Mbio za Mwenge zinavyopigilia msumari utumbuaji majipu

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
UTUMBUAJI majipu, kwa maana ya serikali kuchukua hatua dhidi ya watendaji wabovu katika sekta ya umma, wanaotumia madaraka yao kujinufaisha kwa njia za rushwa na ubadhirifu, imekuwa ni sehemu ya sura ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa vile hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha kwamba bado kuna ‘majipu’ mengi katika sekta hiyo, Watanzania tutegemee kuona majipu yakiendelea kutumbuliwa.

Kwa upande mwingine wa Shilingi, Watanzania tunategemea kuona uwajibikaji zaidi katika sekta ya umma unaimarika siku hata siku. Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zilizozinduliwa hivi karibuni mkoani Morogoro, nazo zinaendelea kuhimiza mapambano dhidi ya rushwa kutokana na kaulimbiu isemayo: “Timiza wajibu wako, kata mnyororo wa rushwa”.

Rushwa imeongelewa mara nyingi na athari zake zinajulikana na rushwa kubwa nchini mwetu ambazo Serikali ya Awamu ya Tano inapambana nazo ni pamoja na mikataba isiyofaa kwa taifa, mapato ya serikali kuingia mifukoni mwa watu, udanganyifu wa malipo ikiwemo mishahara hewa. Matendo hayo, licha ya kuinyima serikali mapato, pia yanachangia kwa kiwango kikubwa kuwanyima wananchi haki na huduma muhimu za kijamii kwa kuwa ni wachache, tena waliopewa madaraka ya kuwatumikia wananchi, ndio wananufaika.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake kwa taifa siku ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Aprili 18, aliwaomba Watanzania kuunga mkono kwa vitendo hatua zinazochukuliwa na serikali kwa vitendo, mintarafu upambanaji na vitendo vya rushwa na ufisadi nchini. Makamu wa Rais anasema hadi Aprili 18 mwaka huu, jumla ya kesi 596 za rushwa na ufisadi zilikuwa zinaendelea mahakamani na jumla ya Sh 6,543,342,793 zilikuwa tayari zimeokolewa.

“Naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha Watanzania wezangu kujiepusha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa,” anasema Makamu wa Rais. Anawasihi watumishi wa umma, sekta binafsi, wajasiriamali na kila mmoja kujiepusha na vitendo vya rushwa na pia watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni, miongozo na taratibu zilizowekwa. Samia anasema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na kwamba haina nia abadani ya kumwonea mtu bali kutenda haki.

Makamu huyo wa Rais anasema lengo la Serikali ni kurekebisha na kurejesha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji serikalini. Anasema hatua zinazoendelea kuchukuliwa za utumbuaji majipu ni utekelezaji Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani inahimiza uwajibikaji, kuondoa aina zote za ufisadi na kubwa ni kuona Watanzania wanapata maendeleo kwa haraka kwa kufaidika na matunda ya nchi yao. “Hatua hizi zinalenga kuwanufaisha Watanzania wote wafaidi matunda katika nchi yao (na siyo vinginevyo),” anasisitiza Makamu wa Rais.

Wakati Mwenge ukihimiza wananchi kuwajibika na kukataa rushwa, tayari mahakama ya wala rushwa na mafisadi iliyoahidiwa na Rais John Magufuli inatazamiwa kuanza rasmi mwezi Julai. Hoja ya kuanzishwa mahakama hii ambayo itakuwa pigo jingine kwa mafisadi inaungwa mkono na wananchi wengi, taasisi binafsi na wadau wengine wa maendeleo nchini. Mkuu wa Takukuru mkoa wa Morogoro, Emmanuel Kiyabo, anakaribisha ujio wa mahakama hiyo akiamini kwamba utasaidia kuharakisha kesi za rushwa na ufisadi.

Mkoani kwake, anasema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2016, mkoa ulidhibiti matukio ya rushwa 19 huku idara mbalimbali za serikali mkoani humo zikishauriwa namna ya kuziba mianya ya rushwa. Kiyabo anasema katika kipindi hicho, jumla ya miradi ya maendeleo 16 yenye thamani ya Sh 3,043,517,540 ilikaguliwa. Anasema baadhi ya miradi hiyo ilibainika kuwepo vitendo vya udanganyifu katika matumizi ya fedha za Serikali na uchunguzi unaendelea.

Anasema katika uchunguzi wanaoendelea nao wameweza kuokoa fedha za Serikali kiasi cha Sh 14,465,000 ambazo zilikuwa mikononi mwa baadhi ya watuhumiwa. “Fedha hizi zimeingizwa kwenye akaunti maalumu ya Serikali ya fedha zinazookolewa,” anasema Kiyabo. Anasema Takukuru mkoani humo pia ilifanikiwa kuokoa kiasi cha Sh 13,200,000 ambazo mkandarasi wa kuweka alama za barabarani katika Manispaa ya Morogoro alilipwa bila kuweka alama hizo.

Kiyabo, amezitaja barabara hizo kuwa ni Kitope, Kingo, Mlapakolo na Nguzo. “Baada ya taasisi kuanzisha uchunguzi na wahusika kufahamu kuwa wanachunguzwa, alama hizo zimewekwa kwa mujibu wa mkataba,” anasema Kiyabo. Kiyabo, anasema Takukuru mkoa imejipanga kuondoa kero kwa wananchi hasa katika maeneo yanayolalamikiwa kwa kuwachunguza watumishi wa umma na kuwafikisha mahakamani pale wanapobainika kufanya vitendo vya rushwa.

Pia anasema Takukuru itaongeza uelewa wa wananchi kuhusu rushwa na wajibu wao katika mapambano na rushwa sambamba na kubaini na kudhibiti mianya ya rushwa. Anasema Takukuru imeamua kuelekeza nguvu nyingi katika maeneo ya vijijini yanayokumbwa na migogoro na mapigano kati ya wakulima na wafugaji mara kwa mara kwa kuwa yapo pia malalamiko ya rushwa.

“Wale wanaofaidika na hali hiyo wakae chonjo maana saa ya kuwashughulikia imewadia... Nawataka viongozi wa vijiji waachane mara moja na tamaa ya kupokea fedha kutoka kwa wafugaji na kuingiza mifugo ovyo katika maeneo yao hali inayopeleka uhaba wa ardhi na kusababisha migogoro na mapigano miongoni mwa wakulima na wafugaji,” anasema Kiyabo. Anawataka wakulima pia waache tamaa ya kupenda malipo ya fidia ya mazao yao kutoka kwa wafugaji isivyo halali na wafugaji wazingatie sheria, kanuni na taratibu za kusafirisha mifugo na kuingiza katika maeneo mapya bila kuathiri maisha ya wenyeji wao.

“Nichukue fursa hii kuwakumbusha wananchi wote kuzingatia utawala wa sheria badala ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuharibu mazao na kuua mifugo, kitendo kinachosababisha hasara kubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” anasema Kiyabo. Wakati Takukuru Morogoro ikieleza mikakati yake katika kupambana na rushwa, ni vyema wananchi tujitokeze katika mbio za Mwenge utakapokuwa unapita katika maeneo yetu na kufanyia kazi ujumbe wa Mwenge: “Timiza wajibu wako, kata mnyororo wa rushwa”.
 
Back
Top Bottom