PostGE2025 Msoto walichopitia Wapinzani katika Uchaguzi Mkuu 2025; Uapisho wa kimyakimya, fomu kukataliwa…

PostGE2025 Msoto walichopitia Wapinzani katika Uchaguzi Mkuu 2025; Uapisho wa kimyakimya, fomu kukataliwa…

Conversations and stories after Tanzania's 2025 General Elections

KwetuKwanza

Senior Member
Joined
Mar 13, 2023
Posts
121
Reaction score
218
Kabla ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 serikali ilitangaza kuwa imefanya marekebisho katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ili iwe huru na haki.

Moja ya maeneo ni kubadilisha jina la tume hiyo na kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambapo iliongezwa neno HURU, kuondolewa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia uchaguzi katika ngazi za majimbo.

Mabadiliko mengine ni kuondolewa kwa sheria ya mgombea wa chama kupita bila ya kupingwa na kutakiwa kupigiwa kura ya ndiyo na hapana hata kama mgombea ni mmoja katika eneo.

Serikali ilisema mabadiliko hayo yalitokana na malalamiko ya wadau mbalimbali kutaka Tume ya Uchaguzi iwe huru, lakini pia baadhi ya sheria zake kulalamikiwa.

Licha ya mabadiliko hayo baadhi ya vyama vya siasa vilisema kubadilisha jina la tume na baadhi ya sheria haiwezi kubadili chochote, kwani waliona bado kuna uhitaji mkubwa wa mabadiliko ndani ya tume.

Baadhi ya vyama vya upinzani, viliunga mkono mabadiliko hayo vikaamua kutangaza kushiriki uchaguzi Mkuu, huku vyama vingine ambavyo vilikosoa mabadiliko hayo vikigoma kuingia katika uchaguzi Mkuu.

Baada ya Uchaguzi Mkuu kufanyika na kuibuka kile kilichotokea, tumezungumza na baadhi ya wagombea vyama vya upinzani hasa ngazi ya ubunge na udiwani watueleze walichokutana nacho katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Tulitaka kujua Je, ni kweli uchaguzi ulikuwa huru na haki, wagombea wao walipewa haki sawa na wagombea wa CCM na Je? Walikutana na changamoto zipi?

Baadhi ya wagombea katika Mkoa wa Simiyu, waliozungumzia mabadiliko hayo wamesema yalifanywa yalikuwa kiini macho tu na wala siyo uhalisia.

Wagombea hao hasa nafasi za udiwani, wanasema kuwa katika mchakato mzima wa uchaguzi, kuanzia uchukuaji wa fomu, kurejesha, kampeini, kupiga kura hadi kuhesabiwa kwa kura hali ilikuwa mbaya sana kwao.

Wanasema walikutana na misukosuko mikubwa sana kutoka kwa wagombea wenzao wa chama tawala (CCM) Jeshi la Polisi, hadi wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya Wilaya hadi vituo vya kupigia kura.

Katika mkoa huo vyama vikubwa vya upinzani vilikuwa ACT-Wazalendo pamoja na CHAUMA, na vyama hivyo kwa asilimia kubwa viliweka wagombea katika majimbo na kata zote za Mkoa huo.

Licha ya kuweka wagombea ubunge na udiwani maeneo yote ya Mkoa, ni chama cha CHAUMA tu ambacho kiliambulia ushindi katika kata moja, ambapo mgombea wake kata ya Gulyati Jimbo la Bariadi Vijijini alishinda uchaguzi huo.

MGOMBEA UBUNGE WA ITILIMA – ACT WAZALENDO: FOMU HAIKUPOKELEWA

Jackson Skania huyu alikuwa mgombea Ubunge Jimbo la Itilima kupitia ACT- Wazalendo, anasema fomu zake zilikataliwa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo akielezwa kuwa alichelewa muda wa kurejesha.

Anasema “Nilifika Ofisi za Msimamizi Masidizi wa Jimbo majira ya 9:30 Alhasiri, nikamkuta Msimamizi msaidizi lakini alikataa kupokea fomu zangu akasema nimechelewa nilitakiwa kuzirejesha Asubuhi.

Skania anasema Msimamizi Msaidizi huyo alidai kuwa muda ambao umebaki nusu saa, hawezi kupitia fomu zake na kumtaka kuondoka ofisini hapo. “Msimamizi aliamua kufunga Ofisi na kuondoka wakati tukiendelea kubishana.

