Jindal Singh
JF-Expert Member
- Sep 9, 2015
- 1,857
- 1,538
Jitihada zinafanywa kukanusha kuwa Israel ni nchi ya kibaguzi kama ilivyokuwa Afrika Kusini wakati wa utawala wa Makaburu.
Mara nyingi Hasbara hupambana na wachambuzi wanaoikosoa Israel kwa kuwashambulia vikali. Mara nyingi mashambulizi haya huchukua sura ya kibinafsi. Kuikosoa Israel huonekana kama chuki dhidi ya Wayahudi, bila ya kujali ukweli kuwa kuna Wayahudi wengi duniani ambao hawakubaliani na sera na siasa za Kizayuni.
Kazi moja inayofanywa na kitengo hiki ni “kuwashughulikia” waandishi wa kimataifa wanaoandika ukweli kuhusu Israel. Mfano bora ni Chris McGreal, mwandishi mwandamizi wa gazeti la Kingreza: The Guardian.
Yeye alikuwa akiandika kutoka Jerusalem na katika makala yake moja aliifananisha Israel na Afrika Kusini ya Makaburu ambako aliwahi kuishi.
Hasbara wakamshukia McGreal na hata kumfungulia ukurasa wake katika mtandao, wakimshambulia na kumpaka matope. Waandishi wengine walioshambuliwa na Hasbara ni Donald MacIntyre wa gazeti la Independent, Tim McGirk wa Time, Molly Moore wa Washington Post, Jim Muir na Kylie Morris wa BBC na Greg Myre na Neil MacFarquhar wa New York Times.
Katika mashambulizi ya Israel hivi karubuni Hasbara ilikuwa na kazi kubwa kuieleza dunia kuwa eti walikuwa wakiwaua wanawake na watoto wa Gaza ili kuilinda Israel. Yaani washambuliaji wanakuwa washambuliwa na washambuliwa wanageuzwa washambuliaji. Mamilioni ya watu walioandamana duniani kote dhidi ya Israel ni ushahidi kuwa hoja hiyo ya Hasbara ilikataliwa.
Hoja nyingine inayotumiwa na Hasbara ni kudai kuwa Wayahudi wana haki ya kuivamia na kuikalia Palestina kwa sababu eti miaka elfu kadha iliyopita walikuwa wakiishi huko. Ni dhahiri kuwa hoja hiyo pia haina mashiko na ndiyo maana wengi wanaipuuza.
Kwa mfano, S V Naadarajah hivi karibuni alijibu katika gazeti la The Guardian (Uingereza) akiwauliza Waisraeli:
“Mnadai kuwa eti mmerudia ardhi mliyokuwa mmeikalia miaka zaidi ya 2000 iliyopita, kuwa eti ardhi yote magharibi mwa Mto Jordan ni miliki ya makabila 12 ya Israel. Sasa mimi ni raia mzaliwa wa Uingereza, wazee wangu ni Wahindu (asili ya Kihindi) kutoka Sri Lanka.
Kwa hiyo mimi nikaishi wapi? Ni dhahiri kuwa siwezi kudai haki ya nchi kutokana na ukaazi wa mababu zangu miaka 2000 iliyopita. Ni kichekesho pia nikisema haki hiyo nimepewa na Mungu. Wamarekani Weusi hawawezi kudai haki ya kuhamia Bara la Afrika kwa sababu tu mababu (na mabibi) zao walitoka huko”.
Hivi karibuni Israel ilishambulia Palestina kwa mabomu na kuua watu zaidi ya 2,000 katika Ukanda wa Gaza. Kati yao ni watoto 540. Zaidi ya watu 10,200 walijeruhiwa. Kati ya waliojeruhiwa, kuna wanaokufa kila siku kutokana na kukosa matibabu. Pia kila siku maiti wanaendelea kufukuliwa katika majengo yaliyopigwa mabomu.
Dunia nzima ilikuja juu na mamilioni ya wananchi waliandamana kote. Hasira zilipanda juu na maneno ya Obama na magazeti ya Magharibi yalishindwa kuwashawishi watu kuwa Israel ilikuwa inashambulia Palestina ili kulinda usalama wa Israel. Angalia CNN au BBC au Fox na utaona mtawala wa Israel akidai “Israel ina haki ya kujilinda” au “Wapalestina wanataka kutumaliza”.
Mawazo hayo yanapewa muda zaidi na uzito bila ya kuwapa watazamaji haki ya kusikiliza mawazo ya upande wa Palestina. Hilo pia liliwakasirisha wengi.
Ndipo Hasbara ikaingia mitamboni na kuanza kazi ya kusambaza propaganda. Nchini Israel wizara ya “ulinzi” ikaanzisha kikosikazi ili kueneza propaganda katika mtandao wa kijamii (facebook).
