Kufanya Ultra Sound. . Amepewa sana Vitamin B Complex, Dawa za minyoo. Na Zingine nying za Kufanya apate hamu ya lakini Bado akisumbua na nikimchapa kumlazishe ale. Anatapika alicho kula. Nilishauriwa nialike watoto wa jiran ale nao. Wang ameishia kukiangalia . Tushaulinee nafanyeje wakuu? ??????
View attachment 2165500
KWA NINI WATOTO HUPOTEZA HAMU YA KULA?
Kukosa hamu ya kula ni tatizo la kawaida kwa watoto ambalo hupelekea wazazi wengi kuwa na wasiwasi juu ya afya ya watoto wao.Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha kukosa hamu ya kula na tatizo hili linapojitokeza tunatakiwa kuwa watulivu na kujaribu kuchunguza kwa makini ni kwa nini mtoto anakosa hamu ya kula. Baadhi ya sababu zaweza kutatuliwa na mzazi au mlezi lakini sababu nyingine kama zisababishwazo na magonjwa zitahitaji msaada wa wataalam wa afya.
Moja ya sababu kubwa ambayo huwakosesha watoto hamu ya kula ni aina mbalimbali za magonjwa. Magonjwa kama
Malaria, kuhara, maumivu ya tumbo, maumivu ya kichwa, magonjwa ya kinywa na koo, homa na mafua au dalili nyinginezo ambazo humkosesha mtoto raha hupelekea watoto kukosa hamu ya kula.
Matatizo ya kifamilia na msongo ni sababu nyingine ambayo huwakosesha watoto raha na hamu ya kula. Kama walivyo watu wazima watoto pia hukumbana na matatizo ya kifamilia kama kupoteza ndugu au vitu wavipendavyo. Lakini pia watoto hukumbana pia na changamoto mbalimbali za kimaisha kama majukumu ya shule au pengine kukumbana na unyanyasaji kama kuzomewa na mambo mengine mengi yanayokiuka haki zao. Kwa hiyo ili kumuepusha mtoto na ukosefu wa hamu ya kula, wazazi na walezi hawana budi kuwa makini endapo wataona mabadiliko yoyote ya kitabia ya mtoto. Kugundua na kuweza kuziondoa sababu zinazomsababishia mtoto msongo, tutaweza kuwarudisha katika hali ya kawaida na hamu ya kula itarejea tena.
Lakini pia wakati mwingine hali hii hutokana na ugonjwa wa kukosa hamu ya kula ujulikanao kitaalam kama Anorexia nervosa. Watoto wenye ugonjwa huu huweza kukaa muda mrefu bila kula ingawa hawana tatizo jingine, na endapo watapewa chakula huchagua aina fulani tu ya chakula jambo ambalo hupelekea kutopata mlo ulio kamili na hii hupelekea kupungua uzito pamoja na kudhoofu kwa afya zao . Jambo hili linapojitokeza ni vyema kumpeleka mtoto kwa wataalam wa afya wa masuala ya lishe ambao watakuwa msaada mkubwa katika kumsaidia mtoto wako kurejesha tena hamu ya kula.
Kiwango kidogo cha ukuaji wa mtoto huchangia kupungua kwa hamu ya kula. Katika mwaka wa kwanza wa maisha ya watoto, watoto hukua haraka lakini baada ya mwaka mmoja kiwango cha ukuaji hupungua na kiwango cha chakula wanachokula pia hupungua.Katika wakati huo, hali hiyo ni ya kawaida katika maisha ya watoto.
Sababu nyingine ambazo huchangia watoto kukosa hamu ya kula ni kama maudhi ya dawa, upungufu wa damu, uambukizi wa minyoo na matatizo ya mmeng'enyo mfano mtoto kutopata choo.
Maudhi ya dawa mbalimbali ambazo hutumika kutibu magonjwa kwa watoto yanaweza kuchangia watoto kukosa hamu ya kula. Mfano daktari akimwandikia mtoto dawa za antibiotiki, zaweza kusababisha tazizo la kukosa hamu ya kula. Kupoteza hamu ya kula kwa watoto wanaotumia antibiotiki ni maudhi ya dawa ambayo huwapata watoto wengi. Dawa nyingine pia zaweza kupelekea kupata maudhi ya dawa kama kichefuchefu na kutapika. Tatizo hili humalizika mtoto anapomaliza dawa na endapo atakuwa amepona.
