Mkurugenzi Shirika la Under The Same Sun ataka umoja kumaliza mauaji ya albino

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,622
8,410
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Under The Same Sun (UTSS), hapa nchini, Vicky Ntetema ameomba ushiriki wa karibu kwa watanzania katika kuendeleza vita ya kupinga mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi huku akisisitiza kuibua wateja vigogo wanaosababisha mauaji hayo.

Vicky ambaye ni nguli katika tasnia ya habari amesema muda umefika wa taifa kuunganisha nguvu ya pamoja kushinda vita hiyo kwa kila upande kushiriki kikamilifu ikiwamo serikali kufanya mapitio ya sheria zake na Jeshi la Polisi kujihoji kwa nini ukatili na mauaji ya albino umeanza kuvuka mipaka ya nchi.

Vicky amesema hayo leo wakati wa sherehe za kupongezwa na ubalozi wa Marekani baada ya kupata ushindi wa tuzo ya Mwanamke Jasiri wa Kimataifa Machi mwaka huu. Marekani ilimtunuku Vicky tuzo hiyo kutokana na juhudi za kupinga mauaji ya walemavu wa ngozi na kuingia kwenye orodha ya wanawake waliopokea tuzo hizo duniani.

Akiwa Mwandishi wa habari wa BBC, Vicky alifanya uchunguzi kuhusu chanzo cha mauaji hayo ya albino huku akibainisha jinsi waganga wa kienyeji wanavyoshiriki katika mauaji hayo kwa lengo la kupata dawa za kuwauzia watu wenye Imani ya kupata utajiri au wanasiasa wanaohitaji ushindi.

Kwa mara ya mwisho kusikika ukatili huo ilikuwa ni Desemba 8, mwaka jana,mlemavu wa ngozi Ester Togolai Maganga(70), wa Lushoto, Tanga alipokatwa kidole na kundi la watu wasiojulikana.

Kwa mujibu wa takwimu za UTSS, kesi 12 zipo katika Mahakama Kuu, watu 11 walishahukumiwa kunyongwa, watu 4 walishaachiwa huru kwa kukosa ushahidi na mmoja akihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kutokana na ukatili wa kukata mguu wa mtu mwenye ulemavu wa ngozi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria,Amon Mpanju aliyehudhuria kama mgeni rasmi amewataka waandishi wa habari waongeze juhudi katika kuibua ukatili na mauaji hayo huku akiahidi serikali kuchukua hatua kwa watakaohusika.

“Serikali itahakikisha elimu inaongezeka zaidi kuhusu upotoshaji wa dhana hiyo ya mauaji ili kupata utajiri, lakini pia wakati huo bado tunahitaji ushirikiano wa kupata ushahidi wa kutosha kutoka kwenye jamii,” amesema.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom