Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,800
- 34,189
Rais John Magufuli
Kwa ufupi
Kauli inayohimiza mshikamano katika kulijenga Taifa hili lililosheheni rasilimali nyingi, lakini linaongoza kwa umaskini kwa kila mmoja kutumia taaluma, karama na fursa aliyonayo kuhakikisha Tanzania yenye neema inaoneka kwa wananchi kupana nafuu ya maisha si ulaghali.
Hotuba nyingi za Rais John Magufuli hukosi kusikia neno, “ndugu zangu nchi hii ni yetu sote tunatakiwa kushirikiana bila kubaguana kwa itikadi za kisiasa, dini na ukabila, naomba tushirikiane tuijenge Tanzania yetu”.
Kauli inayohimiza mshikamano katika kulijenga Taifa hili lililosheheni rasilimali nyingi, lakini linaongoza kwa umaskini kwa kila mmoja kutumia taaluma, karama na fursa aliyonayo kuhakikisha Tanzania yenye neema inaoneka kwa wananchi kupana nafuu ya maisha si ulaghali.
Hata wakati wa kampeni za kuwania urais aliweka mbele utanzania zaidi kuliko chama, msisitizo wake ulikuwa Serikali ya Magufuli itakuwa tofauti na watangulizi wake na makada wa chama chake, ambao kwao chama kwanza mtu baadaye. Haya ni mabadiliko makubwa yanayotoa heshima kwa utaifa kwanza.
Mtazamo wake wa umoja unahitaji mchango wa mawazo, uwajibikaji, kushauri, kukosoa kwa maana ya kujenga misingi imara ya taasisi ya rais iweze kusimama vyema katika kutekeleza majukumu ya kitaifa na kimataifa, kwa masilahi mapana ya nchi yetu na huo ndiyo uzalendo.
Kumezuka kundi la watu wanaojiona wana haki zaidi ya Watanzania wengine, kwa kupenda kuwapinga wanaokosoa au kutoa ushauri kwa Rais kuhusiana na masuala yanayojitokeza nchini. Watu hao hujipambanua kama makada wa CCM.
Tena kwa kauli kali wakati mwingine zinazokosa uzalendo. Vikundi hivi hivi vilikuwa vikijitokeza kuwashambulia watu waliokuwa wakikosoa utendaji wa uongozi wa awamu ya nne, kwa kushindwa kusimamia raslimali za umma na kuacha makundi ya watu wachache kutamalaki katika nchi kwa ufisadi, wizi na kila aina ya hujuma.
Ni hawa hawa waliokuwa wakisema awamu ya nne imefanya mambo makubwa katika nchi, imeboresha uchumi, imekusanya kodi na kuwabeza waliokuwa wakiikosoa, kushauri wakijiona wao wana haki katika Taifa hili, sasa wamehamia awamu ya tano kwa mtindo ule ule wa kujitokeza mbele kama vile urais ni wa kikundi na siyo taasisi.
Yale yale waliyokuwa wakiyatetea leo ni majipu na yanapotumbuliwa na Rais John Magufuli, bila aibu wanajitokeza kushangilia huku wakionyesha wazi kuwa awamu ya nne ilijaa uozo, ilikuwa na wapiga dili, mafisadi na wala rushwa.
Rais Magufuli anahitaji kusaidiwa na Watanzania, namna bora ya kutekeleza majukumu yake kama walivyomwamini kwa ahadi alizotoa, panapotokea jambo ambalo kwao wanaona halikukaa sawasawa wanayo haki kutoa maoni na ushauri, lengo ni kujenga nchi iliyo na umoja.
Ikumbukwe kuwa Rais ni wa Watanzania wote waliomchagua na ambao hawakumchagua, lakini mwenyekiti wa chama anahusu wanachama. Kama akisemwa na wanachama wa vyama vingine wanahaki kutoka na kutetea chama chao, lakini kwa nafasi ya urais bora atoke mtu kama yeye siyo vikundi vya kichama, tujenge utaifa zaidi kuliko uchama kwanza .
Utamaduni wa kukosolewa na kushauri unajenga misingi imara ya uwajibikaji, kwa kuwa unamkumbusha aliye na nafasi kuwa kuna watu wanafuatilia kila analotenda kila siku, wanaotaka Watanzania wasiseme wanatakiwa kutizamwa kwa umakini maana wanalenga kuzamisha meli kama ilivyokuwa awamu ya nne, ili wasimame na kuusema uongozi wa awamu tano kama wafanyavyo sasa wanawabeza waliowashabikia.
Mfano, suala la bei ya sukari Serikali imeweka bei elekezi ya Sh1,800 kwa kilo, bei ya sokoni kwa sasa inakwenda hadi 2,500, sasa wanaotaka kufunga mdomo Watanzania wasiseme kwa madai kuwa mwacheni Rais afanye kazi, ukali huu wa bei hauwagusi? Kama wanaguswa wanadhani kujigeuza mtetezi kunapunguzaje makali ya maisha?
Rais Magufuli anapaswa kuwa makini na watu wanaomjaza sifa tu, ni hatari, hata katika Biblia Takatifu Yesu alipoingia Yerusalemu watoto wa Mayahudi walimshangilia wakiwa na matawi ya mizeituni wakitandaza nguo zao apite mwanapunda wakisema mbarikiwa ajaye.
Baada ya siku tatu, hao hao walisimama na kusema asulubiwe aachwe Baraba ambaye alikuwa mkosefu na hata mwanafunzi wake Petro aliyekuwa mstari wa mbele aliapa kuwa yuko tayari kufa, lakini hatamsaliti na ni huyo huyo aliyemkana mara tatu.
Hivyo, kukubali kikundi cha watu kukusifia asubuhi hadi jioni, lazima ajiulize kama kweli hawa siyo wasaliti.
Uongozi mzuri ni unaosikiliza pande zote za wanaompinga, kushauri, kukosoa na kusifia na hapo ndipo unajua namna nzuri ya kuendesha shughuli, maana inasaidia kujua kwa sababu gani hawa wanasema hivi, je, ikifanyika hivyo faida na hasara zake ni zipi?
Chanzo: Mwananchi