Mapinduzi ndio sasa

Jokajeusi

JF-Expert Member
Joined
Jun 1, 2018
Posts
6,332
Reaction score
10,913
MAPINDUZI NDIO SASA

Na, Robert Heriel
Nami nikiwa katika fikara kuu, nikifikiri yaujazao ulimwengu na kuzunguka humo. Ndipo sauti kutoka katika giza ikasema:
Je ni nani awezaye kuelewa mambo haya, Nikajibu; Mimi hapa.
Kisha ikauliza tena kwa sauti kama ya mvumo wa moto;
Je ni nani atakayeeleza habari hii kwa hao waliokata tamaa, nikajibu, Mimi hapa mtumwa wa fikara zangu Bwana.

#Niite taikon Wa Fasihi Mwanafalsafa akimbizaye akili zake.
Wakati uliotazamiwa umefika, wakati uliongojewa na kutabiriwa na kupotoshwa na lile kundi la nyoka na ng'e waumao. Hao ndio waliojitenga na kukusanya maarifa ya kila namna kutoka pande zote za ulimwengu.
Wakikaa wao kwa wao, makundi kwa makundi, kambi kwa kambi na kuupotosha Ukweli kwa hadaa zao. Wakitumia hila na njama kuificha nuru gizani wasijue nuru ilitwaliwa huko huko. Je Mungu si yule aliyegizani hata hapana macho yawezayo kumuona. Walakini wameikataa ile kweli na kutaka mambo yao wenyewe.

Mimi niliye mdogo, mtu wa zama zangu. Nimemdhulumu nini mtu mweupe hata aninyang'anye haki yangu. Rangi yangu ya gizani wameigeuza ni rangi ya waabudu mashetani. Wamenitukana mimi na mke wangu. Wamewachukua watoto wangu mateka. Jamaa yangu inalia kwa tabu ya njaa. Je lipi kosa langu nauliza. Je ukarimu wangu ndio umegeuka kwao ujinga, au subira yangu imegeuzwa uoga. Nami nimekuwa kitu cha aibu na dharau kwao.
Hata jina langu wameligeuza na kuniita kwa majina yao ya kipuuzi. Wamenidhihaki na kunitukana kila nipitapo. Wamenifananisha na sokwe wa msituni. Masikini Mimi.

Mke wangu hataki chakula changu, nikimletea pishi la mihogo hupaza sauti mlangoni hata majirani wakasikia. Hunitusi hata niletapo viazi vitamu na ndizi kutoka uchagani. Hunipa maneno makali nimpapo mahindi ya makande kutoka Upareni kwao mama yangu. Hunifitinisha na watoto wangu hata chuki yao i dhahiri katika sura zao.
Watoto wangu nisikieni, Mimi ndiya Baba yenu. Niliyempa mama yenu heshima ya kuwaleta ninyi hapa duniani. Nisikilizeni wanangu kutoka katika mifupa yangu. Chakula niwapacho ndicho asili yenu. Kitawajenga afya yenu, nanyi mtakuwa na nguvu na akili ya kupambana na adui zenu. Mle mboga mboga na matunda hapo ndipo mtaimarika mioyoni mwenu. Mahindi, mtama na ngano itawajazeni ari katika misuli yenu. Msisahau karanga, alizeti, ufuta na korosho zitawapatieni joto kipindi cha baridi.

lakini Mama yenu amepata maarifa yaletayo dhiki, mtu mweupe kutoka mbali amemchumbia na kumlaghai na zawadi nzuri na tamu kwa nje, Zilizorembwa kwa urembo na mapambo ya kila namna lakini ndani yake yapo maradhi, ulemavu, aibu na mauti. Msile chakula isipokuwa kile kilicholetwa na Baba yenu, naam ndiye mimi Taikon.
Nami nikajigeuza kidogo ili nijinyooshe kidogo. Kumbe Watoto walinichenga na kunikimbia wakiwa na mama yao.
"Mke wangu rudi nyumbani, Mumeo nakuita
kwa nini kukimbia njiani, huko kuna vita
Embu acha chako kisirani, mwisho takujajuta
Rudi upesi nyumbani Mumeo nakuita"

Hata hivyo alikimbia na kuishia upeoni. Simanzi iliirarua nafsi yangu na kunichana chana kama sulupwete la kichaa.
Basi ndio hivyo mke kakimbia katika riadha ya wendawazimu.
Mimi si yule niliyeumbwa gizan mbona sasa giza limegeuka fumbo kwangu. Si mimi niliyeletwa kwa vikao vya siri mbona yasirini yananipa tabu. Hii nayo yataka hekima kufikiri.

