Majangili wajipanga kumyumbisha Magufuli

Halisi

JF-Expert Member
Jan 16, 2007
2,802
614
Majangili wajipanga
kuiyumbisha serikali

.Wapenyeza kwa wanasiasa na watendaji
.Watengeneza propaganda kujilinda
.Wakumbushia walivyoizima 'tokomeza'
.Wajihami 'utumbuaji majipu' usiwakute

WAKATI serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikitangaza kupambana na majangili, imeelezwa kwamba kwa kutumia mtandao wao wa 'kimafia' majangili hao wanajipanga kuitikisa serikali bungeni na hata nje ya bunge.

Uchunguzi wa KULIKONI umebaini kwamba mikakati hiyo inaandaliwa ili kuiyumbisha serikali ishindwe kukabiliana na vitendo vya ujangili kwa kasi sawa na vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma katika mtindo uliopewa jina la 'utumbuaji majipu'.

Taarifa za hivi karibuni kutoka kwa watu walio karibu na makundi ya baadhi ya majangili zimeeleza kwamba mikakati yao imekwisha kuanza na wanafanya marejeo ya walivyofanikiwa kuzima mapambano dhidi ya ujangili yaliyopewa jina la 'operesheni tokomeza' na kusababisha kung'oka kwa mawaziri wanne wa serikali ya awamu ya nne.

"Wanasema kama waliweza kuwang'oa mawaziri wakati ule kwa kuhamisha makosa ya wachache kuvuruga na vita dhidi ya ujangili kuwa uhalifu kwanini washindwe sasa. Wanajitapa wameshafanikiwa kuwaingia baadhi ya viongozi wa juu wa kisiasa kwa kuwalaghai ili kuzima nguvu zozote zitakazoweza kugusa wanaofadhili ujangili," anasema ofisa mmoja wa serikali.

Ofisa huyo ambaye amewahi kuhusika moja kwa moja na ufuatiliaji wa vitendo vya ujangili, anasema wanaofadhili ujangili na majangili wakubwa wanapigana kufa na kupona wasijulikane kabisa na wana mbinu nyingi ikiwamo kuwatumia wanasiasa kujilinda ama na wao kujiingiza katika siasa kwa kugombea nafasi mbalimbali ama kufadhili watu wao.

"Baadhi wamefanikiwa kuingia katika siasa na wengine wamekwishapenya na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za kisiasa na wengine wamefadhili watu wao ambao wanatii maelekezo yao. Wengine wanatengeneza propaganda zinazosaidia kupotosha hata wadau na viongozi wenye nia na mapenzi mema kwa umma na rasilimali za Taifa," anasema.

Akizungumza bungeni hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema;

“Nchi yetu inakabiliwa na tatizo la ujangili hasa wa tembo, faru na biashara haramu ya nyara za serikali. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ilizindua mkakati wa kupambana na ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali ulioanza kutekelezwa mwaka 2015, kwa kuchukua hatua mbalimbali.

“Hatua hizo ni pamoja na kutumia vifaa na teknolojia ya kisasa kama vile ‘Geographical Information System – GIS’ na ‘Global Positioning System – GPS,’ kuimarisha mfumo wa mawasiliano ya radio kutoka mfumo wa analogia kwenda kidigitali; na kuanza kutekeleza mpango wa kikanda wa kukusanya taarifa za kiintelijensia zinazoongoza doria katika kukamata watuhumiwa na wahalifu.

“Serikali ya Awamu ya Tano, itahakikisha ujangili huu unakomeshwa haraka. Nichukue fursa hii, kuziomba jamii zinazozunguka hifadhi zetu kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali katika vita hii.”

Hata hivyo, baadhi ya watendaji wa serikali wakiwemo wabunge na hata wakuu wa wilaya wameelezwa kushutumu vyombo vya dola vinavyofuatilia taarifa za majangili ikiwamo kuchunguza watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na wale wanaozikodisha kwa majangili.

Katika tukio la hivi karibuni, mmoja wa wakuu wa wilaya moja katika mikoa ya kanda ya ziwa, ametajwa kuwalaumu polisi na uongozi wa mkoa wake kwa kile alichodai kufanya operesheni bila kumshirikisha yeye na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) badala ya kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na wenzake kukamata watuhumiwa na silaha zao.

