China wiki hii itaingia kwenye kipindi cha “Mikutano Miwili”, na ajenda kuu ya mwaka huu ni kujadili na kupitisha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano. Mpango huu wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo hautaamua tu mwelekeo wa China, bali pia kutoa fursa kwa nchi mbalimbali za Afrika zinazojiendeleza kisasa.
Moja ya mafundisho muhimu yanayotolewa na China katika kutafuta maendeleo ya kisasa ni kwamba: “Njia za maendeleo haziwezi kuhamishwa moja kwa moja kutoka kwa nchi nyingine.” Kwa muda mrefu, nchi za Afrika zilitegemea sana mtindo wa kiuchumi wa kimagharibi, na kukosa kutathmini hali ya kipekee ya nchi zao. Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa China unasisitiza tena kuwa maendeleo lazima yategemee hali ya kitaifa, jambo linalotoa mafunzo muhimu kwa Afrika.
Kuna sekta tano ambazo Afrika zinaweza kupata fursa kutokana nazo. Kwanza, kujenga viwanda badala ya kutegemea rasilimali pekee. Afrika ina maliasili nyingi lakini imekuwa ikitegemea usafirishaji wake tu kwa nje. Mpango wa 15 wa Miaka mitano unasisitiza uzalishaji viwandani, na Afrika inapaswa kuzingatia kukuza sekta ya viwanda pia ili kupunguza utegemezi wa maliasili pekee.
Pili, kujenga “miundombinu mipya” kuziba pengo la maendeleo. Miundombinu ya kimsingi ya Afrika inaendelea kuboreshwa lakini mtandao wa intaneti bado ni changamoto. Mpango wa 15 wa Miaka Mitano unasisitiza umuhimu wa kukuza “Miundombinu mipya” kama 5G na mtandao wa usambazaji vitu, jambo ambalo linatoa fursa kwa Afrika kuendeleza uchumi wa kidijitali kwa kushirikiana na China.
Tatu, kuinua uzalishaji wa kilimo na kuongeza kipato. Uzoefu wa China katika kupambana na umaskini ni muhimu kwa Afrika. Hatua zilizowekwa kwenye Mpango wa 15 wa Miaka Mitano kuhusu kilimo, kama vile biashara ya mtandao na mifumo ya ustawi wa kijamii vijijini, inaweza kusaidia Afrika kuboresha uzalishaji na kupunguza pengo la maendeleo kati ya vijiji na miji.
Nne, kukuza maendeleo ya kijani ili kuepuka uchafuzi wa zamani. China imejumuisha mabadiliko ya kijani na uvumbuzi wa kiteknolojia katika mpango wake wa 15 wa miaka mitano. Afrika inaweza kutumia rasilimali za jua ili kuendeleza nishati safi na kuepuka njia ya zamani ya uchafuzi wa viwanda.
Tano, kuingia katika mnyororo wa uzalishaji wa kimataifa. Ili kukabiliana na mabadiliko ya mnyororo wa uzalishaji, Afrika inapaswa kutumia faida ya nguvu kazi changa na maeneo ya biashara huria kuvutia uwekezaji wa viwanda, na kuongeza bidhaa za “Uzalishaji Barani Afrika”.
Mpango wa 15 wa Miaka Mitano unaendana na Ajenda ya 2063 ya Afrika, ambapo pande zote zinataka maendeleo ya viwanda na umoja. Kwa hiyo, kwa kufahamu ipasavyo mpango huo ndipo utakapopatikana ufunguo wa mafanikio katika ushirikiano kati ya China na Afrika katika miaka mitano ijayo.