Skania anasema fomu zake hazikupokelewa na hakukuwa na njia nyingine ya kuweza kupeleka fomu zake kwani msimamizi huyo baada ya kufunga Ofisi aliondoka moja kwa moja na hakurejea tena.

MGOMBEA GIMBI – CHAUMMA: HAKUTEULIWA

Chama cha CHAUMMA nacho kiliweka Mgombea katika jimbo hilo Gimbi Masaba, ambaye yeye alifanikiwa kuchukua fomu na kurejesha lakini hakuteuliwa na tume kugombea.

Gimbi anasema kuwa sababu za kutoteuliwa ni kuwa fomu yake ya kiapo ilikuwa haijasainiwa, ambapo yeye anaeleza kuwa fomu hiyo ilisainiwa na yeye kama inavyotakiwa lakini ilishangaza kukuta kuna fomu yenye majina yake ambayo haijasainiwa.

“Wakati narejesha kile kiapo kilikuwa kimesainiwa kabisa, kuna mchezo ulifanyika kati ya wasimamizi na watu wa CCM, kiapo ambacho kilisainiwa kiliondolewa na kuwekwa kingine ambacho hakijasainiwa,” amesema.

Mgombea huyo anasema hata alipokata rufaa ngazi za juu kwenye INEC, rufaa yake ilikataliwa na hakuweza tena kugombea nafasi hiyo na kupelekea Jimbo hilo kuwa na mgombea mmoja wa CCM tu.

WAGOMBEA 22 WA ACT FOMU ZAO HAZIKUPOKELEWA

Katika Jimbo hilo la Itilima, ACT Wazalendo ilifanikiwa kuteua wagombea nafasi za Udiwani kwa kata zote 22 katika Jimbo hilo, hata hivyo wagombea wote fomu zao hazikupokelewa wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata.

Iko hivi Wagombea wote wa ACT- Wazalendo ngazi ya Udiwani katika Jimbo la Itilima, hakuna hata mmoja ambaye fomu zake zilipokelewa kuwania nafasi hiyo.

Baadhi ya wagombea ambao niliongea nao wanasema wasimamizi wasadizi ngazi ya kata, wote walifunga Ofisini na kuondoka hivyo fomu zao zikakosa wahusika wa kuzipokea.

ALIWAHI LAKINI MSIMAMIZI AKAMWAMBIA AMECHELEWA

Benedictor Michael ni mmoja wa wagombe nafasi ya Udiwani, anasema yeye alifanikiwa kupewa fomu lakini changamoto ilikuwa kwenye kurejesha, alibishana na msimamizi wakati anarejesha na baadaye ofisi ikafungwa.

“Nilipofika Ofisi ya kata, msimamizi aliniambia nisubirie kuna maelekezo, nikafanya hivyo, niliendelea kusubiria hadi muda wa kurejesha ukakaribia kuisha, nikata kujua maekelezo gani, lakini sikupata jibu,” amesema.

Baadaye Msimamizi alimwambia fomu zake haziwezi kupokelewa “Alinitaka tuandike kuwa amechelewa wakati mimi nilifika mapema, baada ya kukataa, mtendaji akafunga Ofisi na kuondoka bila ya sababu.”

Michael anasema wagombea wote wa ACT Wazalendo katika Jimbo hilo ngazi ya Kata, hakuna hata mmoja ambaye fomu zake zilipokelewa, baada ya vikwanzo kuwa vingi na wahusika kufunga Ofisi.

“Kata zote 22 wagombea wenzake ndani ya chama chetu, wote tulifanyiwa huu mchezo, Ofisi zilifungwa bila ya taarifa na sababu za msingi, fomu zetu zilikamilika kila kitu, lakini hazikupokelewa, wasimamizi walifunga Ofisi na kuondoka,” amesema.

Katika maeneo ambayo wagombea wa Upinzani walifanikiwa kuteuliwa na tume kisha kugombea, wanasema waliyopitia hayaelezeki kwani walisumbuliwa sana.

Wanasema kuazia kipindi cha Kampeini, kupiga kura hadi kuhesabu kura, walipitia mambo mengi mazito na magumu, ikiwemo vitisho, kukamatwa na Polisi bila ya hatia na kusumbuliwa sana.

