Marais EAC waimba ‘Hapa Kazi Tu’

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
MARAIS wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wameanza kuzungumza lugha moja wakisisitizana kuchapa kazi, kuondokana migogoro ya ndani na porojo za kisiasa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

Msimamo wa viongozi hao ulijidhihirisha jana kupitia hotuba zao kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara yenye kilometa 234.3 kutoka Arusha-Holili hadi kuingia Voi, Kenya itakayogharimu dola za Marekani milioni 353. Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na marais Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na James Wani Igga aliyemwakilisha Rais wa Sudan Kusini, Salva Kirk.

Wakiongozwa na mwenyeji wao, Rais John Magufuli, anayeongozwa na falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’ katika kuongoza Tanzania, marais Uhuru na Museveni walidhihirisha utayari wao wa kuunga mkono falsafa hiyo, kuhakikisha wanazifikisha nchi wanachama kwenye neema.

Katika hotuba yake, Magufuli aliwataka marais wenzake kujikita katika kushirikiana na kuacha tofauti za ndani kwa kuwa wananchi wanasubiri maendeleo kwa kasi ya hali ya juu. Akihimiza nchi wanachama kumaliza tofauti za ndani mwao, Magufuli alisema nchi za EAC ni tajiri ingawa kwa sasa ni masikini wa kutupwa na ombaomba.

Alisema hazipaswi kuwa ombaomba, bali kinachotakiwa ni kujipanga kikamilifu na kusonga mbele na kuacha tofauti ya kiitikadi ndani ya vyama vya siasa uchaguzi ulishapita. Alisisitiza kwamba wananchi wa EAC wana shida nyingi. “Hatutakiwi kuwa masikini kiasi hiki. Ni lazima tufike mahali tujiulize ni nani aliyeturoga, kama yupo mchawi lazima tumtafute tumkemee...,” alisema.

Malizeni matatizo ndani

Magufuli alisema kila nchi ina matatizo yake ya ndani, ambayo yanapaswa kutatuliwa kuhakikisha rasilimali zake zinatumika kuleta maendeleo. Alitoa mfano wa Sudan Kusini yenye madini aina zaidi ya 22, eneo la kilimo na ng’ombe wengi, kwamba wanakabiliwa a mgogoro wa kugombania madaraka ambao hawana budi kuumaliza na kusonga mbele.

“Hata Tanzania tunayo matatizo yetu, hata Rwanda wana matatizo yao… Kwa sisi tuliopewa dhamana, tushiriki kikamilifu kuondoa matatizo ya nchi zetu,” alisisitiza. Aliendelea, ‘’Sasa umefika wakati sisi viongozi (marais) kumaliza matatizo ya ndani ya nchi na nchi kusonga mbele kwani ni viongozi wa wananchi wa itikadi zote,dini zote na makabila yote bila ya kubagua’’.

Rais Magufuli alisema yeye akiwa Mwenyekiti wa EAC, wameamua kwa pamoja kujenga viwanda katika nchi hizo kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi zao, kwani kwa sasa asilimia 63 ya vijana hawana ajira.

Alisema marais wa EAC wameamua kujenga viwanda kwa lengo la kutoa ajira kwa vijana hao, ambao wako vijiweni na hiyo itasaidia mazao ya kilimo na biashara yanayolimwa katika nchi hizo, kupata soko na kuuzwa ndani ya ukanda na hata nje kwa faida ya wananchi.

Rais alieleza kusikitishwa kuona zao la biashara kama vile pamba, inalimwa nchini lakini inasafirishwa kwenda nje na kutengenezwa nguo na baadaye zinarudishwa nchini kama mitumba baada ya kuvaliwa. Alisema Tanzania sasa haiwezi tena kuwa shamba la bibi kwa wachache kujinufaisha zaidi na masikini kuwa masikini zaidi.

Utumbuaji majipu bado

Rais alisema uamuzi anaofanya wa kuwachukulia hatua watu wanaotumia vibaya madaraka na wala rushwa, si wa kuwaonea, bali vipo vitu vya hovyo ambavyo vimefanyika na kuumiza mamilioni ya Watanzania. Alisisitiza kwamba, wote waliofanya hivyo watachukuliwa hatua na kufikishwa mahakamani, hatimaye wafungwe.

