Alisema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wauguzi kutumia fursa hiyo kujipatia fedha haramu, kwa kuwalazimisha wagonjwa kuchangia gharama za ununuzi wa mafuta ya gari la wagonjwa, ndipo wapate huduma hiyo ya kupelekwa kwenye hospitali za rufani.
Alisema tabia hiyo imesababisha baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha kwa sababu ya kucheleweshewa tiba.
Matiro alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akikabidhiwa gari la kubebea wagonjwa na mbunge wa viti maalumu mkoani Shinyanga, Lucy Mayenga ambalo lilitolewa na Rais John Magufuli kwa kituo cha afya cha Kambarage. Kituo hicho kinahudumia wananchi 28,500.
“Marufuku wagonjwa kuombwa fedha za mafuta kuchangia kwenye gari hili pale wanapopewa rufani kwenda kwenye hospitali kubwa," alisema Matiro kwa sababu "halmashauri imeshatenga fedha hizo."
"Na ninaomba Mkurugenzi (wa Halmashauri) asimame athibitishe hilo mbele ya wananchi ili lisije likaleta mgogoro.”
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Magedi Magezi ambaye ni Ofisa Utumishi, alikiri kuwapo kwa Sh. milioni 17 za kununulia mafuta ya gari la wagonjwa, na kutaka yeyote atakayelazimishwa kutozwa pesa atoe taarifa.
Mayenga alimpongeza Rais Magufuli kwa msaada huo wa gari lenye thamani ya Sh. milioni 290, na kuiomba halmshauri hiyo kulitunza na kulitumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa ili lipate kuokoa afya za wananchi kwa uharaka.
Kaimu Mganga Mkuu wa halmashauri ya manispaa hiyo, Laurent Mhembe alisema kituo hicho cha afya kilikuwa kikiazima gari la wagonjwa katika hospitali ya rufani ya mkoa huo.
Alisema kupatikana kwa gari hilo kwa kiasi kikubwa kutaondoa vifo vya wagonjwa vitokanavyo na kucheleshewa matibabu ya rufani.
Chanzo: Nipashe