Niliitua kalamu, sio juzi wala jana,
Kiwako wataalamu, nasi tungali vijana,
Leo nimeshikwa hamu, kisa ni hii korona.
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge
Andanenga na ngogomo, na tabora joka kuu,
mlichotupa kisomo, hamkuwa na makuu,
Mlilumba na michomo, udugu uso makuu,
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge
Nguvumunda na wengine, wengi walotangulia,
Na ya kheri tulingane, pepo kuwafungulia,
Tusidhanie wengine, nani atatangulia?
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge
Janga limeshatufika, letu sio lake yule,
Kuyadhania mashaka, kwamba yamekoma kule,
Na kujitia wahaka, si yetu ya misukule!
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge
Na zake kubwa dalili, ni kwenye koo kuwashwa,
Ingine yake dalili, pafu hewa kukaushwa,
Na wala usende mbali, kohozi kavu wahishwa,
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge
Joto kali ukihisi, usifanye mazoweya,
Kupumua kama ngisi, na maumivu kupeya,
Kichomi kama yabisi, na mwili kukulegeya,
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge
Haina dawa korona, ila inazuilika,
Haitaki konakona, huku na kule pilika,
Tulia kaya na wana, sijitie hekaheka,
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge.
Ewe mola wanusuru, nasi pia ikhwani,
Imesomba misururu, pande zote duniani,
Nani wa kutunusuru, kama si yeye Manani?
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge.
Hapa naweka tamati, kalamu nabwaga chini,
Nimekumbusha umati, nawe umefanya nini?
Ni ya watu sio miti, sijitie majangani,
Si mchezo si dhihaka, tujikinge tuwakinge