Mtaalaam ashindwa kumbaini aliyeghushi

buswelu moja

JF-Expert Member
Aug 24, 2014
226
180
ARUSHA,SHAHIDI wa saba katika kesi ya kughushi mukhtasari wa serikali ya mtaa wa Levolosi iliyofunguliwa na mkuu wa wilaya ya zamani,Danh Makanga dhidi ya mume mwenzake,Mathew Mollel ameieleza mahakama kwamba hajui ni nani aliandika mukhtasari unaobishaniwa.

Shahidi huyo ,Chrisanta Chitandala ambaye pia ni mchunguzi wa kisayansi wa hati na maandishi kutoka makao makuu ya jeshi la polisi hapa nchini ameileza mahakama kwamba katika uchunguzi wake haelewi ni nani aliuandaa mukhtasari huo.

Akiulizwa swali na mwendesha mashtaka wa serikali,Mary Lucas kwamba mara baada ya kufanya uchunguzi wake ni nini alibaini katika mukhtasari huo shahidi huyo alisema kwamba aligundua kwamba mukhtasari huo haukuandikwa na aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa serikali ya mtaa wa Levolosi,Haruna Fundikira na hajui nani aliuandaa.

Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya hakimu mkazi Arusha,Mwankuga Gantwa shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa pamoja na mukhtsari huo kuwa na sahihi mbili lakini yeye alichunguza sahihi moja kwa kuwa aliagizwa na ofisi ya mkuu wa upelelezi (RCO) mkoani Arusha.

Shahidi huyo ambaye alijitambulisha kuwa alisomea kazi hiyo katika nchi za Scotland na Uturuki alisema kwamba alipatiwa sahihi tisa kama sampuli za kufanyia kazi lakini alichunguza sahihi moja tu kwa mujibu wa taratibu za uchunguzi.

Akijibu swali lililoulizwa na wakili wa upande wa utetezi ,Ephraim Koisenge kwamba je alichunguza maelezo yaliyomo ndani ya mukhtasari huo shahidi huyo alisema kwamba hakuweza kuchunguza maelezo hayo mbali na sahihi peke yake .

Mara baada ya kumaliza kuwasilisha ushahidi wake mwendesha mashtaka wa serikali,Lucas alimweleza hakimu anayesikiliza shauri hilo kwamba upande wa mashtaka utamleta shahidi wa mwisho katika kesi hiyo na kesi hiyo kuhairishwa mpaka Juni 15 mwaka huu.

Hadi sasa ni jumla ya mashahidi saba upande wa mashtaka tayari wameshawasilisha ushahidi wao mbele ya mahakama hiyo ambapo juni 15 mwaka huu shahidi wa mwisho atawasilisha ushahidi wake katika kesi hiyo inayovuta hisia za watu mbalimbali mkoani Arusha.

Katika kesi hiyo nambari 430 ya mwaka 2016 Makanga ambaye aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Bariadi Mashariki alifika mbele ya kituo kikuu cha polisi cha kati na kumtuhumu mme mwenzake Mollel kughushi mukhtasari wa serikali ya mtaa wa Levolosi na kujipatia hatimiliki ya kiwanja namba 231 kitalu DD kilichopo Mianzini jijini hapa.

MWISHO

Source: MWANANCHI
 
Back
Top Bottom