Kurzweil
JF-Expert Member
- May 25, 2011
- 6,622
- 8,410
Rais wa Iran Hassan Rouhani na mwanasiasa mwenye msimamo mkali Ebrahim Raisi wameidhinishwa kuwania uchaguzi wa urais mwezi ujao nchini humo, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Rais wa zamani Mahmoud Ahmadinejad hata hivyo amezuiwa kuwania na jopo hilo linalowachuja wagombea ambalo linadhibitiwa na serikali.
Mshirika wa karibu wa Ahmadinejad Hamid Baghaie pia amezuiwa kugombea urais.
Orodha kamili ya wagombea kwenye uchaguzi huo wa tarehe 19 Mei itatangazwa 27 Aprili.
Wagombea zaidi ya 1,600 walitaka kuwania lakini ni sita pekee ambao walichaguliwa na Baraza Kuu la Walinzi.
Kuidhinishwa kwa Bw Rouhani na Bw Raisi kunatarajiwa kusababisha mvutano mkali wa kisiasa kati ya kambi zao mbili.
Bw Rouhani alichaguliwa kwa kura nyingi mwaka 2013, ambapo aliahidi kufikisha kikomo kutengwa kwa taifa hilo kidiplomasia katika jamii ya kimataifa na kuhakikisha uhuru zaidi wa kijamii.
Miaka miwili baadaye, serikali yake na nchi nyingine sita za Magahribi zilifikia mkataba wa kihistoria kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambapo Iran ilikubali kusitisha mpango wake wa kustawisha silaha za nyuklia na mataifa ya Magharibi nayo yakaondoa vikwazo.
Bw Raisi ni seyed, mtu ambaye anaweza kufuata historia ya ukoo wake hadi kwa Mtume Muhammad.
Ana sifa za kuwa na msimamo mkali kuhusu masuala mengi muhimu na inadaiwa anaungwa mkono na Kiongozi Mkuu wa Kidini Ayatollah Ali Khamenei.
Ahmadinejad, ni mtu pia mwenye msimamo mkali ambaye alihudumu kwa mihula miwili kama rais kati ya 2005 na 2013.
Alishangaza wengi alipojiandikisha kuwa mgombea wiki iliyopita licha ya kushauriwa na Khamenei asiwanie.
Wengine wanaowania ni Mostafa Mirsalim, meya wa Tehran Mohammad Bagher Ghalibaf, Mostafa Hashemitaba na Makamu wa Rais Eshaq Jahangiri.
Chanzo: BBC Swahili