Ukurasa mmoja wa facebook ulikuwa ukiwahimiza Wapalestina waendelee kupigania uhuru wa nchi yao inayokaliwa na Wazayuni. Watu zaidi ya 120,000 walikuwa wanaipenda facebook hiyo na idadi hiyo ilikuwa ikiongezeka kila kukicha. Hasbara ilifanya juu chini mpaka wakaiondoa kwenye mtandao.
Wanafunzi kama 400 wa vyuo vikuu wameajiriwa kwa kazi hiyo iliyokuwa ikifanyika katika ukumbi mkubwa wenye kompyuta kibao. Kila mmoja alikuwa na kazi ya kueneza propaganda. Kazi ilikuwa ikifanywa katika mtandao bila ya kueleza inatoka wapi. Wewe unafikiri umejibiwa na mtu binafsi anayejitegemea kumbe ni chumba cha Hasbara.
Mfano mmoja ni picha iliyoonyesha miji ya magharibi kama Berlin ikipigwa na maroketi ya Hamas. Halafu swali linaulizwa kwa lugha mbalimbali: “Je, wangekuwa wanashambulia mji wako ungefanya nini?”
Katika Hasbara kuna miiko na miongozo waliowekewa wafanyakazi. Ni kuhusu maneno ya kutumia wanapojibu mashambulizi.Wanatakiwakutorudia maneno yanayotumiwa na “maadui” wa Israel. Badala yake wanatakiwa wabadili maneno ili kupindisha maana inayokusudiwa.
Kwa mfano, waandishi wa Hasbara wanatakiwa wasikanushe kuwa Israel ni nchi ya kibaguzi (kikaburu). Badala yake wanatakiwa waonyeshe jinsi Israel ilivyo ni nchi ya “kidemokrasi” ambapo Wayahudi na Waarabu (si Wapalestina) eti wanaishi kwa amani kama ndugu.
Badala pia ya kutumia neno “ardhi ya Palestina iliyovamiwa na Israel” wanatakiwa waseme ardhi inayogombaniwa au yenye utata. Badala ya makazi ya walowezi haramu wanatakiwa waseme majirani au maeneo ya jirani.
Badala ya kusema ukuta unaowagawa Waisraeli na Wapalestina (apartheid wall) wanatakiwa waseme mpaka au uzio wa usalama (security fence). Badala ya kusema mgogoro wa Israel na Palestina waseme ugomvi wa Israel na Waarabu. Lengo ni kufifisha wazo la taifa la Palestina.
Wanapotaja Hamas wanatakiwa waongeze “magaidi wanaoungwa mkono na Iran”
Ukiangalia katika tovuti ya Hasbara utaona jitihada ikifanywa kuwasajili wanafunzi kutoka zaidi ya vyuo vikuu 80 nchini Marekani. Mamia ya wanafunzi wamekuwa wakisafirishwa hadi Israel kupewa mafunzo. Kisha hurudi vyuoni ambako wanaendesha propaganda wakiwa wanaharakati wa Israel.
Wanaoomba ajira ya Hasibara wanatakiwa wajibu maswali kuhusu maisha yao, baba zao, mama zao na babu na bibi zao, iwapo walizaliwa Wayahudi au walibatizwa kutoka dini nyingine, na wameisaidiaje Israel maishani mwao.
Tayari wamewafunza vijana zaidi ya 3,000 katika vyuo zaidi ya 250. Wanaporudi kutoka Israel huendelea kupewa misaada ili kuwawezesha kuandika makala, kuwasiliana na waandishi, waalimu, maprofesa, wanafunzi, wanasiasa, vyama vya siasa na kuhudhuria mikutano katika kampasi zao.
Hivi karibuni tuliona jinsi Hasbara inavyoingilia maandamano ya kuunga mkono Palestina yaliyokuwa yakifanyika kote Marekani. Mara nyingi hujaribu kuvuruga maandamano kama hayo kwa kupiga mayowe au hata kutumia vitisho.
Kwa mfano, Profesa Noam Chomsky ni msomi, mwandishi wa vitabu na mwanaharakati mashuhuri wa Kimarekani anayealikwa kuzungumza katika vyuo mbalimbali. Zamani alikuwa akilindwa na polisi kila anapofika chuoni ili kutoa mhadhara. Lakini siku hizi Hasbara wameshindwa kumzuia kwa vile watu wengi wameanza kugundua mbinu za Hasbara na uharamia wa Israel huko Palestina
Upinzani dhidi ya Uzayuni sasa umejitokeza hata ndani ya Israel. Ndiyo maana siku chache zilizopita maelfu ya Waisrael waliandamana mjini Tel Aviv, wakipinga siasa na sera za Netanyahu huko Gaza, na kumtaka ajiuzulu. Hawa walitoka makundi mbalimbali kama “Meretz” na “Peace Now”.
