Makumbusho zenye miundombinu bora

Makumbusho zenye miundombinu bora

Damaso

JF-Expert Member
Joined
Jul 18, 2018
Posts
6,132
Reaction score
10,514
Maisha kwa kawaida hayana utamu endapo ukitamani kujua ni kitu au vitu gani vitatokea sekunde zijazo, bali kufahamu matukio yaliyopita haswa matukio ya kihistoria basi huleta dhana kubwa sana ya kuongeza maarifa aidha kwenye Nyanja ya kijamii, kiuchumi, kimazingira na kadhalika. Ukiachana na darasani ambapo ni moja ya sehemu ambayo unaweza kujipatia maarifa, basi kuna sehemu moja muhimu sana kwa kila nchi. Ni kawaida kwa dunia ya sasa kukutana na nchi zenye sehemu hizi zaidi ya moja. Sehemu hii sio ngeni masikioni kwa watu, bali ni Makumbusho.

Makumbusho zinabeba mengi sana, iwe ni makumbusho binafsi, kisayansi, kivita, kimazingira au ya kitaifa, basi makumbusho ni sehemu za kipekee sana kwa watu kujipatia maarifa makubwa. Ukienda Makumbusho ndipo utakutana na elimu kubwa sana, kwa upande wa Tanzania, wengi tumeifahamu historia pana kama sio kamili ya biashara ya utumwa, ingawa tulipokuwa mashuleni tulipata wasaha wa kujifunza kuhusu utumwa ila Makumbusho tunapata kuona kwa ukaribu sana, baadhi ya vyumba ambavyo walihifadhiwa watumwa, maeneo waliyopita.

Ingawa kwa wengi wetu huwa ni historia chungu sana kujifunza kwa ukaribu maisha ya watumwa ila hakuna namna ni moja ya njia ya kuelimika zaidi.
Basi uongozi wa makumbusho hizi ukaona ni vyema waweke historia na nyaraka hizi mahala ambapo ni salama, na sio salama tu bali mahala panapovutia, tena mahala ambapo majengo yake tu yatatosha kukutoa mate ya hamu kutamani kuingia kushuhudia vitu vilivyomo humo ndani. Kwa bara la Ulaya, Makumbusho nyingi zimebeba heshima kubwa sana kuanzia nje ya majengo, yaani historia inaanzia nje kabsa hujaingia ndani, vivyo hivyo kwa makumbusho zilizopo Amerika pamoja na baadhi ya nchi za Afrika.
Kutokana na mfumo jumuishi wa taaluma mbalimbali haswa utunzaji wa kumbukumbu pamoja na taaluma za Uandisi na Usanifu wa Majengo basi dunia ikapata bahati sana kuwashuhudia wasanifu majengo wakubwa duniani wakionesha ubabe na utashi wao kwenye kusanifu makumbusho kubwa duniani. Mfano, David Chipperfield, Tadao Ando, Frank Genhry, Iwaan Baan, Hiroshi Sugimoto pamoja na Preston Scott Cohen.

Nikipata pesa nyingi za kutosha basi natamani sana miguu yangu ifike na kukanyanga makumbusho hizi kumi ambazo kwa mitazamo wangu tu naona mazingira yake pamoja na elimu zitauburudisha sana moyo wangu.

1 – The Guggenheim Museum, Bilbao, Spain
Mwendo wa masaa manne kwa treni kutoka Mji Mkuu wa Uhispania, Madrid basi unafiki pale kwenye mji wa Bilbao ambapo ndo makao makuu ya timu maarufu na bora ndani ya ligi kuu ya Uhispania, LA LIGA, hapa ni kwenye makumbusho ya Guggenheim, ambayo ni makumbusho picha kutoka kwa wachoraji magwiji duniani, mpaka picha bora kabsa kutoka kwa Vasily Kandinsky ipo pale. Pia Guggenheim ni makumbusho ambayo inatoa kozi ya muda mfupi kwenye somo adhimu la Sanaa za Kisasa, pia kuna maonyesho pamoja na semina.

