33.
“Ni wazi kuwa yeyote aliyefanya mauaji haya bado yuko katika eneo hilihili. Kwa ajili hiyo nimeongeza ulinzi na kupanua wigo.” Chaku alisema.
Kambambaya alitikisa kichwa na kuunga mkono hatua hiyo, “Walisikia mlio wa bunduki aina gani?” alihoji.
“AK-47, mzee.”
AK! Kambambaya alishangaa. Ile bunduki hatari iliyogunduliwa na Mrusi, Kalashnikov, kwenye vita kuu ya pili ya dunia! Basi hii ni vita! Aliwaza.
Chikaya alimwongoza hadi mahala ilipokuwepo miili ya marehemu. Walilaliana wawiliwawili, baadhi wakiwa wameziangukia silaha zao, mmoja silaha yake ikiwa mkononi kama anayejiandaa kufyatua. Haikuhitaji utaalamu wowote kubaini kuwa kifo kiliwakuta marehemu hawa bila ya wao kutegemea. Ama walivamiwa ghafla, au waliingia katika mtego wa mauti.
Kuiona miili ya vijana hao wasio na hatia, wakiwa hawapo tena duniani, kuliamsha hasira katika nafsi ya Kambambaya. Nani aliyewaua? Kwa nini amewaua? Afanye nini kuwapata haraka wahalifu hawa ili wafikishwe mikononi mwa sheria? Alijiuliza harakaharaka, swali baada ya swali, maswali ambayo yeye binafsi hakutegemea majibu yake yawe karibu kiasi hicho, jambo lililozidi kumpandisha hasira.
Kiasi fulani hasira hizo ziliambatana na hofu, si hofu ya kujua kuwa mahala fulani, katika mtaa fulani, kuna mtu au watu hatari, wenye silaha hatari, ambao wanaweza kuwaua polisi wanne bila ya kigugumizi chochote. Ndiyo, hilo lilimtisha, lakini hofu nyingine ilikuwa juu yake binafsi. Hatua yake ya kuamua kumwinda Joram Kiango kwa nguvu nyingi kiasi hiki ilionyesha kuwashangaza na kutoungwa mkono na wasaidizi wake. Wanavyomjua Joram hawakuona kama ni mtu wa hatari kiasi hicho, wengine hawakuona umuhimu. Lakini maadamu yeye alikuwa na madaraka, alilotaka liwe, likawa.
Hivyo, sasa ilimtisha kwa kutojua atauambia nini umma wa Watanzania umwelewe; kwamba Joram Kiango alishukiwa kuua msichana hotelini! Kwamba kwa ajili hiyo alituma kikosi kikubwa cha askari kumtafuta! Kwamba katika purukushani hizo askari wanne wameuawa kinyama! Nani atamwelewa? Nani atamsikiliza?
Wakati akiwaza hayo Kambambaya alikuwa akiendelea na uchunguzi wa eneo hilo. Akiongozana na Chikaya, na askari wengine wawili, walipita uchochoro hadi uchochoro, wakiikagua nyumba baada ya nyumba. Ikiwa alfajiri ya siku ya kazi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walianza kuamka. Walishangazwa kuona mitaa yao ikiwa ‘imevamiwa’ na polisi wenye dalili za madaraka makubwa. Kambambaya hakutaka kuwabugudhi raia kwa wakati huo. Aliwahoji wawili watatu, maswali mawili matatu, lakini wote walionekana kama wanaoulizwa, “Wewe ni mwanamume?” wakati anajiona ni mwanamume au “Wewe ni mwanamke?” wakati kila mtu anaona kuwa ni mwanamke. Kambambaya aliachana nao na kuendelea na uchunguzi wake.
Uchochoro mmoja uliwafanya watokee kwenye hospitali ya Daktari Omari. Alishangazwa na umati wa watu walioukuta umezingira hospitali hiyo, kila mmoja akiwa anatokwa na machozi ya hofu.
“Kuna nini hapa?” alihoji.
“Daktari ameuawa,” mmoja wa majirani alimjibu. “Daktari yupi?”
“Dokta Omari, mwenye hospitali hii. Wagonjwa waliokuja kupata sindano za masaa wamemkuta akiwa amelala kifudifudi, tundu kubwa likivuja damu toka kisogoni mwake.” Kambambaya hakusikiliza zaidi. Alipenya umati huo wa watu hadi ndani. Mwili wa Daktari Omari ulikuwa bado umelala sakafuni, katikati ya mlango wa kutokea ofisini kwake kuelekea wodini. Risasi iliyomuua ilikuwa imemfumua kisogo na kupotelea katika ubongo wake ilikuwa tayari imeganda na
kufanya kichwa chake kiungane na sakafu.
Kambambaya alitupia macho mezani. Majalada, vitabu, magazeti na vikorokoro vingine vya kiganga vilikuwa katika hali ya mpangilio mzuri. Viti na meza pia vilikuwa katika
utaratibu wake maalumu, hali ambayo ilimfanya apate hisia kuwa kifo kilimkuta marehemu bila purukushani yoyote.
“Mzee unaona pale?” msaidizi wake mmoja alimzindua.