NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaju amewataka wafanyabiashara mkoani Kigoma kutokubali kulipa kodi kwa makadirio, iwapo wataalamu wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawajafika na kutathimini biashara zao.
Dk Kijaju ameyasema hayo mjini Kigoma katika mkutano wake na wafanyabiashara wa mkoa huo na kusema kuwa ni lazima kuwe na uhalisia katika ulipaji mapato kulingana na biashara inayofanyika.
Amesema ana habari kwamba watumishi wa TRA hasa wilaya zisizo na ofisi za mamlaka hiyo, wamekuwa wakiagiza vitabu au kufanya makadirio kulingana na yale yaliyopita kipindi kilichopita jambo linalozua malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara.
"Zipo biashara zinazokua lakini pia zipo biashara ambazo zilipata changamoto hivyo mtaji wake kupungua ni lazima watumishi wa TRA wataalamu wa masuala ya kodi wakatembelea biashara husika wakakagua vitabu kwa uhalisia wake ndipo wakadirie kodi anayopaswa kutozwa mfanyabiashara husika,"amesema DkKijaju.
Pamoja na hilo Naibu Waziri huyo wa fedha na mipango aliwataka wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki kwani ndiyo njia sahihi itakayowafanya walipe mapato kulingana na biashara wanayo fanya.
Ameitaka TRA kutoa mafunzo na semina za mara kwa mara kwa wafanyabiashara kuelezana mtiririko wa namna ya kulipa kodi ili walipe kodi kwa hiari.
Pia amesema, Serikali imeweka mazingira mazuri kwa wakulima kukopa kutoka taasisi za fedha ili kuendeleza shughuli zao za kilimo kitaalamu na kuongeza uzalishaji katika mazao ya kimakakati ambayo yameteuliwa na serikali.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara mkoa Kigoma, Raymond Ndabiyegese alisema kuwa utendaji kazi wa watumishi wa TRA mkoa Kigoma umefanya pande hizo mbili kuwa mahasimu kutokana na kufunga maduka bila kufanya mazungumzo na wafanyabiashara.