ATTACH]


Ukifika mlangoni tu basi Makumbusho hii itakusalimia tu, ni Guggenheim ambayo jengo lake tu ni kazi bora sana ya kisanaa, shukrani nyingi ziende kwa msanifu na mhandisi wa majengo nguli, bwana Frank Gehry.

2 – Moscow State Historical Museum, Moscow, Urusi
Nikimalizana na makumbusho ya Guggenheim basi naenda mpaka kwenye ardhi ya Rais Vladimir Putin kwenye makumbusho ya Moscow State Historical Museum, Makumbusho ya Taifa ya Historia. Ni mwendo wa dakika arobaini na tano kutoka St. Petersburg mpaka makumbusho hii ukitumia treni ambapo ni umbali wa kilomita zaidi ya 702, lakini ukitumia huduma ya basi jiandae kuchukua masaa tisa na nusu. Ndani ya makumbusho hii kuna hifadhi ya mali kale kutoka nyakati za zamani sana, mali kale ambazo zilipatikana kwenye ardhi ambayo kwa sasa ni Urusi.

ATTACH]


Ukiachana na mali kale, Moscow State Historical Museum kuna picha zaidi ya milioni tano, picha ambazo zimekusanywa kuanzia karne ya 19. Moscow State Historical Museum inapatikana kati kati ya makutano ya Moscow’s Red Square pamoja na makutano ya Manege Square. Ukifika ndani tu utakaribishwa na picha kubwa sana yenye kuonesha mtiririko wa watawala wa Urusi, kisha ukienda chini zaidi kuna picha zenye kuonesha mabadiliko na maendeleo ya mwanadamu. Jengo lake tu nalo ni kazi ya sanaa, huku likitiwa nashi na rangi nyekundu iliyokoza, Kumbuka kuwa Moscow State Historical Museum ilifunguliwa mwaka 1872.

3 – Hermitage Museum, St. Petersburg, Urusi
Bado nitasalia Urusi na nitaunganisha safari na kwenda mpaka huko St. Petersburg ambako nakutana na Makumbusho ya kipekee sana ya Hermitage. Makumbusho hii ilianza kazi rasmi mwaka 1764, huku watu wakiamini kuwa makumbusho hii ndo makumbusho ya pili kwa ukubwa duniani.

ATTACH]


Ukitazama tu jengo lake unaweza kukubali au kukataa! Makumbusho ya Hermitage ina vyumba zaidi ya elfu sitini, na kazi za sanaa zaidi ya milioni tatu kwenye eneo lenye mita za mraba laki mbili na elfu thelathini ambazo zinatosha kusema kuwa Makumbusho ya Hermitage kuwa hii ndo makumbusho ya kwanza kwa kuwa na hifadhi kubwa hususani katika upande wa picha huku kukiwa na picha zaidi ya elfu ishirini na tano. Moja kati ya kazi bora sana zinazopatikana humo ndani ni kazi ya Leonardo da Vinci ya Madonna Litta pamoja na kazi ya Rembrandt ile ya Danae.

4 – Doge’s Palace, Venice, Italy
Nikitoka Urusi naruka moja kwa moja mpaka Italia ambapo nitaangalia mechi kadhaa za Ligi kuu ya Seria A kisha mwili ukitulia naelekea mpaka mji wa Venice ambapo nitakwenda kwenye Makumbusho ya Doge’s Palace. Jengo hili lilijengwa kati ya karne ya kumi mpaka kumi na moja huku nia ya kujengwa kwake ikiwa ni kutumika kama ngome. Lakini miundombinu hii ilivutia sana kiasi kwamba ilibadilishiwa majukumu na kufanya kasri ama jumba la kifalme wakati huo ikiwa ni karne ya kumi na mbili.

