Mbunge ataka wananchi wadhibiti ufisadi

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,242
34,903



KUNTI Yusuph Majala, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) mkoa wa Dodoma, amewataka wananchi kujenga tabia ya kuhoji ubora na uendeshwaji wa miradi ya kata na vijiji ambayo hutengewa fedha na halmashauri.

Kunti ametoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Berega, kitongoji cha Nghambi wilayani Mpwapwa, Dodoma.

Pia alijibu maswali ya wananchi juu ya matumizi na utolewaji wa fedha ambazo zinatakiwa kutolewa na halmashauri ikiwemo asilimia tano kwa ajili ya vijana na asilimia tano ya wanawake.

“Zipo fedha ambazo hutengwa na halmashauri kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini fedha hizo haziwezi kupatikana bila kuwepo kwa vikundi ambavyo vimesajiliwa pamoja na wananchi kutimiza wajibu wa kuhoji utolewaji wa fedha hizo.

“Wananchi ndiyo mnaishi kwenye kata na vijiji ambavyo miradi ya maendeleo inatekelezwa, ni lazima mpewe taarifa kwa viongozi wenu juu ya miradi hiyo na muangalie kama inaendana na thamani ya fedha pia lazima asilimia tano ya wanawake na vijana iwafikie kupitia vikundi vyenu,” amesema.

Katika hatua nyingine wananchi wamelalamikia huduma mbovu ambazo hutolewa katika zahanati ya Nghambi, licha ya wananchi hao kuwa wamejiunga na mfuko wa afya ya jamii (HCF).

Ibrahim Maswaswa, miongoni mwa wananchi waliohudhuria mkutano wa Mbunge huyo alisema wananchi wanachangia fedha nyingi katika mfuko wa bima ya afya lakini hakuna huduma yoyote ambayo inapatikana katika zahanati hiyo jambo ambalo linawafanya wananchi kukosa huduma ya uhakika.

“Zahanati yetu haina madaktari na badala yake kuna manesi wawili tu ambao utendaji wao hauwezi kukidhi kiwango cha utoaji wa huduma kwa wananchi wa kitongoji kizima,” amesema Ibrahim.

Kutokana na hali hiyo wananchi walimuomba mbunge kupeleka kilio hicho bungeni ili katika Bajeti ijayo ya serikali zahanati hiyo iweze kuongezewa watumishi pamoja na kuwepo kwa dawa za kutosha tofauti na ilivyo sasa. Mbunge alikubaliana na ombi hilo la wananchi.
 
Naona anapinga na hoja ya chama chake ngazi ya taifa ya kuukumbatia ufisadi.
 
Back
Top Bottom