Kurzweil
JF-Expert Member
- May 25, 2011
- 6,622
- 8,410
Jeshi la Marekani limesema mfumo wake wa Thaad wa kutoa kinga dhidi ya makombora umeanza kufanya kazi nchini Korea Kusini.
Msemaji wa jeshi hilo amesema mtambo huo sasa una uwezo wa kuzuia makombora yanayorushwa na Korea Kaskazini na pia kuilinda Korea Kusini.
Lakini maafisa wameambia wanahabari kwamba itachukua miezi kadha kabla ya mfumo huo katika kutumika kikamilifu.
Hali ya wasiwasi imekuwa ikitanga katika rasi ya Korea, huku Korea Kaskazini ikiendelea kutoa vitisho mara kwa mara.
Marekani nayo imetuma kundi la meli za kivita pamoja na nyambizi katika rasi hiyo.
Jumatatu, ndege mbili za kuangusha mabomu za Marekani zilifanya mazoezi ya pamoja na jeshi la wanahewa la Korea Kusini, operesheni ambayo Marekani ilisema ilikuwa ya kawaida.
Mtambo wa Thaad, ambao kwa kirefu husimamia Terminal High Altitude Area Defence, ulianza kuwekwa wiki iliyopita katika eneo ambalo zamani lilikuwa uwanja wa gofu katika eneo la Seongju katikati mwa Korea Kusini.
Baadhi ya raia wa Korea Kusini waliandamana kuupinga.
Wengi wa wenyeji wanaamini mtambo huo unaweza kulengwa na adui na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wanaoishi hapo karibu.
China pia imepinga kuwepo kwa mtambo huo - ikisema uwezo wake wa rada huenda ukahitilafiana na operesheni zake za kijeshi.
Msemaji wa jeshi la Marekani aliyepo Korea Kusini alisema mtambo huo wa Thaad sasa "unafanya akzi na una uwezo wa kuzuia makombora yanayorushwa kutoka Korea Kaskazini na kuilinda Jamhuri ya Korea."
Lakini afisa mmoja wa ulinzi wa Marekani aliambia shirika la habari la AFP kuwa mfumo huo kwa sasa una uwezo tu wa "kuzuia makombora hatua ya awali" lakini unaimarishwa baadaye mwaka huu vifaa zaidi vya mtambo huo vitakapowasilishwa.
Korea Kaskazini na Marekani zimekuwa zikijibizana vikali wiki za hivi karibuni huku Pyongyang ikiendelea kupuuza marufuku ya Umoja wa Mataifa inayoizuia kufanya majaribio ya makombora.
Taifa hilo lenye usiri mkubwa limetekeleza majaribio mawili ya makombora, ambayo yalifeli, wiki za karibuni, na limesema kwamba liko tayari kufanya jaribio lake la sita la nyuklia wakati wowote.
THAAD ni nini?
- Ni teknolojia ya kujilinda ya kutungua makombora ya masafa mafupi na wastani ambayo huyaharibu yanapokaribia kulipuka.
- Hugonga kombora la kuliharibu
- Ina uwezo wa kufika umbali wa kilomita 200 na inaweza kurushwa juu hadi kilomita 150 angani
- Marekani imewahi kuweka mitambo kama hiyo Guam na Hawaii kujilinda dhidi ya uwezekano wa mashambulizi kutoka kwa Korea Kaskazini.
Chanzo: BBC Swahili