‘’Nisipochukua hatua kwa mambo yalivyofanyika, haina haja ya mie kuwa Rais. Kuna mambo ya hovyo hovyo jamani yamefanyika. Nitawafukuza tu. Hilo halina msamaha,’’ alisema. Magufuli aliomba wananchi wa EAC wawe watulivu, akisisitiza kwamba marais wameamua na ndiyo maana miongoni mwa maazimio yao ni kufanya nchi ziwe na viwanda.

Alisema viongozi wakiungwa mkono na wakaombewa kwa Mungu, wataweza kutekeleza waliyodhamiria. “Mkituombea tutekeleze tunayoweza kufanya tutaweza, msipotusaidia hatutaweza… na ndiyo maana kwa Watanzania wenzangu tumekuwa na hatua ndogo ndogo tunazofanya kushughulikia watu walioneemeka na mambo ya hovyo.

Alisema kwa upande wa Tanzania, kazi ya kutumbua majipu inaendelea na hata idadi ikifika 2,000 haoni tatizo, ilimradi Watanzania walio wengi wanufaike. “Watuache tufanye kazi kwa ajili ya Watanzania walio wanyonge. Tanzania ilikuwa shamba la bibi, watu walikuwa wakifanya ya hovyo. Nimekuwa waziri kwa miaka 20 ninayajua,” alisema.

Alisisitiza kwamba mambo ya mateso kwa wananchi hayana chama. Alisema hatua wanazotaka kuchukua ni kwa ajili ya maslahi ya wananchi wote bila kujali itikadi zao. Huku akikiri kwamba kazi hiyo ni ngumu na ya ajabu, aliendelea kuomba waombewe lengo la kusaidia wananchi litimie.

“Tusipofanya, hakuna sababu ya mimi kuwa rais, ni vyema niende nyumbani nikalale, hakuna sababu ya mimi kuitiwa rais..kwa hiyo nawaomba ndugu zangu Watanzania mniunge mkono tufanye haya tunayofanya….mambo ya hovyo.” Aliendelea kusema, “ juzi tumeshindwa kuingia mambo ya roaming kwenye EAC kwa sababu sisi hatujasafisha nyumba yetu.

Kwenye TCRA ilibidi nifukuze baadhi ya wafanyakazi ; Pale zaidi ya Shilingi bilioni 400 zimepotea, tungeweza kununua ndege na kutengeneza barabara. Lakini watu wamechezea pale na bado wanajiita wasomi.

Na ndiyo maana tumeamua kufukuza, na tutawafukuza na bado watapelekwa mahakamani. Wafungwe wapate machungu ya wananchi waliyotengeneza miaka mingi,” alisema akisisitiza kuwa ni lazima ifike mahali waache kuvumiliana na kuoneana aibu.

Aonya uvyama

Magufuli ambaye alitumia nafasi hiyo, kuwashukuru wakazi wa Arusha kwa kumchagua kuwa Rais, aliwahakikishia kuwa yeye ni Rais wa Watanzania wote akisisitiza kutowabagua kwa misingi ya vyama na itikadi nyingine.

“Nataka niwahakikishie mimi ni kazi tu,” alisema. Alimpongeza Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akisema hana makeke, anajali maisha ya watu. “Nisipompongeza nitakuwa mnafiki.

Ni kijana safi, hana makeke, anajali maisha ya watu…uchaguzi umeisha, tufanye kazi tuhakikishe wananchi wanapata maendeleo,” alisema na kutania akisema, “Ukimuona Nassari sura yake ni Chadema lakini moyo wake ni CCM.”

Aliwaambia marais wenzake kwamba, wananchi wote walio kwenye nchi za jumuiya wanachohitaji si vyama, bali wanataka maisha mazuri. Alisema mambo ya kuomba omba misaada hayana budi kuisha.

Vile vile alisema mambo ya watu wachache kuwa matajiri na wengine wakabaki masikini , pia yaishe. Alisema marais wa nchi wanachama wanapaswa kujikita kubadilisha maisha ya wananchi wote wa Afrika Mashariki.

