Umeme wazidi kuleta kizaazaa Mbeya
na Christopher Nyenyembe, Mbeya
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
KUKOSEKANA kwa umeme kwa siku nne mfululizo kumeufanya Mkoa wa Mbeya kuendelea kuwa gizani na kuwaongezea makali ya maisha wakazi wa mkoa huo, hususan ndani ya jiji hilo huku shughuli muhimu zikiwa zimesimama.
Hali ikiwa hivyo, mmoja wa mainjinia wa TANESCO kutoka makao makuu, inadaiwa kuwa alirushwa na umeme kutoka kwenye transfoma iliyoharibika na kupopoteza fahamu. Alikimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambako alipatiwa matibabu.
Tukio hilo la kuanguka kwa mtaalamu huyo wa umeme aliyejulikana kwa jina moja la Mkweche, limekuwa gumzo jijini humo huku wananchi wa maeneo ya Mwanjelwa kwenye kitongoji maarufu, wamekuwa wakiyazomea magari ya TANESCO yanayopita hapo, kwa madai kuwa zote hizo ni hujuma na matunda ya mkataba mbovu wa umeme wa IPTL.
Tanzania Daima imekuwa ikifuatilia kwa karibu malalamiko yanayotolewa na wananchi tangu mkoa huo kuwa giza totoro nyakati za usiku kukosekana kwa umeme kulifanya shughuli mbalimbali zisimame, huku wale wachache wanaotumia majenereta wamepandisha gharama za utoaji wa huduma zikiwamo mashine za kusaga nafaka, kuchaji simu na masaluni.
Kukatika kwa umeme huo tangu Jumapili iliyopita, kumekuwa kinyume kabisa na tangazo la TANESCO lililoelezea kuwa umeme huo utakatwa kutoka tangu saa 3.00 siku hiyo hadi saa 10.00, lakini hali imeonekana kuwa tofauti kabisa na hivyo kusababisha mkoa huo utawaliwe na miungurumo ya majenereta.
Kuhusu tukio lililomkumba juzi mtaalamu wa umeme kutoka makao makuu akiwa kwenye timu iliyoungana na mafundi wengine wa mkoani humo, kuwa alidondoka kutoka juu ya transfoma kwa madai kuwa alirushwa na umeme, lakini taarifa za ndani kutoka kwenye shirika hilo zimekuwa zikificha tukio hilo.
Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Dk Eliuter Samky, alipohojiwa jana alikiri kutokea kwa tukio hilo akidai kuwa walimpokea hospitalini hapo mfanyakazi wa TANESCO aliyeletwa, baada ya kupata maumivu makali lakini hakuweza kumtaja jina lake.
"Unajua huyu ni mgonjwa na hatuwezi kutoa siri za mgonjwa, ila ninachofahamu ni kuwa mfanyakazi wa TANESCO ameletwa hapa na sijui kama ameanguka huko kwenye transfoma au sehemu nyingine, tumemtibu alikuwa ameumia," alisema Dk Samky.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, mbali ya watendaji wengine wa TANESCO kusita kutaja jina lake uliweza kufanikiwa kulipata jna moja la Mkweche kuwa ndiye aliyeanguka katika pilikapilika za kurejesha umeme ambao bado umezua kitendawili mkoani humo.
Mbali ya tukio hilo, wakazi kadhaa wa Mwanjelwa walionekana wakiyazomea magari ya TANESCO kila yalipokuwa yakipita kuwa huo wote ni ufisadi uliosababishwa na mkataba mbovu wa umeme wa IPTL ambao umeliingizia hasara taifa na kusababisha fedha za kutengeneza muindombinu mingine kwa umeme wa dharura kutokuwepo.
Baadhi ya wananchi walisikika walipokuwa wakiyazomea magari hayo kuwa wanamtaka, Waziri wa Nishati na Madini, Wiliam Ngeleja, afike mkoani humo ili aweze kuwaeleza kwa kina tatizo hilo na kwa nini hakuna transifoma za dharura.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa, Dk Samky, alisema kuwa huduma muhimu katika hospitali hiyo zimesimama na wanachokifanya ni kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa mahututi ili kuokoa maisha yao na huduma nyingine ambazo hawatumii umeme.
Katika chumba cha X-Ray hakukuwa na huduma zozote zinazotolewa na hivyo kuwafanya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kuikosa, na kwamba huduma inayoweza kutolewa hapo ni ile ya ultra-sound, huku mawodini wauguzi wamekuwa wakitumia mishumaa kuendelea na huduma mbalimbali.
Mazingira hayo yote yamesababisha pia bei za vyakula zipande kama mchele, baada ya watu kukosa umeme wa kusagia nafaka na kujikuta wakinunua mchele kwenye masoko kupanda bei.