TAASISI ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, mkoani Arusha imegundua mbinu mbadala ya kutokomeza mdudu ajulikanaye kama ‘kanitangaze’ ambaye ni jamii ya viwavijeshi, baada ya kemikali kushindwa kufanya kazi.
Mtafiti Never Mwambela amesema mdudu huyo ni tishio hivi sasa, kwa kutoboa nyanya na viazi mviringo.
Amesema wao walitafiti dawa ya vimelea vya asili kwa ajili ya kumdhibiti mdudu huyo, ambayo ni ya kimiminika na nyingine ya unga ambayo hunyunyizwa kwenye udongo pamoja na mazao shambani zikiwemo, nyanya, viazi, mahindi na mengineyo.
Amesema dawa hiyo imepata mafanikio makubwa wa wakulima walioitumia wa maeneo ya Ilula mkoani Iringa, Ngara na Nyuki mkoani Arusha, Babati mkoani Manyara na Kilosa mkoani Morogoro.
Amesema wao kama taasisi, dawa hiyo haijaanza kuuzwa ila wanasubiri vibali kutoka kwenye taasisi husika, na kwamba utafiti huo wameufanya kwa miaka mitatu.
Amesema Kanitangaze ni jamii ya viwavi jeshi ambaye ni mharibufu kwa mazao. Wakulima wamejitahidi kutumia kemikali mbalimbali bila mafanikio, na mwisho mdudu huyo anakuwa sugu wa dawa.
Amesema mdudu huyo aliingia nchini mwaka 2014 akitoka Amerika ya Kusini.