SeriaJr TW
JF-Expert Member
- Oct 21, 2012
- 246
- 224
Katiba ndiyo inatoa haki na uhuru wa wananchi kujumuika bila kuvunja sheria. Ibara ya 18 ya Katiba Sehemu ya (1) inasema bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
Sehemu ya (2) inasema kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.
Mbali ya Ibara hiyo ya 18 ya Katiba, sura ya 258 ya Sheria ya Vyama vya Siasa sehemu ya IV inatoa haki kwa chama chochote cha siasa kuandaa mkutano au maandamano. Ibara ya 11 (1) inasema chama chochote chenye usajili wa muda au wa kudumu; (a) kinaruhusiwa kuandaa mikutano yake eneo lolote katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kujitangaza au kutafuta wanachama baada ya kuwapa taarifa polisi wa eneo husika; (b) kinastahili kupewa kinga na msaada wa ulinzi ili kiweze kufanya mkutano wake kwa amani.
Ili shughuli hizo za kisiasa ziweze kufanyika kwa amani, vyama vya siasa vinapaswa kulijulisha Jeshi la Polisi ili uwepo ulinzi kwa usalama wao.
Sheria ya Jeshi la Polisi kifungu cha 43 sehemu ya (1) inasema yeyote anayetaka kuandaa mkutano au mkusanyiko au kufanya maandamano atapaswa kuwajulisha polisi katika muda usiopungua saa 48 kabla ya siku ya mkutano, muda na mahali kujulisha kwamba siku ya mkutano au maandamano imekaribia.
Japokuwa Katiba iko wazi na sheria ya vyama vya siasa pamoja na ya Jeshi la Polisi zote zinatoa uhuru kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na wa muda kufanya mikutano yao wakati wowote, mahali popote ili kunadi sera na kupata wanachama, Jeshi la Polisi limekuwa likivunja na kusambaratisha mikutano ya vyama vya upinzani pekee lakini linalinda ya chama tawala.
Kila polisi walipozuia mikutano ya upinzani walitoa sababu nyingine hazina mashiko. Mfano, walipozuia mahalafi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi wa Chadema mjini Dodoma walidai kuna ugonjwa usiojulikana na walipozuia mkutano wa Chadema mjini Kahama walidai ni kuzuia vurugu baada ya CCM kusema itafanya mikutano ya kufuta nyayo za Chadema.
Sasa vijana wa Chadema wanajihamasisha kwenda Dodoma kuvuruga mkutano wa CCM, je, polisi watazuia kama walivyofanya CCM waliposema wataandaa mikutano ya kufuta nyayo za Chadema?
Sisi tunadhani, jeuri hii ya vijana wa Chadema inatokana na polisi wenyewe kujichanganya kutokana na sababu walizokuwa wanatoa walipokuwa wanafuta mikutano ya Chadema.
Tunaamini kuwa polisi wanaweza kuepusha vurugu hizi za vyama kama wangekuwa wanatoa sababu za msingi, lakini kufuta mkutano wa chama fulani kutokana na kauli ya chama kingine haikuwa muafaka.
Chanzo: Mwananchi