ATTACH]


Sasa humo ndani kuna kazi za sanaa bora sana, kama picha za Titian pamoja na Veronese. Lakini pia watalii hupata nafasi ya kuwa na ziara ambayo huishia kwenye chumba ambacho kilitumika kama jela huko chini.
Ila binafsi natamani sana nifike kuona ile kazi bora za uandisi iitwayo Bocca di Leone, ambayo ni sanduku la barua ambalo limejengwa kwa mfano wa kichwa cha simba dume. Pia sitopata taabu sana kwani nikimaliza kupiga misele ndani ya Doge’s Palace nakwenda kuangalia mechi za ligi ya Seria A pamoja na Seria B.

5 – Museu do Amanhã, Rio de Janeiro, Brazil
Nikimalizana na purukushani za Italia basi nachukua safari yangu navuka nchi nyingi tu na ninahama bara la Ulaya na kueleka bara la Amerika ya Kusini pale kwenye ardhi ya mafundi na wakongwe wa kucheza soka, Ronaldinho, Ronaldo, Romario, Neymar na ninafikia kwenye jiji la Rio de Janeiro ambapo nitaelekea moja kwa moja mpaka makumbusho ya Amanhã, pale kwenye viunga vya Pier Maua, makumbusho ya Sayansi.

ATTACH]


Kwa mpenzi wa maendeleo ya sayansi basi makumbusho hii itakupa mwanga halisi wa dunia inapoelekea haswa. Nitashangaa sana majengo yake huku nikiburudika na mambo ambayo yanazalishwa na michakato ya kisayansi. Usanifu wa majengo yake kwa hakika ni moja kati ya usanifu wa kipekee sana. huku ikionekana kama makumbusho ya kipekee iliyoweza kutumia sayansi na teknolojia vyema.

6 – Kunsthistorisches Museum, Vienna, Austria
Nikimaliza kutalii kwenye mji wa Rio de Janeiro kwa kupasua mipira nitakayokutana nayo mtaani basi natoka zangu mpaka uwanja wa ndege na ninaruka mpaka Austria kwenye mji wa Vienna katika makumbusho ya Kunsthistorisches, makumbusho bora na mahususi kwa Wapenzi wa kazi za sanaa.

ATTACH]


Shukrani kwa usanifu bora wa makumbusho hii kutoka kwa Gottfried Semper, kwa namna alivyosanifu makumbusho hii hakika ni lazma ubakie mdomo wazi kwa mshangao mkubwa.

Ukiwa ndani utapata wasaha wa kipekee kutazama na kufurahi utashi na ustadi wa kiwango cha ju cha uchoraji wa picha kwenye enzi mbalimbali, lakini kazi ambayo natamani sana kuitazama kwa ukaribu ni kazi kutoka kwa Diego Velázquez ile picha ya Infanta Margarita Teresa. Mbali na picha hii, pia makumbusho hii ina hifadhi ya mali kale kutoka Misri kama vile majeneza, vidani vya thamani haswa dhahabu na fedha, pia kuna mali kale kutoka Ugiriki pamoja na Rumi. Makumbusho hii ina maktaba kubwa yenye vitabu vya kale, pia makumbusho hii ina hifadhi ya sarafu zaidi ya laki sita.

7 –Musee du Louvre, Paris, Ufaransa
Nikimalizana na Austria naruka kidogo mpaka Ufaransa nakwenda kwenye Jiji kubwa la Paris, kisha napumzika kidogo na kwenda kuangalia mechi moja ya Ligi Kuu ya Ligue 1, kufurahia harakati za Lionel Messi kwenye uwanja wa Parc de Princes kisha asubuhi na Mapema naanza na Makumbusho bora sana ndani ya Ufaransa, hii ni makumbusho ya Louvre, huku Wafaransa wao wakisema ni Musee du Louvre, basi ukiachana na ule mnara mkubwa na mrefu wa Eifel Tower ambapo pia nitanyoosha shingo juu kama nahesabu nyota, basi makumbusho hii ni ya kipekee sana ndani ya Ufaransa na Jiji la Paris.