Hata serikali ya Marekani imeanza kuwakosoa watawala wa Israel, licha ya misaada ya dola bilioni tatu wanayowapa kila mwaka. Wakati Israel ilikuwa ikiporomosha mabomu huko Gaza, Rais Obama alijaribu kumzuia Netanyahu wa Israel. Akampigia simu na kumtaka asitishe mashambulizi yake.
Netanyahu akatoa sharti kuwa Marekani impatie silaha za mashambulizi. Obama akasita ndipo makao makuu ya jeshi la Marekani (Pentagon) iliendelea kuipa Israel silaha bila ya kuidhinishwa na Obama wala waziri wake wa Mambo ya Nje, John Kerry.
Wachambuzi wanasema hivi karibuni Netanyahu alimtaka Obama aishambulie Iran na Syria, kitu ambacho Obama hakufanya. Pia Obama na waziri wake Kerry walielewa kuwa ili kuwadhibiti Wapalestina ni vizuri kuendelea na mazungumzo yaliyokuwa yameanza tangu 1993 bila kuzaa matunda.
Netanyahu akashawishiwa kuingia katika mazungumzo kinyume na chama chake cha Kadima na mawaziri wake. Kama ilivyotarajiwa, mazungumzo yalivunjika na Obama na Kerry walimtupia lawama Netanyahu.
Yote haya yalimkasirisha Netanyahu na ndipo alipoanza kuwasiliana na washikaji wake katika jeshi la Marekani na Pentagon. Hali ilizidi kuharibika Netanyahu alipoamua kuishambulia Gaza, kwa mara ya tatu katika miaka sita.
Katika macho ya Wapalestina, Obama akaonekana kuwa ameshindwa kumdhibiti Netanyahu na kufanikisha mazungumzo licha ya ahadi alizotoa. Obama akawa na kazi nzito ya kuilinda Israel na kuwalaumu Wapalestina kuwa eti ndio wenye makosa.
Dunia nzima ilielewa kuwa Obama alikuwa akiongopa kwa sababu nchini Marekani hakuna rais anayeweza kubaki madarakani bila ya kuiunga mkono na kuisaidia Israel kwa hali na mali.
Hiyo ni nguvu ya Uzayuni nchini Marekani. Mwandishi wa Kingereza, Alan Hart, alimuandikia barua ya wazi Obama akimshauri ajiuzulu iwapo anataka akumbukwe katika historia, kuliko kuendelea kurudia uwongo ulio dhahiri.
Tarehe 20 Julai mwaka huu wizara ya vita ya Israel iliomba Pentagon iwapatie mizinga aina ya 120-mm na 40-mm. Baada ya siku tatu ombi likakubaliwa bila ya kutangazwa. Hakuna idhini iliyotolewa na Obama wala Kerry.
Katika uwanja wa diplomasia mambo yalikuwa tofauti. Tarehe 25 Julai ofisi ya Kerry ilimtumia Netanyahu barua ya siri ikimshauri asitishe mashambulizi. Netanyahu alitakiwa aijibu lakini alichofanya ni kuiwasilisha mbele ya baraza la mawaziri wake ili ipigiwe kura.
Baada ya muda barua hiyo ikavujishwa na kutangazwa magazetini, jambo ambalo lilimkasirisha Obama. Kwa upande wa pili, Netanyahu hakufurahishwa na hatua ya Kerry kuwasiliana na Qatar na Uturuki ili kuishinikiza Hamas ikubali kusitisha mapigano, wakati Israel ilikuwa inawasiliana na Misri.
Wakati hii vuta nikuvute ilipokuwa ikiendelea baina ya Israel na Marekani, ikatangazwa tarehe 30 Julai kuwa kombora la Israel liliibomoa shule ya Umoja wa Mataifa ambamo Wapalestina kama 3,000 walikuwa wameomba hifadhi.
Siku hiyohiyo ikatangazwa nchini Marekani kuwa nchi hiyo iliipa Israel makombora iliyokuwa imeomba. Hii ikapandisha hasira za serikali ya Marekani. Wakaona jina la Marekani linachafuliwa, na labda huenda kesi ikifikishwa katika mahakama ya kimataifa basi hata aliyetoa silaha anaweza akahukumiwa. Tayari tume ya Umoja wa Mataifa iko mbioni kukusanya ushahidi.
Marekani pia haiwezi tena kujifanya kuwa ni msuluhishi wakati akisaidia upande mmoja wa Israel kwa silaha za dola bilioni tatu kila mwaka. Wapalestina wameanza kugundua kuwa kumbe walikuwa wakidanganywa walipoambiwa wakae meza moja na Israel ili kuzungumzia amani na usuluhishi wa madai yao.