Majaliwa: Agizo la kulipa kodi halimaanishi adhabu

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa agizo la Rais John Magufuli kutaka kila mmoja alipe kodi halina nia ya kuadhibu, bali kutukumbusha wajibu wa kulipa kodi na kufanya kazi.

Alisema ili kutimiza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni, ni lazima nchi iwe na rasilimali fedha za kutosha kuwezesha kutekeleza miradi iliyojipangwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, katika mkutano mkuu wa Jukwaa la Maendeleo mkoani Rukwa na Katavi, Majaliwa alisema ni vema kila mmoja aone umuhimu wa kutimiza wajibu na kuchangia ili kupata fedha za kutosha.

Alisema kazi waliyonayo sasa ni kukusanya mapato zaidi kwa lengo la kukamilisha miradi iliyokuwepo na kuwataka Watanzania kubaini wakwepa kodi, ili wachukuliwe hatua stahiki.

“Rais amekuwa akiomba kila Mtanzania kumsaidia katika kukusanya mapato. Hii haimaanishi kwamba anawaadhibu bali ni kuwakumbusha wajibu wa kufanya kazi na kulipa kodi,’’ alisema Majaliwa. Alisema, kila mfanyabiashara, mkulima, mfanyakazi, mwanafunzi na watoa huduma za jamii, wanatakiwa kulipa kodi kulingana na kipato cha kila mmoja.

Alisisitiza kuwa, kila mmoja anapaswa kuwajibika katika masuala ya ulipaji wa kodi na Serikali itatekeleza waliyojipangia na matatizo yaliyokuwepo yatapungua. Akitolea mfano wa viwanda, Waziri huyo alisema kuwa, endapo wafanyakazi wa viwandani watachakata bidhaa zenye ubora na viwango, wakizipeleka nje ya nchi wataongeza mapato.

Pia alisema, zipo biashara za magendo ambazo zinaingia nchini bila ya kulipiwa kodi, hivyo ni vyema Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Vijiji kushirikiana kutambua wafanyabiashara ambao wanapotezea Taifa mapato yake.

“Ni nafasi sasa ya kubadilika kwa kuacha kufanya shughuli kwa mazoea na kukaa kwenye vijiwe. Mikoa ambayo wananchi wake wakiamka wanacheza bao na karata, ni tofauti na Mikoa ambayo wananchi wake wanafanya kazi,’’ aliongeza.

Kwa mujibu wa Majaliwa, mtu yeyote asikubali kupotezewa muda bali ajenge utamaduni wa kufanya kazi na kwamba mabadiliko yenye tija yataonekana. Alisema, watahakikisha wanatimiza ahadi ya Serikali ya kuanza ujenzi wa reli kwa kushirikiana na sekta binafsi itakayotoka Kaliua- Mpanda na Karema.

Pia alisema, Serikali itakamilisha barabara ya Sumbawanga- Kayuni hadi Nyakunazi yenye Kilometa 562, barabara ya Matai- Kasesya; Kibaoni-Majimoto hadi Inyonga na barabara ya Ipole, Koga hadi Mpanda yenye kilometa 255.

Alisema wataanza ujenzi na ukarabati wa barabara za Tabora- Ipole-Koga hadi Mpanda yenye kilometa 359. Kwa upande wa huduma za jamii, alisema watahakikisha kila zahanati inapata dawa kwani awali Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD), ilikuwa inatumia fedha nyingi kununua dawa kwa mawakala hivyo wameweka mikakati ya kununua dawa kwenye vyanzo husika.

Hata hivyo alisema, suala la elimu bure linatakiwa kutiliwa maanani kwamba hakutakuwa na michango yoyote ya mitihani katika shule za kutwa na bweni, ada pamoja na michango mingine.

Aliwahakikishia Watanzania kuwa, viwanda vilivyopo vitafufuliwa kwa lengo la kuimarisha utengenezaji ajira kwa vijana. Katika hatua nyingine, alimpongeza Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda kwa kuwa katika orodha ya viongozi waliotumikia nchi kwa ufanisi na kiongozi aliyetukuka.
 
Rais, mawaziri na wabunge nao wana wajibu wa kulipa kodi kwenye mishahara na posho wanazo zipata kama raia wengine. Sio kutuhubiria kulipa kodi wakati ninyi mna kwepa kulipa kisheria
 
Back
Top Bottom