ATTACH]


Makumbusho hii Mwanzoni kabsa ilitumika kama ngome wakati wa utawala wa Mfalme Philippe Auguste huku ikiwa inafanya kazi sambamba na kasri la Mfalme huku ikiwa pia ni makazi ya wafalme wa Ufaransa wakati wa Ufalme wa Mfalme Henri IV mwishoni mwa karne ya kumi na sita. Kuna hifadhi ya vitu vingi kutoka Misri, Ugiriki, pamoja na Roma hata baadhi ya vitu kutoka karne ya kumi na tisa.

Lakini kama hufahamu ni kuwa Musee du Louvre ndo makumbusho kubwa ya sanaa duniani, na ukiachilia mbali urembo na ustadi wa usanifu wa makumbusho hii, humo ndani ndo kutakufanya urudi tena kufanya utalii. Musee du Louvre ndo maskani ya kudumu ya kazi za sanaa kubwa na maarufu duniani, kazi kama Sanamu la Aphrodite pamoja na picha tamu sana ya Mona Lisa iliyochorwa na Leonardo Da Vinci, pia kuna kazi za kukutoa hamu kabsa kutoka kwa Theodore Gericault ya The Raft of the Medusa. Natamani sana kushuhudia kazi ya The Three Graces kutoka kwa Lucas Cranach, An Odalisque kutoka kwa Jean-Auguste-Dominique Ingres, kazi za sanaa ya the Great Sphinx by Tanis, the Statue of Ain Ghazal pamoja na The Coronation of Napoleon.

8 – The Metropolitan Museum of Art, New York, Marekani
Nikitoka zangu Ufaransa nakwenda mpaka kwa Biden huko Marekani na miguu yangu inafika kwenye Jiji la raha bwana, New York pale Fifth Avenue, ambapo nakutana na Makumbusho ya Jiji ya sanaa ya Metropolitan Museum of Art, makumbusho ambayo ni moja ya makumbusho kubwa duniani, na moja kati ya vivutio vikubwa ndani ya Jiji la New York. Ni makumbusho iliyofunguliwa mwaka 1872, na mpaka sasa makumbusho hii inahifadhi kazi za sanaa zaidi ya milioni mbili kutoka kila kona ya dunia.

ATTACH]


Sanamu za zamani mpaka picha kutoka kwa magwiji wa sanaa ya uchoraji kutoka Ufaransa na Italia, mpaka wasanifu wa vinyago na Sanamu kadha wa kadha. Metropolitan Museum of Art inatoa nafasi ya kipekee sana ya kutazama kazi kutoka kwa mafundi haswa wa sanaa, huku ikiwa ni kawaida kwa maonyesho mbalimbali yanayofanyika ndani ya Metropolitan Museum of Art kuvunja rekodi. Nikifika humo natamani sana kutazama picha iliyochorwa na Andrea del Verrocchio hii ni picha ya Madonna, pia natamani kuona ile picha ya The Abduction of the Sabines kutoka kwa mchoraji Nicolas Poussin.

9 – Niterói Museum of Art, Rio de Janeiro, Brazil
Baada ya kutembelea makumbusho ya Metropolitan Museum of Art huko New York, Marekani nitarejea Brazil kwenye Jiji la Soka, Jiji la Rio de Janeiro mpaka pale kwenye Makumbusho ya d'Orsay, ambayo ni mahala panapoonesha ustadi wa usanifu wa majengo haswa huku makumbusho hii ikiwa ni kitu cha kujivunia sana kwa wakazi wa Rio de Janeiro.

