Habari zenu wakuu!!
Niende moja kwa moja kwenye mada ambayo inatokana na jambo linaloonekana ni hulka au tabia za kina mama wa kambo ambao siku zote wamekuwa mshale wa mateso kwa watoto walioachwa na mwanamke mwingine.
Matukio mengi ya kikatili yamekuwa yakiwahusisha mama wa kambo kuwanyanyasa watoto wa mume hasa watoto wa kike, mfano kuna kisa cha mama wa kambo huko mkoa wa Tabora kumpiga na kumpaka pilipili mtoto sehemu zake za siri, yaani ni ujinga, upumbavu au ushetani kiasi gani mama wa kambo unaendekeza, unakosa hata robo ya uchungu kwa mtoto wa mwanamke mwenzio? Unawapenda wanao je huoni Kama ni damu moja na huyo unayemnyanyasa? Maisha ni safari ndefu huenda Mungu amekukutanisha makusudi na huyu mtoto unayemtesa ili baadaye aje akusaidie. Huko mkoani Mara mama mmoja alionekana kumtesa sana mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 7, mtoto alikuwa anapewa majukumu utafikiri yeye ndo kaolewa, mtoto anateswa hadi alikuwa anapewa adhabu kama kuunguzwa sehemu za siri na zingine nyingi za kikatili.
Miaka ya nyuma kama miaka ya 1970 hivi kulikuwa na kijana aliyekuwa akiteswa sana na mama wa kambo kuchapwa, kulishwa kinyesi, kunyweshwa mkojo na muda mwingine kuunguzwa ilikuwa sehemu yake ya maisha lakini Mungu alimpa uwezo na akili ya upambanaji yule kijana leo hii ni mtu ana kazi yake na ana maisha mazuri amekuwa msaada mkubwa kwa yule mama aliyekuwa akimtesa anamchukulia kama mama mzazi na muda mwingine anapompa zawadi asiporidhika analalamika kwamba iweje anampa kidogo amesahau visa alivyokuwa anavifanya awali.
Mama wa kambo, kuna watoto siku ya akina mama hawaoni hata thamani ya kuwatakia kheri kina mama kwa sababu wewe ni chanzo akikumbuka uliyoyafanya anawafananisha kina mama wengine kwamba wana tabia Kama zako, kuna watoto wengine hawana mama, mama zao walishakufa lakini bado wanathamini uwepo wako kama mama yao wanatamani uwalee Kama wanao ili wafarijike wajisikie amani na furaha moyoni wasahau machungu ya kupotelewa na mama zao wazazi unapowatesa unawasogeza karibu na kaburi la mama yao na kutamani kufa kabla ya siku zao.
Mama wa kambo, unamnyima chakula mtoto wa mumeo mtu hanyimwi chakula mpe ale ashibe akuombee kheri kwa Mungu, watoto wana nafasi kubwa sana ya baraka na neema kutoka kwa Mungu unapowatesa unajizibia baraka zako. Kuna mama fulani aliwapenda sana wanae kiasi kwamba alitaka wafanikiwe kwa kila kitu kama ni kwenye elimu basi alijitahidi sana kumshawishi mume wake kulipa ada na kufanya kila liwezekanalo ili wafanikiwe ilihali nyuma kuna watoto walioachwa na mwanamke mwingine ambao hakuona thamani yao Wala hakutaka wafanikiwe mwisho wa siku wale waliokuwa hawathaminiwi wamefanikiwa na wale waliokuwa wakipewa kila kitu wanaulaumu mtaa wamegeuka maadui kwa ndugu zao wakidai wao walisababisha wasifanikiwe.
Mwanaume mwenzangu kuwa makini sana na matendo ya mama wa kambo kwa watoto wako usiwe mfuata maagizo akisema mchape mwanao unakata fimbo unachapa bila kuhoji, wasikilizeni sana watoto wenu mtokapo kazini wana mengi ya kuwambia, jenga urafiki na watoto wako ili waone urahisi wa kukueleza kero zao na masaibu wanayopata kutoka kwa mama zao wa kambo, usiwe mtemi kwa wanao yapo mengi maovu wanayopitia ila kwasababu ya utemi wako wanafanya siri wakiamini wewe na mkeo ambaye ni mama yao wa kambo lengo lenu ni moja.
NB. Mama wa kambo, uchungu unaopata kwa mwanao tambua hata mama wa huyo mtoto unayemtesa alikuwa nao kwa mwanae hivyo basi thamini uchungu wa mwanamke mwenzio kwa mtoto wake.