Miaka 25 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, bado tuna upinzani wenye walakini

AUGUSTINO CHIWINGA

JF-Expert Member
Apr 23, 2017
220
689
Mwaka huu wa 2017 Tanzania imetimiza miaka 25 kamili ya mfumo wa vyama vingi. Mfumo huu ulianzishwa baada ya kupigiwa kura ya maoni nchi nzima chini ya Tume ya Jaji Francis Nyalali (Marehemu) na matokeo yalionesha kwamba wengi 80% walitaka tuendelee na mfumo wa chama kimoja huku wachache 20% wakitaka mfumo huu tulionao sasa.
Lakini kwa hekima za viongozi wa wakati huo ikaonekana ni busara wachache wakasikilizwa hivyo tukaanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Dhamira ya kuleta mfumo huu wa vyama vingi ilikua ni kukuza demokrasia na kuleta changamoto mpya ya kisiasa.
Hapo ndipo vyama vingi vikaibuka na kusajiliwa rasmi vyote vikiwania kukitoa madarakani chama tawala CCM.

Vyama hivyo hivyo mtihani wao wa kwanza katika dhamira yao ya kuiondoa CCM madarakani ukawa ni uchaguzi wa mwaka 1995.Hata hivyo vyama hivyo vikaangukia pua kwani Chama Cha Mapinduzi kiliibuka na Ushindi mnono chini ya Rais mteule wa wakati huo Benjamin Mkapa.

Na kwa kuanzia mwaka huo wa 1992 hadi leo 2017 ni takribani miaka 25, vyama hivyo vimeshindwa kutimiza dhamira yao ya kuitoa CCM madarakani.

Ni pasi na shaka upinzani uliopo Tanzania una walakini sana katika mambo mengi na haujashiba kuweza kuiondoa CCM madarakani.
Mathalani kimuundo na kisera vyama hivi vimeachwa mbali na Chama Cha Mapinduzi.

Vyama hivi vya upinzani kwa miaka yote hiyo vimeshindwa kuaminika na umma wa Watanzania kutokana na walakini kadha wa kadha ikiwemo kuonekana ni vyama vya kina fulani tu vikikosa muundo madhubuti wa umoja wa Watanzania bila ya kuwabagua . Vyama hivi vingi ni vya mfukoni.

Wapinzani wamedhibitisha kua hawawezi kuwaletea watanzania maendeleo kwani vimejikita katika ulalamishi na uchonganishi usio na maana yeyote.
Hawajajikita katika kutatua kero za watanzania hata pale walipobahatika kupata nafasi za uwakilishi kama vilr udiwani na ubunge.

Walakini mwingine ni katika Itikadi , vyama hivi vya upinzania ni vya kipebari na uliberali. Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inaitambua nchi yetu kua ni ya Kijamaa.
Ujamaa ambao unazingatia Utu,Heshima na Thamani ya binadamu katika kujenga jamii iliyo na usawa bila ya unyonyaji wala ukabaila. Sasa hapa moja kwa moja vyama hivi vinapingana na Katiba ya nchi katika msingi muhimu wa Itikadi na Sera ya Tanzania.Jambo hili ni hatari sana maana chama kilichopo madarakani CCM kimejitahidi kuishi na bado kinaendelea kuishi katika misingi ya ujamaa na ndio maana mpaka leo nchi yetu ni shwari na amani imetawala na maendeleo yanapatikana kwa usawa kwa misingi ile ile ya ujamaa.

Wakoloni waliotutawala (Wajerumani na Waingereza) kwa jumla ya miaka 70 ambao nao sera zao zilikua ni hizo hizo za ubepari walitunyonya na walituachia kilometa 31,000 tu bara bara za lami.
Lakini chini ya Itikadi ya Ujamaa ya CCM sasa hivi wametujengea zaidi ya kilometa 121,000 za lami.
Chini ya ubepari wa ukoloni upatikanaji wa maji vijijni ilikua ni asilimia 2% tu lakini kupitia Ujamaa wa CCM sasa hivi upatikanaji wa maji vijijini ni asilimia 53%.

Kuuacha ujamaa maana yake ni kukaribisha Taifa la wanyonyaji na wanyonywaji , wavuna jasho na wavuja jasho kitu ambacho kinaweza kubomoa umoja na mshikamano wa Watanzania na kuzorotesha ukuaji wa uchumi sawa kwa wananchi na hata pia kusababisha uvunjifu wa amani.

Uchu wa madaraka ni eneo jingine ambalo linafanya upinzani uingie walakini.Vyama hivi vina ombe kubwa la uongozi ,viongozi waasisi hawataki kabisa kuachia wengine kushika madaraka.
Wamenga'ngania wao tu kila uchwao.Huu ni walakini kama tunaweza kua na viongozi wa upinzani ambao ni vinga'nga'nizi wa madaraka wasiotaka kunga'tuka kwa hiari yao basi ni hivyo hivyo ndivo watakuja kuongoza milele Tanzania iwapo watanzania watafanya ukichaa wa kuwachagua.
Nchi yetu ni tajiri ina gesi na raslimali lukuki iwe iwavyo hatupaswi kuwachagua wapinzania wa aina hii watuongoze kwani wanaweza kuzigeuza baraka hizo za mali kua ni laana kwa Watanzania kama vile ilivyotokea nchini Kongo.

Upinzani wa Tanzania umekosa maudhui (Content) unajiendea endea tu bila ya kujua inakokwenda na ndio maana uliweza kumkaribisha na kumpa nafasi ya kugombea Urais mwanasiasa fisadi ambaye walitumia miaka mingi sana kumshtaki mbele ya Watanzania kua ni mwizi na fisadi hivyo hafai kuongoza taifa.

Upinzani ambao umekosa maudhui pia unakosa misimamo ya kusimamia kwa umadhubuti kile wanachokiamini katika muktadha wa misingi ya hoja zao na sera.
Asubuhi wanasema yule ni kunguru jioni wanasema yule ni njiwa.
Upinzani wa namna hii unaweza kuuza mbuga zote na madini yote kutokana na kutokua na msimamo katika yale mafungu waaminiayo na kuyasadiki.
Pamoja na hayo pia Uadilifu ndani ya vyama hivi ni wa shaka shaka.Kwani vimekua vikitumia vibaya ruzuku wanazopewa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwani pamoja na kutimiza umri wa miaka 25 vyama hivyo vimeshindwa kujenga hata ofisi za maana.
Mwanafalsa wa Kimarekani John Rankin alipata kuainisha nguzo 6 za Siasa na wanasiasa ambapo nguzo mojawapo ambayo aliiweka namba mbili ni kua wanasiasa lazima waishi kwenye uwazi (The power to live in the light)
Hapa alimaanisha kwamba vyama vya siasa na wanasiasa lazima waweke mambo yao katika hali ya uwazi ili kujenga uaminifu kwa jamii husika.Lakini kinyume chake upinzani wa Tanzania bado wanaishi gizani ,taarifa za hesabu za fedha zao kila zinapokaguliwa zinakutwa na ufisadi wa kutisha.Bado mfumo wao sio Shirikishi kwa maana kumetengenezwa ombwe kubwa kati ya viongozi wa juu na wanachama wao.
Viongozi wa juu hawataki kuwashirikisha wanachama wao hivyo kupelekea kutengeneza tabaka la waamuzi na waamuliwa.

Ukiangalia kwa upande wa Bungeni huku ndiko wapinzani wanapoonesha zaidi walakini wao.
Wameligeuza Bunge letu kua ni kichaka cha wahuni kwa kutukana matusi na hata kupigana.
Wameshindwa kabisa kujenga hoja zenye maslahi kwa watanzania au kuishauri serikali kwa busara kwenye mambo ya kimsingi badala wamegeuza Bunge kua sehemu ya kukwamisha serikali kuleta maendeleo na sio sehemu ya kusaidia serikali kuleta maendeleo.

Kwa navyojua mimi Bungeni ni mahali pa kuendeshea mijadala yebye tija na afya kwa jamii lakini wabunge wa upinzani walifikia hadi hatua ya kususia bunge la bajeti kwa kutoka nje.Sasa hapa ndipo mtu unajiuliza maswali kama walisusia bunge la bajeti wanategemea watajuaje kuhusu mipango ya serikali kwenye maeneo yao ya uwakilishi yaani kwa lugha nyepesi upinzani wa Tanzania hautaki maendeleo yafike Tanzania kwa haraka na ndio maana wanafanya kila waliwezalo kukwamisha upatikanaji wa maendeleo kwa Watanzania.
Upinzani wa namna hii sio wa kizalendo na wala hauna maana ya kuwepo kabisa.

Upinzani wa Tanzania umejikita katika mizizi ya vurugu fujo na uvunjifu wa amani.
Haujajikita katika kutatua shida na kero za watanzania bali katika kuzalisha kero hizo zaidi.
Wameishiwa kabisa hoja za maana zenye mashiko kwa Taifa wamekua ni watu wa uzushi majungu na fitna.
Watu wa kulalamika zaidi badala ya watatuzi wa mambo.

Augustino Chiwinga.
 
Back
Top Bottom