Kurzweil
JF-Expert Member
- May 25, 2011
- 6,622
- 8,410
KOCHA wa timu ya Simba, Jackson Mayanja, amewafunda wachezaji wa Tanzania na kuwataka kujituma wanapokuwa uwanjani ili wapate soko la kimataifa na kufikia hatua kama ya Mbwana Samatta, anayechezea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
Kocha huyo raia wa Uganda alisema hayo mara baada ya kushuhudia mchezo wao uliopita dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ambapo wachezaji wa timu pinzani walikuwa wakitumia muda mwingi kulinda lango lao na kushindwa kupambana ili kupata mabao.
Akizungumza jana mara baada ya kumalizika kwa mazoezi yaliyokuwa yanafanyika katika Uwanja wa TCC Chang’ombe jijini hapa, Mayanja alisema ni vema mchezaji akaonyesha kiwango chake vizuri pindi anapopata nafasi ya kucheza ili aweze kujitangaza zaidi.
“Wachezaji wanatakiwa kubadilika na kuangalia zaidi mbele ili wafanikiwe kama wenzao ambao wanacheza soka la nje, mfano mzuri ni Samatta ambaye kwa sasa anaendelea kuipaisha Tanzania Ulaya, hivyo wanatakiwa kufahamu wanapocheza watu wengi wanawaangalia huo ndio mwanzo wa kuvitangaza vipaji vyao,” alisema.
Akizungumzia mchezo unaowakabili dhidi ya Coastal Union unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi hii Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kocha huyo alisema wanataka kuvunja mwiko kwa kuamini kuwa timu kubwa lazima zifungwe na timu hiyo wanapokutana katika uwanja wao.
Alisema mpira wa sasa hauna desturi ya kufungwa ugenini, isipokuwa kila mtu anakuwa na mipango yake itakayomfanikisha kupata ushindi, kitu ambacho wao wamejiwekea ili kupata pointi tatu muhimu ili waendelee kupeta kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Tunatarajia kuondoka Alhamisi au Ijumaa kuelekea Tanga, ila kwa sasa kikosi kipo vizuri tunaendelea na mazoezi kwa ajili ya kupambana katika mchezo huo na majeruhi wanaendelea kuimarika,” alisema.
Chanzo: Mtanzania