Uambukizi wa minyoo huchangia tatizo hili. Minyoo huingia katika mfumo wa mmeng'enyo wa watoto na kusababisha upotevu wa damu. Minyoo hutegemea ufyonzaji wa damu kama chakula chao, na katika uambukizi sugu hupelekea kuvuja kwa damu,upungufu wa damu, kuhara,kichefuchefu,kutapika na kukosa hamu ya kula. Endapo mtoto ataonyesha dalili za umbukizi wa minyoo, ni vyema kuwaona wataalam wa afya ili kuweza kufanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu.
Ugonjwa wa upungufu wa damu ambao kwa kitaalam hujulikana kama anemia, husababishia watoto tatizo hili. Kiwango kidogo cha madini ya chuma katika damu, huwapata watoto ambao hawapati lishe ya kutosha yenye madini haya. Lakini pia anemia yaweza kusababishwa na uambukizi wa minyoo au hata magonjwa mengine. Watoto wenye anemia huwa wadhaifu na wasio wachangamfu, na kama ugonjwa usipotibiwa utaathiri afya ya mtoto hata maendeleo yake shuleni. Ni vyema mtoto akafanyiwa vipimo vya damu endapo utahisi au ataonyesha dalili za ugonjwa wa anemia.
Kwa watoto hasa wadogo, kukosa choo hupelekea kukosa hamu ya kula. Kwa hiyo inapotokea basi ni vyema kupata msaada wa wataalam ili mtoto aweze kuondokana na tatizo hilo.
Wazazi na walezi wazingatie yafuatayo ili kuboresha hamu ya kula ya watoto wao:
Kuwa na ratiba nzuri ya kumpa mtoto chakula, na mtoto apewa chakula anapokuwa na njaa.
Usiwagombeze au kutoa maonyo makali kwa watoto wakati wa kula.
Kuwa na milo midogo kati ya milo mikubwa.
Mpe mtoto kiasi kidogo cha chakula lakini mara nyingi kwa siku na siyo kumshindilia kwa wakati mmoja.
Usimlazimishe mtoto kula kama hana njaa.
Hakisha mtoto anashiriki katika michezo, kwa kuwa michezo huusisha matumizi ya nishati ya mwili na kuboresha mifumo mbalimbali ya mwili.
Wakati mwingine mpe nafasi mtoto wa uchaguzi wa chakula akipendacho, lakini chini ya uangalilizi wa mzazi au mlezi ili afanye uchaguzi ulio sahihi.
Wakati wote wazazi na walezi tukumbuke kuwa tatizo la kukosa hamu ya kula ni la kawaida kwa watoto wengi, na tatizo linapojitokeza hatuhitajiki kuwa na wasiwasi kila wakati. Kama mtoto wako ana afya njema, anapata usingizi vizuri na ni mwenye furaha, hauna sababu ya kuwa na wasiwasi. Lakini kama tatizo litaendelea kwa muda mrefu, basi hatuna budi kuonana na wataalam wa afya kwa msaada zaidi.
Watoto zaidi ya mwaka 1 zingatia mlo kamili wenye makundi yote ya chakula. Mtoto anapokula aina tofauti za vyakula hukamilisha mlo kamili. Mlo kamili utamsaidia mwanao kupata aina zote za virutubisho anavyovihitaji. Kuwa mbunifu ili kugundua aina ya chakula mtoto akipendacho.Wakati mwingine watoto wanapopewa chakula kwa mara ya kwanza huwawia vigumu kuikubali ladha ya chakula hicho, lakini baada ya muda fulani tunapoendelea kuwapa chakula hiki hujifunza na kujikuta wamezoea ladha ya chakula hicho. Kama mtoto hatopenda kula yai la kuchemsha jaribu kumpa maziwa, na kuendelea kubadili vyakula kadiri mtoto anavyopendelea. Ubunifu wa aina za chakula na ubadilishaji kulingana na chakula akipendacho, utaondoa tatizo la mtoto kukataa kula. Mfano, chakula kama nyama kitamwongezea mtoto protini, lakini anaweza pia kupata protini kutoka katika nati, maharagwe,dengu na njegere.