ATTACH]


Makumbusho hii ilifunguliwa rasmi mwaka 1996, na shukrani nyingi ziende kwa mhandisi Oscar Niemeyer ambaye alifanya kazi bora sana kutengeneza muonekano wa makumbusho hii. Humo ndani kuna kazi za sanaa zaidi ya elfu moja na mia tano kutoka kwa wasanii wa Kibrazili wa karne ya ishirini, huku kivutio kikubwa ikiwa ni kazi bora kutoka kwa gwiji wa sanaa huyu ni João Sattamini.

10 – Museum of Islamic Art, Doha, Qatar
Natoka zangu Brazil na kueleka kwa masheikh pale kwenye Qatar kujiandaa na harakati za kuangalia kombe la dunia la mwaka 2022, lakini kabla ya hayo yote nitaruhusu miguu na akili yangu kuelekea kwenye Makumbusho ya Sanaa za Kiislamu iliyopo pale kwenye Jiji la Doha, Qatar.

ATTACH]


Natamani sana kushuhudia makumbusho hii ambayo ilisanifiwa vyema sana na Mhandisi IM Pei, ambaye alipata wazo la kutengeneza makumbusho hii kutokana na muonekano wa Msikiti wa Ibn Tulun wa pale Cairo, Misri. Ni makumbusho ambayo inahifadhi vyombo vya udongo, chuma, na vioo ambavyo mtu anaweza kuviona kwenye makabati ya vioo.

11 – National Gallery, London, Uingereza
Huko London kuna Makumbusho ya kipekee sana ni makumbusho ya National Gallery ambayo mwanzo yalikuwa ni makazi ya mchoraji wa nyumba aitwaye Argerstein, makumbusho hii ni moja kati ya makumbusho ambazo hupokea watu wengi sana ndani ya Jiji la London. Ni makumbusho yenye hifadhi ya kazi za sanaa nyingi sana, zaidi ya picha elfu mbili na mia tano ambazo zilipata kuchorwa kuanzia mwaka 1250 mpaka 1900.

ATTACH]


Humo ndani natamani sana kuona picha The Raising of Lazarus iliyochorwa kiustadi na Sebastiano del Piombo, pia ile picha ya The Madonna of the Pinks iliyochorwa vyema sana bwana Raphael pia ile picha ambayo imewaacha watu hoi kwa ufundi wake bwana mkubwa Leonardo da Vinci ya The Virgin and Child with Saint Anne and Saint John the Baptist.

12 – National Museum of Holland, Rijksmuseum, Amsterdam, Uholanzi
Mwisho kabsa nitaelekea mpaka Uholanzi kwenye Jiji la Amsterdam katika makumbusho ya Taifa ya Rijksmuseum, ambayo ina hifadhi ya kazi za sanaa zaidi ya elfu nane ambazo zinaonekana katika vyumba themanini, picha hizi hutoa ujumbe na mtiririko wa hadithi ya Wadachi ya miaka mia nane katika Nyanja za Sanaa pamoja na historia.

ATTACH]


Lakini macho na moyo wangu utakuwa ukiangalia na kushangaza picha ambazo zimechorwa kwenye kizazi cha dhahabu cha wadachi, kama picha ya The Night Watch kutoka kwa mchoraji Rembrandt pamoja na picha ya The Milkmaid iliyochorwa na Vermeer.

Hizi ni makumbusho kumi na mbili ambazo nikipata uwezo mzuri wa kifedha pamoja na afya njema basi nitakwenda kushangaza shangaa. Maana zamani wahenga walisema “Mkaa bure si sawa na mtembea bure”, ni utamaduni wangu sana kupenda kujifunza kuhusu vitu vingi. Kama ni kitu ambacho kimepewa nafasi na moyo wangu basi nitafanya niwezalo ili niweze kulisoma na kulielewa vyema. Nimeweka orodha sio kwa maana ya kukejeli makumbusho ambazo zinapatikana ndani ya bara letu ama wengine wanavyosema kuwa nimekengeuka ila kitu Kizuri kisifie ili tujue ni wapi tunatakiwa kurekebisha. Dunia ya sasa imeendelea kubadilika tena kwa kasi kubwa, hivi sasa kutafuta mali kale sio tatizo ila tatizo ukishazipata hizo mali kale, je una uwezo wa kuzitunza zikadumu miaka mingi baadaye.

