Mwanahabari Huru
JF-Expert Member
- Mar 9, 2015
- 14,243
- 34,903
Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilala ulifanyika Jana tarehe 27/04/2016 siku ya jumatano katika ukumbi wa mikutano wa Arnotoglou ulifanyika na kumalizika salama chini ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala mhe. Charles Kuyeko.
Kwa mujibu wa kanuni na sheria Mstahiki Meya ndiye Mwenyekiti wa mikutano yote ya baraza LA madiwani na pale inapotokea Meya hayupo basi Naibu Meya ndiye ataongoza mkutano.
Kwa kuweka kumbukumbu sawa na hasa kwa wale ambao hawana taarifa ni kwamba Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala ni Mhe. Omary Kumbilamoto ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Vingunguti kupitia Chama cha Wananchi-CUF.
Mstahiki Meya alifungua mkutano na baadae Katibu alisoma agenda za mkutano, agenda ambazo zilipokelewa na wajumbe kwa kauli moja na kisha kuendelea na mkutano.
Pamoja na wajumbe wa mkutano wa Baraza la madiwani kuzipokea agenda za mkutano huo kwa kauli moja huku Katibu wa mkutano huo ambaye ni mkurugenzi wa manispaa akidhani mambo yangeenda kama alivyo panga yeye na wale aliowaita wataalamu wake kwa kudhani kuwa madiwani wa UKAWA, huenda hawako makini na pengine hata nyaraka hawasomi vilivyo.
Wakati Katibu/Mkurugenzi akiwaza hivyo alijikuta katika wakati mgumu, pale Madiwani walipougomea muhtasari wa mkutano wa baraza la Madiwani lililopita.
Muhtasari huo umegomewa kutokana na umakini mkubwa wa kusoma na kuchambua nyaraka muhimu hasa kanuni za kudumu zinazoongoza baraza hilo ulioonyeshwa na madiwani wa UKAWA.
Kutokana na madiwani wa UKAWA kuwa na uelewa na ufahamu mzuri wa kanuni, sheria na taratibu na misingi ya kuendesha serikali za mitaa, walimshauri Mstahiki Meya kutosaini muhtasari wenye makosa ya makusudi, ambapo mhe. Kuyeko alikubaliana na ushauri huo na kusema hawezi kusaini nyaraka ambayo inamakosa, hasa makosa yaliyofanywa na watendaji kwa makusudi ili kutimiza lengo fulani.
Mara baada ya Mstahiki Meya, kugoma kusaini muhtasari huo, mkurugenzi wa manispaa ndugu Isaya M. Mngurumi alijaribu kumshawishi na kumsihi Meya aachane na ushauri wa madiwani kisha asaini muhtasari huo, Meya alimjibu mkurugenzi kuwa niletee kifungu cha kanuni za kudumu kinacho mpaka mamlaka yeye (Meya) kusaini nyaraka yoyote yenye makosa.
Wakati mkurugenzi akihangaika kutafuta msaada wa kifungu alichoombwa na Mstahiki Meya, Diwani wa Kata ya Majohe, mhe. Waziri aliomba kutoa taarifa kupitia kifungu cha 15 (2 na 4) cha kanuni za kudumu ambacho kinampa mamlaka Mstahiki Meya kusaini muhtasari baada ya kuthibitishwa na baraza LA madiwani kuwa hauna makosa, na Meya kuwahoji madiwani kama asaini au asisaini. Kufuatia kifungu hicho cha kanuni, mhe. Waziri alisema ni makosa kwa mkurugenzi kujaribu kumshawishi Meya kusaini muhtasari wenye makosa na inapelekea kuwa na mashaka na mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi na Mwanasheria wa Manispaa walishindwa kujinasua kutokana na kukosa msaada wa kikanuni na sheria inayoweza kujibu hoja ya mhe. waziri.
Mabishano hayo yaliibuka mara baada ya madiwani kuhoji uhalali wa taarifa za muhtasari wa mkutano wa kwanza wa baraza la Madiwani, ambapo Meya na Naibu Meya walichaguliwa. Muhtasari huo unaonyesha taarifa kuwa wajumbe halali wa mkutano huo ni 54, kura zilizopigwa ni 31 kura zilizoharibika ni 0 (sifuri) hapa ndipo mgogoro ulipoanzia.
Aidha Wajumbe walimtaka akabadirishe muhtasari uwe na maelezo ya wajumbe 23 walienda wapi wakati wa kupiga kura, ili hali wanaonekana walikuwepo kwenye kikao cha Uchaguzi?
Mhe. Shukuru Dege Diwani wa Kata ya Mnyamani alisema Mkurugenzi na wataalamu wake wakabadirishe muhtasari huo na Maneno lazima yasomeke kama ifuatavyo; Wajumbe na wapiga kura halali ni 54, waliofika ni 54 na akidi imetimia, waliopiga kura ni 31, wajumbe waliosusia Uchaguzi wa Meya na Naibu Meya ni 23, kura zilizoharibika ni 0 na baada ya hapo Meya atasaini na itakuwa kumbukumbu halali kwa mujibu wa kanuni za kudumu.
Aidha, Madiwani na mhe.Meya walimtahadharisha mkurugenzi kujaribu kujigeuza kuwa Mwenyekiti wa mkutano wa baraza huku akijua yeye ni Katibu na Mwenyekiti ni Mstahiki Meya. Tahadhari hiyo imetolewa kwa Mkurugenzi kutokana na Mwenyekiti/Meya kufunga agenda inayohusiana na kusaini muhtasari na yeye akajaribu kuanza kurudisha nyuma kwa kumshawishi Meya asaini.
Hata hivyo wakati mkutano huo ukianza mara tu baada ya Mstahiki Meya kufungua mkutano na Katibu kusoma agenda, wenyeviti wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Ilala ambao walihudhuria mkutano huo walionyesha mabango yenye ujumbe unaotaka halmashauri iwaongezee posho badala ya zile wanazopata kwa sasa ambazo ni sh. 40,000/ kwa mwezi na bado hawalipwi kwa wakati.
Mstahiki Meya alisoma mabango hayo ya wenyeviti wa serikali za mitaa ambapovaliwaambia suala hilo lilishafanyiwa kazi maana liko ndani ya bajeti ya mwaka 2016/2017 na kuanzia julai mwaka huu wanatarajia Manispaa ya Ilala itawapa wenyeviti
serikali za mitaa posho ya sh.100,000 kwa mwezi na atahakikisha wanalipwa kwa wakati. Katika kuonyesha kukubaliana na kauli ya mhe. Meya, wenyeviti hao walishusha mabango na kuwapigia makofi waheshimiwa Madiwani.
Imetolewa leo tarehe 28/04/2016,
Na Alex Massaba
Katibu wa Meya Manispaa ya Ilala.
0656 568256.