Mimi ni yule kijana apendwaye na mabinti wenye akili. Warembo wenye rangi nzuri za kuvutia.Sura nzuri zilizotukuka mithili ya malaika. Waupendao uafrika wao. Hao ndio mama zangu, hao ndio wake zangu nitakao waoa, hao ndio bibi zangu, shangazi zangu na dada zangu.
Nikaenda kwao mke wangu, huko kuitwapo ukweni. Nilimkuta mke wangu na wakwe zangu nikawasalimu kwa salamu. Nilisema kilichonipeleka ni kumchukua mke wangu na wanangu. Ewaa penye wakubwa hapa haribiki jambo. Tulijadili kimila na desturi ikaonekana nia yangu si nzuri. Mke wangu wangu alikataakata kata kurudi zaidi alisema anachoweza kunisaidia ni kunipa watoto tuu. Ila yeye abadani hataki,
Nilirudi nikiwa na wanangu kiasi nikiwa na furaha.

Kutokana na vyakula walivyokuwa wanapewa na Mama yao kutoka kwa yule mtu mweupe. Wanangu walianza kuugua.
Enyi wanangu, niliowazaa kwa nguvu ya mapenzi ya dhati kwa mama yenu. Kunyweni dawa hizi; ndizo miti shamba kama vile mizizi, majani, magombe na mbegu zake. kwani hizi ndizo zitakazowapeni nafuu kwa afya zenu. lakini wanangu walishupaza shingo zao. kutwa walilia wakimtaka mama yao aje.
Mama yao alikutwa katika kumbi ya burudani yenye muziki wa yule mtesi wangu, mtu kutoka nchi za baridi kali. Alikutwa akiwa nusu ya uchi akicheza mdumange wa kisasa. Pia nasikia alikutwa akibambiwa na vijana weupe wakimpapasa pasa mwilini mwake huku wakimnyeshwa kileo kikali.
Nasikia alikuwa akinitukana sana na mara kwa mara alitema mate chini kisha akiinua chupa yake ya mvinyo na kubwia fumba kubwa zaidi.
Maneno yaliouchoma moyo wangu yalikuwa; Mme wangu anamambo ya kizamani, ni mtu wa mila na desturi.
Naumia sana mimi mtu mweusi.

Ewe mke wangu, si mimi niliyekukuta bikira na kufanya agano na wewe siku ile. Kwa jasho la wazee wangu kutoka bara letu pendwa nikakutolea mahari na zawadi kedekede. Na harusi kubwa tulifunga siku ile. Ngoma za asili za kisambaa na kimakonde zilipigwa nawe kwa madaha ulicheza huku umbo lako lenye ukaribu na namba nane ukilichezesha kwa madoido na vingorimbo. Hukumbuki.
Tena sauti tamu ya zeze na santuri ilipigwa iliyoamsha midadi ya wageni waalikwa na kufanya siku ile kufaa sana. Je zile shanga walizovaa wale mabinti wacheza ngoma na vyungu kichwani havikukufurahisha.

Isitoshe hata kile chakula chako cha mtori uliopikwa kwa ustadi mkubwa siku ile mbona ulionekana kuridhika.
Basi mke wangu alikuja na madawa mengi mfango wa changarawe, pia alikuja na sindano, akiwa na watu kadhaa.
Aliwapa watoto zile dawa na kuwachoma ile sindano. La haula watoto waliinuka na nafuu iliwapungia mkono. Sura zao zikawarejea nao wakaonekana ni watu.