ATTACH]


Kuna mhadhiri mmoja kutoka Chuo Kikubwa nchini aliwahi kusema “Kuna vitu vingi sana vipo kwenye ardhi na hata kwenye maji na vimeendelea kudumu ila vikishatolewa maeneo yake basi vinaharibika kwa kasi sana. Kwa wenzetu wamewekeza sana kwenye kutafuta teknolojia bora za kutunza vitu hivi, na ndo maana ni rahisi kukutana na picha nyingi za kale kutoka Afrika ambazo zimekaa kwenye Makumbusho kubwa, hata tukizihitaji turudishiwe, swali linarudi, Je tunaweza kuzitunza zisiharibike, achilia mbali wizi na tabia zisizo na busara baina yetu. Watu kuingia na Vyakula ama vinywaji ndani ya Makumbusho kwa kigezo cha wao kuwa ni wafanyakazi. Hii ni sawa na kile kisa cha Afisa Misitu kulazimisha kuingia kwenye hifadhi ya mizinga ya nyuki wakati ambao nyuki wanaweza kukuletea madhara.

ATTACH]


Je makumbusho ipi imekupa msisimko? Ni makumbusho ipi tunaweza kuchukua mfano na kutengeneza makumbusho ya namna hiyo hapa kwetu, naomba nikaribishe mjadala!
Asante kwa muda wako!
Naomba kuwasilisha Andiko!
 

Attachments

  • images%20(35).jpg
    images%20(35).jpg
    58.3 KB · Views: 25
  • images%20(36).jpg
    images%20(36).jpg
    47.7 KB · Views: 24
  • images%20(37).jpg
    images%20(37).jpg
    89.5 KB · Views: 20
  • images%20(38).jpg
    images%20(38).jpg
    47.6 KB · Views: 25
  • images%20(39).jpg
    images%20(39).jpg
    67.6 KB · Views: 24
  • images%20(40).jpg
    images%20(40).jpg
    113.1 KB · Views: 28
  • images%20(41).jpg
    images%20(41).jpg
    51.8 KB · Views: 27
  • images (42).jpg
    images (42).jpg
    78.2 KB · Views: 31
  • images%20(35).jpg
    images%20(35).jpg
    58.3 KB · Views: 19
  • images (36).jpg
    images (36).jpg
    47.7 KB · Views: 25
  • images (38).jpg
    images (38).jpg
    47.6 KB · Views: 23
  • images (44).jpg
    images (44).jpg
    30.9 KB · Views: 28
  • images (41).jpg
    images (41).jpg
    51.8 KB · Views: 28
  • images (40).jpg
    images (40).jpg
    113.1 KB · Views: 30
  • images (37).jpg
    images (37).jpg
    89.5 KB · Views: 18
  • images (38).jpg
    images (38).jpg
    47.6 KB · Views: 19
  • images (39).jpg
    images (39).jpg
    67.6 KB · Views: 21
  • images (40).jpg
    images (40).jpg
    113.1 KB · Views: 19
  • images (41).jpg
    images (41).jpg
    51.8 KB · Views: 22
  • images (42).jpg
    images (42).jpg
    78.2 KB · Views: 19
  • images (43).jpg
    images (43).jpg
    56.1 KB · Views: 19
  • images (44).jpg
    images (44).jpg
    30.9 KB · Views: 18
  • images (45).jpg
    images (45).jpg
    68.4 KB · Views: 18
  • images (46).jpg
    images (46).jpg
    65.4 KB · Views: 23
  • images%20(49).jpg
    images%20(49).jpg
    64.2 KB · Views: 23
  • images%20(48).jpg
    images%20(48).jpg
    33.1 KB · Views: 19
Back
Top Bottom