Ili kumsaidia mtoto aondokane na tatizo la kukataa kula, mpe aina mbali mbali za vyakula kutoka katika makundi yafuatayo.
Vyakula vya wanga
Viazi mviringo au viazi vitamu.
Nafaka kama mahindi, mchele, ngano na nyinginezo.
Majimbi na ndizi.
Nafaka zisizokobolewa huwa na kiasi kikubwa cha fiba ambazo zina aina nyingi za virutubisho.Kuwa makini na kiasi unachompa mtoto kwa kuwa nafaka hizi zisizokobolewa hushibisha sana na kumpa kwa wingi kutasababisha mtoto kuvikataa vyakula hivi. Kumbuka tumbo la mtoto ni dogo na ni kiasi kidogo kitakachomfanya ashibe.
Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya chuma na protini.
Mtoto anahitajika kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya chuma na protini mara mbili kwa siku.Vyakula hivi ni kama:
Nyama.
Samaki.
Nati.
Mayai.
Njegere,maharagwe na dengu.
Hakikisha unanunua nyama yenye ubora kutoka katika bucha zenye nyama iliyopimwa.Epuka kununua nyama kutoka wauzaji wa mitaani ili kumwepusha mtoto na magonjwa hususani ugonjwa hatari kama kimeta. Kama utapendelea kumpa mtoto vyakula aina ya nati(karanga,kweme,korosho,nazi na nyinginezo) hakikisha zimesagwa na kumchanganyia katika chakula chake ili kuepuka mtoto kukabwa.
Vyakula kutokana na maziwa.
Maziwa.
Jibini.
Mtindi (yoghurt)
Kama utapenda kumpa mtoto mtindi, chagua ule usiowekewa ladha na usio na sukari nyingi. Kama utapenda kuongeza ladha, fanya hivyo kwa kuchanganya na matunda yenye ladha azipendazo mtoto. Maziwa ni chanzo kizuri cha madini ya kalshamu (calcium). Hakikisha mtoto wako anapata kiasi cha nusu lita ya maziwa kwa siku. Madini haya ni muhimu kwa kuwa huimarisha mifupa,meno na muhimu kwa utendaji kazi wa misuli. Watoto wenye upungufu wa madini haya hupatwa na ugonjwa ujulikanao kama rickets ambao husababisha udhaifu wa mifupa ambayo hupinda na kusababisha matege. Hakikisha mtoto wako anatumia maziwa yasiyoondolewa siagi kwa kuwa watoto wanahitaji nishati nyingi ya mwili ili wakue. Pia maziwa haya yasiyoondolewa siagi huwa na kiwango kikubwa cha Vitamini A.
Matunda na mboga za majani.
Embe,chungwa ,zabibu na nanasi.
Tikiti maji.
Parachichi.
Papai.
Karoti.
Mboga za majani.
Matunda ni muhimu kwa watoto kwa kuwa huwaongezea aina mbalimbali za vitamini muhimu zinazohitajika mwilini. Jaribu kubadilisha aina za matunda kulingana na ladha aipendayo mtoto.
Vyakula vinavyohitajika kwa kiasi.
Vyakula vyenye mafuta mengi na sukari nyingi ni kama siagi, mafuta ya mimea, keki,chokleti,chipsi, biskuti, pipi na vinywaji kama soda.Miili ya watoto huitaji kiasi kikubwa cha nishati, lakini kuwapa kiasi kikubwa cha vyakula hivi kwaweza kusababisha kuwa na uzito mkubwa(obesity). Endapo utachagua kumpa vyakula hivi, hakikisha anakula kiasi kidogo na ikiwezekana ale vyakula hivi kwa vipindi mfano wakati wa sikuu ya kuzaliwa au siku za mwisho wa wiki pekee.Ni vizuri tahadhari kuchukuliwa kwa kuwa vyakula vyenye sukari nyingi huweza pia kusababisha magonjwa ya kuoza kwa meno.
Watoto hawaitaji kula vyakula vyenye chumvi nyingi. Epuka vyakula vya migahawani ambavyo huwa na chumvi nyingi.
Kama mtoto ana tatizo la pumu, aleji ya chakula au kuna historia ya aleji katika familia,epuka kumpa chakula kama karanga kabla ya kuonana na mtaalam wa lishe au daktari ili kuweza kuzuia madhara anayoweza pata mtoto.