Uhuru afagilia ‘Kazi Tu’

Kwa upande wake, Rais wa Kenya, Uhuru alisema, “Tupunguze maneno na sasa iwe kazi tu wananchi wafurahie nchi zao. Tutengeneze kila kitu hapa hapa EAC na siyo kununua kutoka nje ya nchi hii ni aibu.”

“Tunapaswa kuanza rasmi safari ya kwenda Kanani (matumaini) na safari hii ndefu sana, lakini ina manufaa kwa wananchi wa nchi za EAC kwani safari hiyo ikikamilika na kufika kunakohitajika, vijana wengi watapata ajira,” alisema.

Aidha, alisema anatambua historia ya Rais Magufuli akiwa Waziri jinsi alivyowezesha ujenzi wa barabara nchini. Alimwomba aendelee na ujenzi wa barabara ziungane na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akihimiza uchapa kazi, Uhuru alisema serikali za nchi za EAC zimelala na siyo wananchi kwani wanashirikiana kwa kila hali ikiwemo kufanya biashara kwa pamoja bila ya kubaguana. Rais Uhuru alisema wananchi wa EAC wanafanya biashara kila mara na kila kona lakini viongozi wa nchi hizo wako katika usingizi mzito kwa kuweka vikwazo vya hapa na pale.

Alisisitiza marais kuondoa vikwazo hususan mipaka na vizingiti , badala yake waruhusu wananchi wafanye biashara ya wazi bila ya kificho kwa maslahi ya nchi hizo za ukanda. Alisema viwanda vingi vya nguo vimekufa katika nchi za jumuiya bila sababu za msingi.

“Na sasa tunaamua kuvaa mitumba. Hilo lazima libadilike,” alisema. Aliendelea kusisitiza, “mmejaliwa kuwa na gesi na gesi iwanufaishe kwa asilimia kubwa na pia gesi hiyo ije nchini kwangu kwa kuuzwa kwa bei nafuu.”

Museveni ‘akubali’ Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema Afrika imelala, inashtuka kutaka maendeleo wakati kumekucha, jambo alilosema kwa sasa halitakiwi kwa watu wa EAC, kwani wanapaswa kuamka na kufanya kazi ya kuinua uchumi bila ya woga.

Rais Museveni alisema serikali ya Tanzania imejitahidi kujenga barabara zake za ndani, tofauti na zamani hivyo nguvu hiyo inapaswa kuunganishwa katika nchi za jumuiya. Alisema zamani alikuwa akitumia gari aina ya Land Rover ya kizamani kusafiri katika baadhi ya mikoa lakini kote huko kulikuwa hakuna lami bali kulikuwa na vumbi.

Alisema lakini sasa anaweza kuja nchini na usafiri huo hadi jijini Dar es Salaam kwa kuwa kila kona kuna lami. Aliomba viongozi wenzake kushirikiana kwa dhati kujenga barabara katika nchi za EAC akisisitiza kuwa hizo ni sehemu ya shughuli za kimaendeleo na kiuchumi zitakazowezesha nchi kusonga mbele bila vikwazo.

Barabara iliyozinduliwa Mradi huo wa ujenzi wa barabara unagharimiwa na Shirika la Jica la Japan, Benki ya Afrika (ADB) pamoja na fedha za Serikali ya Tanzania. Rais Magufuli alisema, kwa mara ya kwanza Arusha itakuwa na barabara yenye njia nne.

Licha ya marais Museveni, Kenyatta wakiwa na mwenyeji wao Rais Magufuli, viongozi wengine waliohudhuriwa sherehe hizo za kuweka jiwe la msingi, ni pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na viongozi wa EAC akiwemo Katibu Mkuu wa Jumuiya aliyemaliza muda wake, Dk Richard Sezibera.
 
Rais Uhuru
alisema wananchi wa EAC wanafanya
biashara kila mara na kila kona lakini
viongozi wa nchi hizo wako katika
usingizi mzito kwa kuweka vikwazo vya
hapa na pale.
 
Back
Top Bottom