Mmoja wa wagombea nafasi ya Udiwani katika Jimbo la Kisesa kupitia chama cha ACT- Wazalendo, anasema kuwa wakati wa kampeni alisubiriwa sana na wafuasi wa CCM pamoja na Polisi.

Anasema kuwa baada ya kuteuliwa na Tume ili kugombea, alianza kupokea ujumbe kutoka kwa wafuasi wa CCM wakimtaka aachie ngazi na asigombee lakini alikataa.

“Walionitaka nisigombee walikuwa ni wafuasi wa mgombea mwenzangu ndani ya kata kupitia CCM, lakini hilo jaribio lilishindikana kwa sababu nilijua nilikuwa naungwa mkono sana na wananchi.

Anasema kuwa baada ya jambo hilo kushindikana, wafuasi wa CCM walianza kuingilia mikutano yake ya kampeni, “Yaani nikiwa na mkutano kijiji fulani, wao wanakuja na bendera zao wanapita na kupiga kelele na kuharibu mkutano wangu.”

Anasema aliamua kukaa kimya na kuvumilia manyanyaso hayo, lakini wafuasi wake ambao walionekana wamebeba au kufunga bendera za chama chake chake kwenye vyombo vya usafiri walipigwa na wafuasi wa CCM na kuchomewa bendera zao.

Mgombea huyo anasema manyanyaso hayakufanywa tu na wafuasi wa CCM, bali yalikuwa pia wanafanywa na vyombo vya ulinzi na usalama, kwani walikamatwa wafuasi wake ambao walionekana wakiwa na bendera za chama chake na kupeleka kituo cha Polisi Meatu.

Anasema CCM na vyombo vya usalama walifanya kila vurugu katika mikutano yake, lakini alikuwa mvumilivu na kuendelea na Kampeini, hata hivyo alifanikiwa kumaliza salama na kufika siku ya kupiga kura.

Anaeleza baadhi ya mawakala wake hawakujitokeza siku ya kupiga kura, baada ya kupata vitisho, hivyo siku hiyo hiyo ilimlazimu kuwaleta mawakala wengine wapya ambao nao hawakuwa na elimu yeyote.

“Wale ambao walikuwa wana elimu na walipewa viapo mapema, walitishiwa maisha hivyo siku ya uchaguzi hawakutokea, nikaamua kuwaleta wale ambao tuliwaweka kama akiba, changamoto yao hawakuwa na uelewa wa mambo vizuri lakini tulifanikiwa kumaliza zoezi la kupiga kura,” amesema.

Anasema kuwa baada ya upigaji kura, zoezi la kuhesabu liliendelea ambapo dalili za mgombea wa CCM zilikuwa mbaya, ambapo anaeleza wakati wa kujumlisha matokeo zoezi hilo halikufanyia makao makuu ya kata kama ambavyo inatakiwa kisheria.

POLISI WALIKIMBIA NA MABOKSI YA KURA

Anasema kilichofanyika vyombo vya ulinzi vilikimbia na maboksi ya kura na kwenda nayo makao makuu ya Halmashauri “Mpaka leo sisi kwenye kata yetu hatujawahi kutangaziwa matokeo ya Mgombea Udiwani, na hatujui nani alishinda.

Anaeleza baada ya polisi kukimbia na maboksi ya kura, yeye pamoja na baadhi ya wafuasi wake walianza kutafutwa na vyombo vya ulinzi na usalama, baadhi walikamatwa lakini yeye alifanikiwa kukimbia na kujificha.

“Wafuasi wangu waliokamatwa walifikishwa Polisi na kuwekwa rokapu, siku ya tatu waliachiwa huru bila ya kuambiwa nini sababu za kukamatwa, hata mimi mwenyewe sikujua sababu za kutaka kunikamata,” amesema.

Anasema katika mchakato mzima wa uchaguzi alipitia mateso makubwa sana, ambayo mengine hawezi kuyaeleza kwani yanatia hasira, na kuongeza chuki dhidi ya mchakato wa uchaguzi nchini ambao siyo wa kidemokrasia.

MAWAKALA WA ACT HAWAKUPATIWA VIAPO

Mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Maswa Mashariki naye kupitia ACT-Wazalendo Abel Mpina naye anasema alipitia magumu kama mgombea pamoja na wafuasi wake.