Wanangu hizo mlizopewa ni geresha tuu. Nisikilizeni mimi ndiye baba yenu. kwa sasa inaonekana ni dawa lakini mbeleni ni sumu yenye kuua, tena yenye kuondoa nguvu za uzazi, tena zenye kuondoa akili na maarifa .
Mke wangu hakujali na masikioni aliweka kifaa fulani cha watu weupe ambacho kiliimba nyimbo za lugha za watu kutoka nchi za mbali.
Kioja kilizuka baada ya mke wangu kuwaogesha watoto. Alikuja na viguo vifupi vyenye kuziba tupu tuu za watoto wakati sehemu kubwa ya miili yao ikipigwa na upepo. Loooh!
Mke wangu, wewe umevaa kiguo hicho kinachoonyesha utupu wako unataka na watoto nao waonekane. Mke wangu alijibu kwa kifupi; Ndio usasa huu, Acha ushamba.

Siku moja nilienda kwa huyo mtu mweupe ambaye pale alimiliki Hekalu. Niliingia kuona ni nini anafundisha mke wangu, watoto wangu, jamaa zangu na watu wenye ngozi kama mimi. Nilisikia akisema kuwa wao ndio wenye Mungu wa kweli, eti wao ndio wamebarikiwa na sisi watu weusi tulilaaniwa.
Tena eti, mababu zao ndio watu mashuhuri na ndio mmoja wao aliukomboa huu ulimwengu.
Nilishangazwa na mambo yale sana. kama hiyo haikunitosha, nilishangaa kuona kapu kubwa likiwa tupu likipelekwa mbele baadaye yule mtu aliomba kwa huyo mungu wake. Kisha alisema maneno mengi akiwataka watu hasa weusi watoe hata kile kidogo walichonacho kwani mungu wake angewaongezea maradufu.
machozi yalinitoka, huzuni na simanzi viliweka kambi moyoni mwangu. Niliona watu wangu wanavyotaabika kutafuta pesa, wanavyohenyeka kulima vibarua, kuvua samaki, kufuga mifugo na kazi za kila namna lakini leo wanatoa fedha kwa dini ya mtu mweupe. Hivi si wangeipeleka hata kwa watoto yatima, au si wangeipeleka kwenye kujenga hospitali na watu watibiwe bure, zijengwe shule na miundombinu mingine ya kijamii na kiuchumi. Lakini mke wangu na watoto wamepewa mungu mweupe, mwenye shida na hata vitu vidogo walivyo navyo.

Nilipitiwa na usingizi lakini niliota ndoto mbaya sana. Katika ndoto nilimuona yule mtu ,weupe kutoka nchi za barafu akifundisha watoto wangu shuleni, watoto wa jamaa na rafiki zangu. Walichofundishwa hakikuendana na asili na mazingira yao. Tena walifundishwa kumheshimu mgeni kuliko mwenyeji, zaidi ya hayo walifundishwa kumuogopa mtu mweupe. Jambo hili lilifanya watoto wawe duni na watumwa wa watu weupe.

Mapinduzi ndio sasa, yakupindua mila za mtu mweupe na kurejesha utamaduni wetu.
Mapinduzi ya kufuta dini zote zenye maudhui isiyompa thamani muafrika. kama dini zao hazitupi thamani nasi hatuna haja ya kuzipa thamani.
Mapinduzi ya kufuta elimu yoyote katika vitabu vyetu vinavyompa nafasi mtu mweupe kuwa ndiye mtawala.
Mapinduzi katika vyombo vya habari yatakayo tangaza utamaduni wetu na mila zetu.
Hatuwezi jivunia kitu kinachovua nguo na kudhalilisha utamaduni wetu.
Hatuwezi kujiona duni tungali tuna nguvu kama jamii yenye nguvu ya Mungu aliyegizani.
Mungu wetu amekuja Waafrika tuamke, tumtukuze yeye pekee.
Mapinduzi ndio sasa.

Niite TAIKON WA FASIHI UPEPO MWEUSI UVUMAO
https://web.facebook.com/photo.php?...21615440164.1073741830.100003869970435&type=3
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…