Natumai nyote mu wazima, nami mzima kabisa hivi sasa namshukuru jalali kwa kunijaalia hii hali.
Naomba nijongee moja kwa moja kwenye mada husika, ya kuwazungumzia hawa wanyama tuwafugao au muwafugao majumbani kwa ajili ya mambo kadha wa kadha.
Jamii yetu asilimia kubwa humfuga mbwa kwa ajili ya ulinzi wa nyumba haswa nje ilimradi kusiweze kuvamiwa au kutokewa kwa uhalifu wa aina yeyote ile. Hulishwa kwa mara moja kwa siku, hii ni kwa takribani asilimia 98% kwenye jamii yetu ndiyo humuhudumia namna hiyo.
Kiumbe huyu hushinda kutwa nzima bila mlo, huku usiku akifunguliwa ndipo hushibishwa na kupatiwa maji. Ilimradi aingie lindoni. Yaani hii inamaanisha hupewa pumbazo kidogo ilimradi afanye kazi kwa utiifu mkubwa mno. Naye hakati tamaa, huishi namna hiyo hata mwisho wa uhai wake ukafika.
Ukimwita awe kachoka au hajachoka, awe ana njaa au hana, anaumwa au mzima wa afya. Basi atakuja tu hatojali hali yake, zaidi ya kuitikia wito wako wewe unayemfuga. Anayekupenda na hata kutaka kuwa karibu nawe kila muda, akiwa hapendi kufokewa zaidi ya kutaka kuoneshewa upendo muda wote. Ingawa hatujali tunaishia kumuweka nje kisa usafi. Tunamuwekea mipaka kisa ni mbwa, wa kuishi nje.
Hata ukifa kama ulikuwa unamwoneshea upendo na kuwa naye muda mwingi, na akajua ulipozikwa basi atakuja kulala makaburini au juu ya kaburi akiamini unaweza kuamka na kumjia tena kukaa naye. Huyu ni Mbwa!
======
Paka ni kiumbe mwingine anayefugwa na jamii nyingi duniani, ila huku kwetu dhumuni ni kumuweka kwa ajili ya ulinzi wa vitu vya ndani dhidi ya Panya waharibifu. Kupunguza mijusi ndani ya nyumba, maana hivyo ni sehemu ya chakula.
Huyu ni mnyama apendwae sana na wanadamu, hata wengine kufikia kulala naye chumba kimoja. Wakivutiwa na usafi wake, manyoya yanayopendeza. Hata kufikia kumpa chakula mara tatu ingawa wajibu wake mkubwa ni uwepo wa Panya tu, jambo ambalo ufanisi wake hupungua zaidi akishiba kupitiliza.
Paka pamoja na kupendwa na kumjali kila muda, unaweza kumwita kwa lengo la kucheza naye akakaa kimya. Si kwamba hajasikia, hata anakuwa amesikia huweza kuamua tu asije. Kukufuata kwake yategemea na maamuzi yake ila si kuendana na utiifu wake.
Kiumbe huyu ukimpa chakula kidogo ni tabu lazima akuibie kingine, humfungi kama mbwa. Hatumii muda mwingi kuifanya kazi yake, maana 70% ya maisha yake huyatumia kwenye kulala tu. Ila ndiyo huyu tunayemjali sana, kuliko yule mtiifu ambaye hata ukifa anaweza kulifuata jeneza lako hadi makaburini. Ukifukiwa atakaa hapo, akiwa na imani utarejea.
=======
Hebu chukulia mfano watu uliyonao maishani mwako, hakuna ambao unawapa uangalifu kama wa
Mbwa . Vipi ambao unawachukulia kama
Paka, hawapo?
Kumbuka thamani zao mapema, kuliko kuja kuzijua muda ambao umeshachelewa.
Mwonekano hausadifu yaliyomo ndani ya vifua vyao, mjali anayekujali. Mthamini anayekuthamini, usije kujuta ukija kumkosa.
Wasalaam.
Hassan O Mambosasa
Tanga, Tanzania
19/12/2018