Anasema hali ilikuwa mbaya zaidi kwa mawakala wake, kwani wote walishindwa kupatiwa viapo kwa wakati na kusababisha kuingia wamechelewa katika vituo vya kupigia kura.

Abel anasema kuwa mawakala wake siku ya kuapa, hawakuambiwa ni muda gani wataapishwa, jambo ambalo lilimsubua sana na kuangaika kupata hatma ya mawakala wake.

WALIWAAPISHA KWA SIRI MAWAKALA WA CCM

“Kilichofanyika walikuwa wakiwaapisha kwa siri mawakala wa CCM na sisi tulivyogundua haraka haraka tukawapeleka wa kwetu kuapishwa.

Anasema alifanikisha zoezi la kuwaapisha mawakala wake wote, ambapo hawakuruhusiwa kuondoka na viapo vyao bali vilibaki kwa wasimamizi wa uchaguzi.

“Siku ya uchaguzi mawakala wangu walichelewa kuingia katika vituo baada ya viapo vyao kuchelewa kuletwa kwenye vituo, na hili jambo lilifanywa maksudi, saa tano Asubuhi ndiyo wakaruhusiwa baada ya viapo vyao kupatikana”

Anasema kuwa licha ya changamoto hiyo, baada ya kupiga kura maeneo mengi katika jimbo hilo matokeo hayakubandikwa kwenye mbao baada ya kuhesabu, na badala yake maboksi ya kura yalikimbizwa.

Nguvu ya vyombo vya dola ilikuwa ni kubwa sana, iliwatia hofu sana wananchi wangu hasa mawakala, wengi walikuwa wanakamatwa ovyo ovyo bila ya sababu za msingi.

Mmoja wa Viongozi wa Chama cha ACT Mkoa anasema kuwa wagombea wao wengi ambao walikuwa wanaungwa mkono na wananchi walipitia wakati mgumu katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Sanane Shenya ni Katibu wa chama hicho mkoa anasema chama chake kiliamua kuingia katika mchakato wa uchaguzi mwaka 2025 ili kuona kama kweli yale mabadiliko yaliyosemwa na serikali kama yana ukweli.

“Ndugu yangu pale hakuna mabadiliko, ile kuita tume huru ya uchaguzi, kilichobadilika ni jina tu lakini matendo ni yale yale, ile ilikuwa danganya toto, hakuna mabadiliko hata kidogo, kukandamizwa kwa upinzani kuko pale pale,”

Anasema walipima na kujionea kwa macho yao, wagombea wao tanuru la moto ambalo walipitishwa lilitoa taswira kabisa kuwa hapakuwa na nia ya dhati ya kufanyika kwa uchaguzi wa Demokrasia.

“Kile ambacho kililalamikiwa na vyama ambavyo havikushiriki uchaguzi ndicho tulikutana nacho, ni wakati sasa wa vyama vyote vya upinzania nchini kuungana na kukataa huu nyanyasaji, bila ya hivyo hatuweza kushinda na kuwa na uchaguzi wa demokrasia”,

Shenya anasema kuwa wagombea wao walinyanyaswa, kuteswa, kukamatwa bila ya sababu, mambo ambayo alieleza wagombea wa CCM wao hakuna hata mmoja alifanyiwa hivyo na badala yake walishiriki uchaguzi kwa amani.

Anasema kuwa katika uchaguzi wa nchini kwetu, hakuna demokrasia, hakuna usawa wala haki na badala yake uchaguzi upo kwa chama kimoja CCM na vyama vya upinzania vinanyanyaswa, kuteswa na kunyimwa na haki yao ya msingi.
 
Bado kuna wajinga waliweza kuingia kwenye uchaguzi
 
Hao ni wanafiki uchaguzi ulikuwa huru na wazi, kama usingekuwa hivyo wangekaa pembeni kama chadema. Huwezi kuilaum CCM Kwa ujinga wenu na unafiki hamku lazimishwa kushiriki uchaguzi. Mkapewa pesa na magari Bado mna lalamika nini Sasa. CCM akili kubwa msipokuwa na msimamo mkaendekeza njaa Kila uchaguzi mtalia , CCM inataka wapinzani Sirius ukikubali kula nawe utaliwa
 
Back
Top Bottom