"Nimeshitushwa sana na kauli ya DC kusema kwamba hana uhusiano mzuri na uongozi wa mkoa hasa polisi kwa kuwa waliingia ndani ya wilaya yake na kukamata watuhumiwa bila kushirikisha wilaya. Ingekua ni ziara ya kutembelea angekua sahihi lakini upelelezi na ukamataji huwezi kujulisha kila mtu. Huyu kuna siku atalaumu ziara za kushitukiza.

"Upelelezi wa mambo mazito kama ujangili mara nyingi huwa hatutoi taarifa kabla ya kujiridhisha tumefanikisha kupata walipo wahalifu. Sasa kama DC anaweza kulaumu watendaji wenzake wa serikali kwenye vyombo vya habari hastahili kabisa kufanya kazi serikalini.

"Sisi ndani ya serikali ni wamoja bila kujali taasisi zetu sasa ni hatari kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama anatuhumu polisi na kuchochea wananchi badala ya kuwatuliza. DC anaposukuma wananchi walalamike eti wametishwa na polisi huyo ni wa kumuangalia vyema. Nadhani ndio maana Rais John Magufuli anasita kutangaza Ma DC wapya maana anaona kuna majipu kibao," anasema.

KULIKONI imewahi kuripoti kwamba majangili na maswahiba zao wamekua wakitumia ng'ombe katika kukwamisha juhudi za serikali na wadau wa vita dhidi ya ujangili.

Uchunguzi wa muda mrefu umebaini kwamba, kumekua na mkakati wa muda mrefu
unaohusisha wahusika, wafadhili na wanufaika wa ujangili katika kutumia wafugaji katika kuzuia juhudi za uhifadhi wanyamapori na kuzuia na kupambana na ujangili.

Rais Magufuli John Mafufuli ameteua Majenerali kuongoza Wizara za Maliasili na Utalii na Wizara na Mambo ya Ndani, ikielezwa ya kuwa amedhamiria kwa dhati kukabiliana na ujangili na uhalifu wa aina zote.

Majenerali hao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ni Jaji Meja Jenerali Projest Rwegasira, ambao kwa mara ya kwanza walishirikiana kuwakamata majangili walioua tembo watatu na kutungua helikopta katika pori la Mwiba wilayani Meatu.

Hata hivyo, pamoja na dhamira njema ya serikali na wadau wa uhifadhi
wanyamapori na mazingira, inaelezwa kuna mkakati unaohusisha wanasiasa
wenye maslahi katika ujangili wakiwamo wabunge ambao wanawatumia wafugaji
wa ng'ombe kwa kuwahamasisha wazidi kuvamia mapori ya akiba ili yasiwe na
udhibiti wowote.

Uchunguzi umebaini kwamba kuna wabunge wenye maslahi na ujangili ambao
wamekusanya fedha nyingi kutoka kwa baadhi wafugaji ambao wameelezwa kuchangishwa wastani wa shilingi 500,000 kwa kila kaya yenye mifugo ili kufanikisha mikakati hiyo.

Mbali ya wanasiasa, wahusika wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwamo kufadhili taarifa katila vyombo vya habari zenye lengo la kuvuruga vita dhidi ya ujangili.

Serikali imekuwa ikifanya uchunguzi na msako wa majangili kwa kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama na wadau wengine wa maliasili, utalii na mazingira, juhudi ambazo zimekuwa zikivurugwa mara kwa mara na genge la kimafia la majangili na wafuasi wao.

Vitendo vya ujangili duniani vinatajwa kuwa na mahusiano ya karibu na ugaidi, biashara ya dawa za kulevya na utakatishaji wa fedha haramu, vitendo ambavyo kwa kiasi kikubwa huhusisha rushwa kubwa inayopenya hadi kwa wanasiasa na watendaji wazito.

Vitendo hivyo pia huweza kuhatarisha maisha ya watu wanaofuatilia na hata kuhatarisha amani na usalama wa Taifa ikiwa wahusika na mtandao wao hawatadhibitiwa

Source: Kulikoni, Ijumaa, Mei 6, 2016
 
Back
Top Bottom