Mafuta ya kula nayo bei juu

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,287
Mafuta.jpg

Wakati Watanzania wakiendelea kuumia na bei ya juu ya sukari, sasa watalazimika kutoboa zaidi mifuko yao kununua mafuta ya kupikia.


Utafiti uliofanyika katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam umeonyesha kuwa lita moja ya kiungo hicho cha chakula inauzwa kati ya Sh2,800 hadi Sh3,000 kutoka Sh2,500 ya awali.

Wafanyabiashara walieleza kuwa wananchi wanashtuka bei hiyo sasa, lakini ilianza kupanda taratibu tangu Machi wakituhumu kuwa hali hiyo imesababishwa na hatua ya Serikali kuzuia mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi.

Serikali imekana madai hayo ikieleza kuwa zuio lolote la bidhaa ni lazima litangazwe wazi.

Mfanyabiashara wa bidhaa za jumla Manzese, Andrea Uiso alisema katoni ya mafuta ya Korie ya lita tatu inauzwa kati ya Sh 49,000 hadi Sh50,000 kutoka kati ya Sh37,000 hadi 42,000 ya awali.

Cosmas Laswai, muuza duka la rejareja Buguruni Rozana alisema sasa wanalazimika kuuza Sh2,800 kwa lita moja baada ya kununua mafuta hayo kwa bei ya jumla ya Sh51,000 ili kufidia hasara.

“Nilipowauliza sababu ni nini wenye maduka ya jumla walinijibu kuwa baadhi ya kampuni wanazochukua bidhaa hii walikuwa wanasafisha visima vyao vya mafuta ndiyo maana kitu kama hiki kimetokea,” alisema Laswai.

Laswai alishauri Serikali kuhakikisha inazuia mfumuko wa bei ili kukabiliana na hali hiyo, kwani wao hawapendi kuuza bidhaa kwa bei ya juu, lakini mazingira yamelazimisha.

Mfanyabiashara wa chips Ilala Bungoni, John Samwel alisema kupanda kwa bidhaa hiyo kumewathiri kibiashara na kwamba hali ikiendelea hivyo watalazimika kupandisha bei ya chips kavu kutoka Sh1,500 hadi Sh2,000 kwa sahani.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage alimwambia mwandishi kwa simu kuwa hajui kama bei ya bidhaa hiyo imepanda, wala Serikali haijapiga marufuku mafuta kutoka nje ya nchi.

“Kwanza sijui kama bidhaa hiyo imepanda. Halafu Serikali ikitaka kupiga marufuku kitu chochote lazima itangaze kwenye vyombo vyake ikiwamo gazeti, hivyo hakuna taarifa kama hizo,” alisisitiza Mwijage.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasindikaji wa Mafuta ya Alizeti Tanzania, Ringo Iringo alieleza kushangazwa na upandaji bei wa mafuta hayo ambayo alidai ni yale yanayoingizwa kutoka nje ya nchi.

Alisema mafuta ya alizeti ambayo wanayazalisha hapa nchini yameshuka bei kwa sasa kutoka Sh45,000 hadi Sh41,000 kwa ndoo ya ya lita 20 kutokana na msimu huu kuwa wa mavuno.


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom